Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nami nashukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kutoa mchango wangu katika hoja iliyoko mezani ambayo ni Hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa katika vipindi viwili kwa maana ya wakati anafungua Bunge la 2015 na Bunge hili la sasa la 2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu utajikita zaidi katika eneo la diplomasia ya uchumi. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais, ametembea katika maono na dira ile ambayo ameizungumza katika hotuba zake mbili na kuonyesha umahiri na ujasiri mkubwa wa kusimamia kile ambacho anakielekeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kipindi cha miaka mitano, 2015 - 2020 Tanzania imeweza kufungua Balozi nane ambazo zinafikisha Balozi takribani 43 duniani kote. Ongezeko hili la Balozi nane kwa kipindi kifupi cha miaka mitano inaonyesha dhamira ya wazi kabisa kwamba Mheshimiwa Rais anataka sasa aipeleke Tanzania huko duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii maana yake nini? Maana yake sasa ni kwamba Wizara za kisekta zinatakiwa zifanye kazi mahsusi ili hizi Balozi ambazo tumezifungua zikawe fursa za kibiashara na fursa nyingine kutoka kwao kwa maana ya kutuletea teknolojia pamoja na mitaji. Kwa mfano, sasa hivi tumefungua Ubalozi kule Havana, Cuba, tunajua wenzetu wale ni wajuzi sana wa kilimo hasa cha umwagiliaji. Kwa hiyo, tunatarajia kuiona Wizara ya Kilimo ikifungamanisha sasa uanzishwaji wa Ubalozi Havana, Cuba pamoja na kusaidia sekta ya kilimo hapa nchini kwa maana ya kubadilishana utaalam na ujuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo hilo hilo la diplomasia ya uchumi, Mheshimiwa Rais ameahidi kwamba tunanunua ndege ya mizigo kwa ajili ya kusafirisha mazao hasa ya mbogamboga na matunda. Hii maana yake nini? Maana yake ni kwamba ni lazima sasa tujiandae kwamba hayo mazao tunayotaka yaende kwenye ulimwengu mwingine, tumeyaandaa kwa kiasi gani? Ndiyo hiyo hoja ambayo alikuwa anaizungumza Mheshimiwa Humphrey Polepole hapa kwamba ng’ombe wetu tutaendelea kuwaacha wazurure huko halafu baadaye tuseme kwamba wanaweza kwenda kushindana kwenye masoko mengine ya dunia? Ni lazima sasa Wizara zichukue hii kama changamoto ili ndege hii isije ikapaki airport haina shughuli za kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu lugha ya Kiswahili. Sasa hivi lugha ya Kiswahili ni miongoni mwa lugha 10 zinazozungumzwa zaidi ulimwenguni. Hapa kuna haja ya dhati kabisa kwa Wizara ya Elimu kupitia mtaala upya. Tunataka kukipeleka Kiswahili katika nchi za Kusini za Afrika (SADC), nchi 16. Huwezi ukapeleka Kiswahili hiki ninachozungumza hapa kwenye nchi ambazo zilikuwa zinatawaliwa na Mreno. Maana yake ni kwamba ni lazima sasa tutengeneze mtaala mpya, tuandae wataalam mbalimbali wa kusoma lugha, wawe na ujuzi wa kujua Kireno, Kifaransa, Kiingereza, Kiarabu, Kichina na lugha nyingine zote ili watakapokwenda kuipeleka bidhaa ya Kiswahili katika hayo maeneo, basi kusiwe na shida ya kuwa na ukalimani. Kwa hiyo, nawafumbua macho Mawaziri kwamba ikishazungumzwa kwenye Hotuba ya Rais sisi turudi katika sekta zetu kuchakata na kuweka hiyo mipango ili mambo haya yaweze kwenda vile ambavyo tunakusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusu biashara. Wizara ya Mambo ya Nje ina mpango wa kufungua Ubalozi Mdogo pale Lubumbash, hili ni eneo la kibiashara. Tumeona nchi yetu tunajitahidi sana katika uzalishaji, tunatakiwa tutumie fursa hii ya Balozi tunazozifungua na Balozi Ndogo kuhakikisha kwamba mazao ya Watanzania yanapata masoko. Siyo ya Watanzania tu na bidhaa zinazotoka nchi za wenzetu na zenyewe ziweze kuja hapa kwetu na kutunufaisha katika maeneo yote ya kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaposema diplomasia ya kiuchumi, hili ni jambo kubwa tunalotakiwa tulitazame kwa jicho la kimkakati. Balozi hizi nane ambazo zimeanzishwa, zote ukizipitia ni za kimkakati. Tukizungumza mahusiano yetu na Uturuki, ni eneo la kimkakati la kibiashara; tukizungumza na Algeria, ni eneo la kimkakati; tukiwaangalia Jamhuri ya Korea Kusini nalo ni eneo la kimkakati. Tusibweteke, tutumie fursa hii, tupitie upya Hotuba ya Mheshimiwa Rais, kila sekta ambayo imeguswa, basi ifungamanishe kila jambo linalopatikana kwa kuzipitia upya sera zetu na miongozo yetu mbalimbali kuhakikisha kwamba tunakwenda kuipeleka Tanzania katika uchumi huo wa kati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii. (Makofi)