Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalenga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa nafasi hii ya kipekee niliyopewa ya kuweza kuchangia hotuba ya Rais. Kwa kweli, kwanza nimshukuru Rais mwenyewe na Chama changu cha Mapinduzi kwa kunipa nafasi ya kugombea kuwa Mbunge wa Jimbo la Kalenga. Pia niwashukuru wananchi wa Kalenga pamoja na familia yangu kwa kunisimamia, kuniamini, kuniombea, mpaka leo nimesimama hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa sababu ameendelea kuliweka Taifa hili katika hali ya amani. Ndiyo maana hata leo Watanzania tunaweza kufanya mambo yetu kwa uhuru ni kwa sababu, tunaye Rais ambaye anapenda amani na kweli ameilinda amani. Pia namshukuru Rais kwa sababu ya nidhamu kubwa ambayo ameileta kwenye Taifa la Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, George Washington alisema kwamba imani ni roho ya jeshi. Jeshi dogo katika kukaa kwa pamoja linaweza likafanya mambo makubwa. Ndiyo maana sasa kama nchi tumeweza kuingia katika uchumi wa kati kwa sababu ya ile nidhamu kama Taifa ambayo tumejijengea. Kwa hiyo, nimshukuru sana Rais kwa ajili ya hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi na Watanzania wengi tunamuunga mkono, tuko pamoja naye pamoja na vijembe vinavyoendelea vya watu wasio na macho ya kuona uzalendo mkubwa huu unaofanywa na Rais wetu. Tupo Watanzania ambao tutamtetea usiku na mchana na nchi hii itafika kwenye hatima yake tukufu na sisi tukiwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa habari ya kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais yako mambo mengi, lakini mimi niliona nianze kujielekeza kwenye kilimo. Upande wa kilimo hii Program ya Pili ya Kuendeleleza Sekta ya Kilimo ukiitizama imejaa majawabu mengi sana ambayo yataleta majawabu makubwa ya upungufu wa chakula katika Taifa la Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nafahamu kwamba bado haijaanza kupewa pesa. Kama hii Program ya Pili ikianza kupewa pesa tutatatua changamoto nyingi kwenye kilimo. Kwa mfano, tumeeleza kwa mapana sana ni namna gani tutakwenda kutengeneza skimu za umwagiliaji. Tukianza kuipatia pesa tunaweza kuanza kuwapa Maafisa Ugani pesa kidogo, kwa mfano Afisa Ugani mmoja kwa kila kata; tukachagua kata fulani kwamba huyu akatengeneze miche ya korosho, huyu akatengeneze kishamba-darasa chake cha miche ya parachichi watu wakaenda kujifunza pale wakapata ujuzi na wakaendelea. Serikali ina-finance kwa kumpa ruzuku na yeye huyu Afisa Ugani atapata pesa kwa sababu utakuwa ndiyo mradi wake. Tukifanya namna hii tutakuwa tumetengeneza motisha kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine ni namna gani tunalinda ardhi. Ardhi yetu imeendelea kufa kwa sababu ya sumu kali. Je, hizi mbolea ambazo tunaleta sijui tunazikaguaje kwa sababu nimepita maeneo mengi yalikuwa mazuri unakuta sasa hakuna kinachoota kwa sababu ya mbolea za sumu. Suala hili tuliangalie sana namna gani tunaweza kulinda ardhi zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kwenye mbegu, hata Rais ameendelea kuzungumza. Ndugu zangu sasa hivi biashara kubwa duniani ambayo itakuwa kama ya mafuta ni biashara ya mbegu. Kuna vita kubwa hawa wakubwa kutuletea mbegu, nimeona sehemu fulani walileta migomba ikawa inazaa sana lakini mwishoni inaoza. Kwa hiyo, kama Taifa ni lazima tujielekeze katika kutunza mbegu zetu za asili ili tusifike mahali tukawa watumwa na tukizembea tutakuwa watumwa kwelikweli.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni linalohusu masoko kwenye kilimo. Watu wamekuwa wakizungumza kwamba tusiuze bidhaa Kenya. Haya ni makosa makubwa na nisingependa mtu azungumzie habari ya kutokuuza bidhaa Kenya. Mimi nalima parachichi pale Njombe, Wakenya wanakuja shambani kwangu wananunua kilo moja Sh.1,500/= parachichi inayobaki naenda kuuza kiwandani kilo moja Sh.300/= sasa wewe unasemaje Mkenya asije kununua, nikauze wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, suala la msingi tulete ushindani. Tuhimize wafanyabiashara wakubwa kama ilivyo kwa Coca washindane lakini usizungumzie habari ya kutokuuza Kenya ni kosa kubwa sana hilo. Kwa hiyo, suala la masoko kwanza tuache kuwazuia Watanzania kuuza bidhaa zao nje kwa sababu tunavyowazuia tunapunguza pia tija mazao yanaendelea kuoz. Kwa hiyo, hilo ni jambo la msingi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine kwenye kilimo…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja.