Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru kipekee kuweza kunipa nafasi ya kuchangia hotuba hii ya Mheshimiwa Rais. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyenipa kibali kuingia mahali hapa, hakika nimeona ni kwa namna gani jinsi Bungeni kulivyo pazuri kiasi kwamba kweli ukiwa umeingia humu kutoka lazima utamani kutoa roho ya mtu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikishukuru Chama Cha Mapinduzi chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli Rais wetu kipenzi kwa kuweza kuhakikisha uchaguzi huu unakuwa wa haki, lakini pia kusimamia wanyonge wote wa nchi hii waweze pia kushiriki katika maamuzi ya kutunga sheria katika nchi hii. Niweze kushukuru familia, wadau, rafiki, jamaa, viongozi wa dini na marafiki zangu wote wana maombi wote walioweza kunisaidia kuweza kufika mahali hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho lakini si kwa umuhimu nishukuru Wanasongwe, niwashukuru wanawake wa mkoa wa Songwe kwa kuweza kuwa wazalendo na kunipa nafasi ya kuweza kuingia mahali hapa, bila kura zao haikuwa rahisi, lakini waliweza kusimama imara na kunipa kura na leo niko ndani ya Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kujielekeza katika hotuba hotuba ya Mheshimiwa Rais. Kipekee niseme hii ni hotuba ambayo imejaa matumaini mengi kwa Watanzania. Watanzania tunayo imani kubwa na Mheshimiwa Rais kulingana na namna ambavyo ameweza kufanya kazi kubwa ndani ya miaka mitano iliyopita, aliyofanya ni mengi kila mtanzania anajua.
Mheshimiwa Naibu Spika, nijikite katika kipembele cha elimu ya ufundi, nikirejea vyuo vya VETA na DIT ambavyo viko katika Mkoa wangu wa Songwe. Serikali imeweka pesa nyingi sana katika hivi vyuo vya VETA na DIT, ni vizuri vinavutia na vina mazingira mazuri sana kwa watoto wetu kuweza kupata mafunzo ya ufundi pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto iliyopo ni kwamba, hivi vyuo havitumiki ipasavyo, havitumiki kwa kiwango kinachostahili. Ukienda katika maeneo yale idadi ya wanafunzi waliopo katika vyuo ni wachache. Kama Serikali imeweka pesa basi tutafute namna ambayo itakuwa nyepesi kwa vyuo hivi kuweza kupata wanafunzi na mchango wangu kwa Serikali, ningependa kushauri mambo yafuatayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kungekuwa na direct enrolment ambayo wale wanafunzi ambao wanakuwa hawajapata nafasi ya kuingia Sekondari, wapewe nafasi, wachaguliwe kama wanavyochaguliwa wale walioenda sekondari, waweze kupangiwa vyuo vya ufundi. Hii itasaidia wale wazazi wa wale watoto waone kama watoto wao nao pia wamepata opportunity na wakawajibika kuwapeleka watoto katika hivyo vyuo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niombe kwa halmashauri kwa sababu tayari tunayo 10% ambayo tunatoa kama mkopo, tungetumia pesa hii kuweza kusababisha mafunzo kwa vile vikundi ambavyo vimekuwa vimeanzishwa. Kumekuwa na changamoto ya utoaji wa pesa nyingi kwa vikundi lakini wanavikundi wanashindwa kubuni miradi yenye tija, wanaishia kubuni pikipiki, wanaishia kubuni bajaji, lakini pia wanaishia kubuni kubuni miradi ya ufugaji kuku, kitu ambacho kinasababisha washindwe kufanya marejesho mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuongezea na kumalizia…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Muda umeshaisha Mheshimiwa, kengele imeshagonga.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi. (Makofi)