Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Maryam Salum Msabaha

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kuhusu Suala la Elimu; elimu ya Tanzania bado haijaboreshwa, ni tofauti na nchi jirani. Elimu ya Tanzania inasikitisha sana, ni lazima Tanzania tuwe na elimu bora ili wananchi waweze kukabiliana na changamoto za maisha. Ni vizuri Watanzania wapate elimu bora ili kujenga Taifa la watalaam wa sayansi na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijijini hawana elimu bora, shule zipo mbali na makazi ya wananchi, hii inapelekea wanafunzi wa kike kupata mimba za utotoni kwani wanapoenda shule wanakutana na vishawishi mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanafunzi wa kike wanapata taabu sana, wanapokuwa wameingia katika hedhi; kwani shule wanazosoma hazina vyoo vizuri. Vyoo ni vibovu na pengine shule nzima hakuna, kuna vyoo viwili, kimoja wavulana na kimoja wasichana. Ni vizuri Serikali ijenge shule bora na nzuri na wanafunzi watakuwa na bidii ya kusoma na tunaweza kupata wasomi wazuri wenye vipaji mbalimbali, ambavyo vitakuwa ni muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri tupitishe Sheria Bungeni, Wananfunzi wa kike, wanapopata mimba wakiwa shuleni wapewe fursa nyingine, wanapozaa warudi tena kusoma shule au Serikali iwajengee shule maalum kama walivyofanya Zanzibar na hao wanaowapa mimba wanafunzi wachukuliwe hatua kali za Kisheria. Je, ni lini Serikali itahakikisha inarudisha shuleni wananfunzi wa kike waliopata mimba katika umri mdogo? Na ni lini Serikali itajenga shule bora vijijini wanafunzi wa kike wasipate taabu wanavyoingia kwenye hedhi pia vyoo bora iwajengee?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la Elimu ya Watu Wazima, baadhi ya wananchi wa Tanzania, ambao ni watu wazima hawajui kusoma na kuandika. Ni vizuri Serikali ikarudisha elimu hii ya watu wazima na ikafika mpaka vijijini. Wakuu wa Mikoa na Wilaya wakaratibu ni wananchi wangapi hawajui kusoma na kuandika na wakawekewa muda maalum wa kusoma. Vilevile, wapewe semina elekezi kuhusu elimu na faida ya elimu kwani katika tawala wa Rais ziliopita akiwepo muasisi wa nchi hii Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, elimu hii ya watu wazima ilikuwepo na watu wazima nao walikuwa wakisoma jioni. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha elimu hii ya watu wazima wasiojua kusoma na kuandika inarudishwa na kuboreshwa hasa vijijini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la Vyuo Vikuu ni vizuri Serikali yetu ijenge Vyuo Vikuu vingi hapa nchini ili wanafunzi wanaohitaji kusoma Vyuo Vikuu wasiende kusoma nje ya nchi kwani baadhi ya wanafunzi wakienda kusoma nje ya nchi wanakuwa wanashawishika na kuamua kufanya kazi katika nchi jirani kwani wanakuwa wana vipaji vizuri. Wanafunzi wa vyuo Vikuu wakopeshwe mikopo na hiyo mikopo isikopeshwe kwa upendeleo. Vilevile, ni vizuri Serikali iwekeze katika elimu na wanafunzi wataka kuwa na juhudi ya kusoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali, Chuo Kikuu Huria kwa tawi la Zanzibar liboreshwe, naona kama limesahulika. Wanafunzi wa elimu ya juu kwa upande wa Zanzibar, wapewe mikopo kwa wakati muafaka kwani wanafunzi wa elimu ya juu kwa upande wa Zanzibar wakitaka mikopo ni lazima wafuate Bara. Hii itasaidia kuondoa kero za Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la Walimu, walimu ni watu ambao wamesahulika! Walimu ambao wako pembezoni bado hawajawa na miundombinu mizuri ya kufundishia, wanafundisha katika mazingira magumu. Makazi wanayokaa hayaridhishi, maji ni taabu na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukitaka kuwa na elimu bora ni lazima tuwawezeshe walimu kwani wakiwa wanalalamika watakuwa hawawezi kufundisha wanafunzi vizuri. Lazima mishahara yao wapate kwa wakati muafaka kwani walimu wanaoishi vijijini mishahara yao ni mpaka waifuate mjini na mshahara wenyewe ni mdogo, haukidhi mahitaji na mwalimu anakuwa hafundishi na anaanzisha kufanya biashara ndogondogo ili kujikimu na maisha kama kuuza karanga, ubuyu na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi jirani za wenzetu, walimu wanathaminiwa na wanaheshimika lakini hapa Tanzania hatuwajali walimu na hatuoni umuhimu wao. Walimu ni nguzo muhimu ya maendeleo, Je, ni lini Serikali itahakikisha walimu wanapewa kipaumbele na kulipwa stahiki zao kwa wakati muafaka?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la shule za binafsi, baadhi ya shule za binafsi mazingira yake siyo mazuri! Sehemu wanazolala wanafunzi haziridhishi zina kunguni na kadhalika. Vyakula wanavyokula siyo vizuri kwa afya zao. Naomba Serikali iwe inakagua shule hizi mara kwa mara na zile ambazo hazipo kwenye kiwango zifungwe au kutozwa faini.