Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Eng. Hamad Yussuf Masauni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kikwajuni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. ENG. HAMAD MASAUNI YUSSUF: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nianze kwanza kuipongeza Serikali kwa ufanisi wa utekelezaji wa Mpango wa Miaka Mitano iliyopita ambao tumeona mwenendo wa viashiria vyote vya uchumi vikiimarika licha ya nchi yetu ama dunia kwa ujumla kukumbwa na janga la Covid 19.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mtazamo wangu mafanikio haya yamechangiwa zaidi na uongozi imara, uongozi thabiti na wenye maono katika nchi yetu. Mara nyingi uongozi thabiti na uongozi imara hupimwa pale Taifa linapoingia katika misukosuko ama Taifa linapohitajika kutoa maamuzi magumu na mazito kwenye maslahi ya nchi na watu wake hapo ndio unaweza kujua kama nchi hii ina uongozi thabiti ama laa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi bahati njema Mheshimiwa Dkt. John Magufuli, kiongozi wetu mkuu amejipambanua vya kutosha katika eneo hilo, wala sio nilichokipanga kukizungumza hapa. Leo nimepanga kuzungumza mchango wangu kuhusiana na mpango. Nitaomba angalau nitumie hata dakika moja nizungumze jambo moja la msingi sana na hasa kwa sisi ambao tunatokea Zanzibar. Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli wakati akiwa vilevile ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi amesimamia vema maandalizi ya ilani ambayo maandalizi hayo katika Ibara 136(e) kwenye maeneo mahususi ya Zanzibar yameweza kutoa mwelekeo mpya wa uchumi wa blue kama ni sekta ya kipaumbele kwa Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichukue fursa hii kumpongeza sana Rais wa sasa hivi wa Zanzibar, Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi ameanza vizuri sana katika siku si zaidi ya mia moja tumeshuhudia utiaji saini wa mikataba mikubwa ya ujenzi wa bandari za uvuvi, bandari za mafuta na gesi, bandari za mizigo, kiwanda cha kuchakata samaki, Chuo Kikuu cha Uvuvi, chelezo na kadhalika haya ni mapinduzi makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni imani yangu kabisa miradi hii itakapokuwa imekamilika kwa wakati, basi itaiondosha Zanzibar na kupiga hatua kubwa sana ya kimaendeleo na changamoto ya ajira kwa vijana ikiwemo vijana wa Jimbo langu la Kikwajuni itakuwa limepata ufumbuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Magufuli, maono yake haya hayakuwa yameanzia juu juu, mtakumbuka mara nyingi zinapokuja shughuli za uchumi wa bluu miaka ya nyuma alikuwa aki-delegate kwa Rais wa Zanzibar aliyekuwa wakati huo Dkt. Shein, lakini kana kwamba hiyo haitoshi, ameamua kugawa meli nusu kwa nusu bila kujali ukubwa wa kijiografia wala kidemografia kwa Taifa hili kati ya Zanzibar na Bara hii inadhihirisha ni mapenzi makubwa ambayo anayo kwa Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze sana Waheshimiwa Wabunge katika hili wameunga mkono naamini hii inadhihirisha umma kwamba muungano wetu huu si muungano wa vitu ni Muungano wa kidugu wa damu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja katika mpango, langu ni moja kwamba juu ya mafanikio yote ambayo tumeyazungumza ni ukweli usiofichika kwamba tuna changamoto ya idadi ya maskini wengi katika nchi hii. Wataalam wanasema kwamba wananchi wa Tanzania ambao wanaishi chini ya Dola 1.9 ni zaidi ya nusu. Ni kweli kasi ya umaskini imepungua kwa mujibu wa takwimu za miaka kumi mpaka 2018, wanasema kasi ya umaskini imeshuka kutoka asilimia 34.4 kuja asilimia 26.4. Hata hivyo, takwimu hizo hizo za wakati huo huo zinaonesha kwamba idadi ya umaskini imeongezeka zaidi ya milioni moja, kutoka maskini milioni 14 kuja 15.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hapa kuna jambo la kufanya ambapo tunaenda nao, kwanza lazima tujue tatizo ni nini? Tatizo ni moja kubwa la msingi kwamba sekta hizi ambazo zinaajiri watu wengi, kwa zaidi asilimia 66.6 ikiwemo kilimo, mifugo na uvuvi ukuaji wake ni mdogo kulinganisha na sekta ambazo haziajiri watu wengi kama vile ujenzi, huduma, madini na kadhalika. Kwa hiyo kuna haja ya msingi ya kuhakikisha kwamba sasa kipaumbele chetu tunawekeza katika sekta hizi ambazo zinaajiri watu wengi zaidi na kuzifungamanisha sekta hizi na viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kauli mbiu ya mpango wetu wa mwaka ujao unazungumzia kwamba ukuaji wa kujenga uchumi wa viwanda na kuchochea mageuzi ya uchumi na maendeleo ya watu. Sina shaka kwenye maendeleo ya watu tumefanya kazi nzuri, tunapozungumzia kupungua kwa umaskini ni kwa sababu ya kazi nzuri ambayo imefanya kwenye kuwekeza katika sekta ya elimu, katika sekta ya maji, sekta ya umeme vijijini na maeneo mengi, ina maana umaskini umepungua kasi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitajika sasa hivi tuwekeze katika kuona jinsi gani tunaibua fursa za kiuchumi kwa watu ambao wanashiriki katika sekta hizi na njia peke ya kufanya hivyo ni kuona kwamba sasa tunaifungamanisha na viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni yangu ni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, nataka tufanye marekebisho katika hii kauli mbiu, badala ya kusema kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu mimi nasema iwe na kupunguza idadi ya maskini huku mwisho imalizie hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, bahati mbaya au bahati nzuri jimbo langu mimi sisi tunalima asmini tu, kwa hiyo naomba nitoe mapendekezo zaidi nikijikita katika uvuvi. Jambo la kwanza na kubwa kuliko yote ili viwanda vya uvuvi viweze kusimama lazima wawepo samaki wa kutosha na samaki wa kutosha hatuwezi kuwapata kama hatuna utaratibu mzuri, aidha, wa kupitia public ama private sectors. Kwa hiyo, lazima ili hoja ya Mheshimiwa Rais aliyoizungumza ya kununua meli katika Bunge hili kuanzia bajeti ya mwaka huu tuhakikishe kwamba Serikali tunaishauri inaongeza bajeti ya kuweza kununua angalau meli mbili kila mwaka za uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile wewe ni champion wa hili jambo, ulifanya kazi nzuri sana ya kuhakikisha kwamba tunasimamia kupitisha Sheria mpya ya Uvuvi wa Bahari Kuu. Hoja ya uvuvi ya bahari kuu haiepukiki na hoja hii ilipofikia imefikia pazuri, nimpongeze Waziri wa Mifugo na timu yake wameanza kazi vizuri. Sasa hivi kanuni lazima aziharakishe, lazima ahakikishe kwamba wanashirikiana na mwenzake Waziri wa Zanzibar kuharakisha kanuni. Kanuni hizi zitakapokamilika ndipo changamoto nyingi ambazo zilikuwa zikikwaza sekta ya uvuvi na viwanda vitakapokuwa vikipata ufumbuzi ikiwemo suala la tozo na suala la leseni, utaratibu wa exemption na mambo mengine mengi, utaratibu wa kujengea uwezo vijana wetu ili waweze kushiriki katika sekta hii ni na mambo mengi ambayo tuliyajadili vizuri mwaka uliopita kwenye mabadiliko la sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, katika Mpango huu limezungumzwa suala la ujenzi wa Bandari ya Mbegani, kwa mtazamo wangu kwanza bandari moja haitoshi. Nakumbuka Mheshimiwa Rais wa hapa wakati anazindua Bunge alishangazwa sana kuona kwamba ukanda mzima wa bahari hindi kuanzia Lindi, Mtwara, Mafia, Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Pemba, Ugunja, hakuna hata kiwanda kimoja cha kuchakata samaki. Hii inasababishwa na nini? Kwa sababu tutakapokuwa tumeimarisha miundombinu mizuri, miundombinu ya viwanda, miundombinu ya bandari na tukaweza kuwajengea uwezo wananchi wakashiriki vizuri katika uchumi huu wa bahari kuu, itasaidia sana kuweza kuchochea sekta hii na sekta ya uvuvi itaimarika na hatimaye tutaweza kupambana na changamoto ya kupunguza umaskini katika nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nilidharimia kuchangia katika eneo hilo la uvuvi, nakushuru sana kwa kunipa fursa hii. (Makofi)