Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Neema William Mgaya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia mada hii. Awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kunirudisha tena ndani ya Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia niwashukuru wapigakura wangu, akinamama wa Mkoa wa Njombe kwa kunichagua kwa kura nyingi za kishindo na kuweza kurudi tena ndani ya Bunge hili. Vilevile nikishukuru chama changu Chama Cha Mapinduzi kwa kuteua jina langu na kuniwezesha kuwa Mbunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri aliyoifanya ndani ya miaka mitano kuweza kutekeleza miradi mikubwa mbalimbali ndani ya nchi yetu, ukiwemo Mradi wa Stiegler’s, ukiwemo Mradi wa Standard Gauge. Miradi hii itakwenda kuufanya uchumi wetu wa Tanzania kuwa uchumi mkubwa lakini vilevile uchumi endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dira yetu ya Tanzania ni dira ya uchumi wa viwanda ambao utakuwa shindanishi lakini vilevile jumuishi kwa maisha bora ya Watanzania. Nimeona Wizara wana mipango mizuri ya kuhakikisha kwamba wanatumia malighafi mbalimbali zilizopo ndani ya Tanzania yetu ili kuweza kujenga uchumi imara na endelevu. Malighafi hizo zikiwa ni pamoja na malighafi ya uvuvi, malighafi zinazotokana na mazao, malighafi zinazotokana na madini na malighafi ambazo zinatokana na mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza kujielekeza kwenye malighafi ambazo zinatokana na madini. Kule kwetu Ludewa, Mkoa wa Njombe sisi tuna Mradi wa Liganga na Mchuchuma. Kwenye mradi ule kuna takribani madini ya chuma pamoja na mengine tani milioni 128. Kama Serikali itaamua sasa kutekeleza mradi ule, tutakuwa na chuma kingi ambacho kitasaidia kama malighafi katika viwanda vya kutengeneza nondo, mabati, vifaa vinavyotumika kwenye madaraja na vifaa ambavyo vinatumika kwenye reli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi huu wa Liganga na Mchuchuma, kama Serikali itaamua kuanza kuutekeleza tutakwenda kuokoa takribani bilioni 640 kwa mwaka ndani ya miaka 30 ya uhai wa mgodi huu wa Liganga na Mchuchuma, sambamba na kuweza kuzalisha ajira 35,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali, sisi wananchi wa Mkoa wa Njombe kwa muda wa miaka mingi tumekuwa tukiupigania, tumekuwa tukisimama, Wabunge mbalimbali wamekuwa wakisimama ndani ya Mkoa wa Njombe na Mikoa jirani kuiomba Serikali ianze kutekeleza Mradi huu wa Liganga na Mchuchuma. Kwa sababu kama nia yetu ni kukuza uchumi wa Tanzania, mradi huu kama utatekelezwa utakwenda kuchangia Pato la Taifa (GDP) asilimia tatu mpaka nne. Naomba Serikali itusikilize ili iweze kutekeleza mradi huu wa Liganga na Mchuchuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie malighafi ambazo zinatokana na mazao kama ya mbao. Mikoa ya Njombe, Songwe, Mbeya, Iringa, Rukwa, Katavi na Tanga ni wakulima wazuri sana wa mazao ya mbao. Naiomba sasa Serikali ihamasishe wawekezaji wa viwanda vya karatasi ili sisi Watanzania sasa twende kutumia karatasi zetu za hapa hapa Tanzania na kuhamasisha kufunguliwa kwa viwanda hivi vya karatasi. Hii itatusaidia pia kukuza ajira kwa watoto wa Kitanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nashangaa sana kama ikiwa mpaka sasa hivi Serikali na watu wengine tunaendelea kuagiza furniture kutoka nje ya nchi wakati tuna Magereza, JKT na wananchi ambao wana viwanda vya kutengeneza furniture, wanatengeneza furniture nzuri na zenye ubora kuzidi zile zinazoingizwa kutoka nje ya Tanzania ambazo nyingi ni mavumbi ya mbao, siyo mbao halisi kama zile furniture zinazotengenezwa hapa nchini kwetu Tanzania. Naiomba Serikali, i-discourage uingizaji wa furniture kwa kuweka kodi kubwa katika bidhaa hii na kupunguza gharama za kodi katika raw materials kama msasa na zile accessories ambazo zinatumika kunakshia furniture ili kuchochea uanzishwaji wa viwanda vingi vya furniture ndani ya Tanzania yetu na kuweza kukuza uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa nimejipunja sana kama sitazungumzia malighafi ya zao la parachichi ambalo liko ndani ya Mkoa wangu wa Njombe. Halikadhalika Songwe, Iringa, Katavi na mikoa mingine ya Tanzania wanalima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali imefanya jitihada kubwa sana ya kuweza kuwasaidia wakulima wetu wa parachichi kuweza kusafirisha parachichi nje na kuuza ikiwa ghafi. Naona ni wakati sasa Serikali ijikite katika kuhakikisha kwamba inahamasisha viwanda vinavyotengeneza cosmetics inayotumia malighafi ya parachichi kama conditioner ya nywele au lotion, majani ya parachichi unaweza ukatengeneza asali au dawa. Serikali ihamasishe viwanda hivi vya kutengeneza cosmetics ambayo inatokana na malighafi ya parachichi, viwekezwe kwa wingi nchini wakati huo tukiendelea kuhamasisha wakulima kuendelea kulima parachichi kwa wingi. Kwa kufanya hivyo, itasaidia pia kuongeza ajira kwa viwanda hivi ambavyo vitaenda kufunguliwa ndani ya mikoa yetu hii ya kulima parachichi na kuweza kukuza uchumi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kuzungumzia malighafi inayotokana na wanyama. Naipongeza Serikali kwa jitihada mbalimbali inazochukua kuhakikisha wameweza kuhamasisha na ku-convince viwanda mbalimbali vinavyotumia ngozi kutengeneza mikoba, viatu na mikanda. Naomba tusiishie level hiyo ya kutengeneza tu viatu, mikanda na mikoba, hebu tuige kwa wenzetu wa Ethiopia. Wao ndio wanao-supply ngozi katika Kampuni ya Mercedes Benz kwenda kutengeneza zile seat cover zake. Naomba Serikali ifikirie katika mlengo huo, hii yote ni katika kuweza kukuza pato la Taifa letu na uchumi wetu na kuufanya uweze kuwa endelevu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara ya Kilimo. Juzi hapa Mheshimiwa Hussein Bashe alizungumza namna bora ya kuboresha mbegu ili tuweze kupata malighafi nyingi kwa kuwa na mbegu bora katika masuala mazima ya kilimo. Haitoshi, inabidi Wizara ya Kilimo ishirikiane na Wizara ya Viwanda, baada ya kuwa Wizara ya Kilimo inaweka mikakati mizuri ya kuboresha mbegu zetu ili kuweza kupata malighafi bora na kuongeza mavuno, inabidi Wizara ya Viwanda ikae makini katika kuhakikisha kwamba malighafi hizo zinazotokana na kilimo zinatumika hapa hapa Tanzania katika kuchochea viwanda, kwa kuhamasisha viwanda vingi kufunguliwa ndani ya nchi yetu na kukuza uchumi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. (Makofi)