Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Salome Wycliffe Makamba

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie kwenye mapendekezo haya ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano na wa Mwaka Mmoja. Wamezungumza wengi lakini mimi napenda nianze kwa kutafuta tumekwama wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nasoma Mpango huu wa Tatu wa Serikali ilibidi nirudi nyuma niangalie Mpango wa Pili na Mpango wa Kwanza wa Maendeleo. Ukiangalia Mpango wa Pili wa Maendeleo ambao ndiyo tunaumaliza, Serikali kwenye eneo la ukuaji wa uchumi, ilikuwa imepanga kukuza ukuaji wa uchumi mpaka asilimia 10 ifikapo mwaka 2021. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyoanza tu ule Mpango mwaka 2016 tulianza na 7%. Tulipoanza tu Awamu hii ya Tano 2016 tukaporomoka kutoka 7% mpaka asilimia 6.8. Tukajipanga vizuri, mwaka uliofuata mwaka 2017/2018 tukarudi asilimia 7%. Hivi ninavyozungumza, tangu Awamu ya Tatu ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi, kiwango cha ukuaji wa uchumi kimebaki 7%. Tafsiri yake ni nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafsiri yake ni kwamba ukuaji wa uchumi katika nchi yetu ya Tanzania umesimama tangu mwaka 2001. Kwa maana hiyo, Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwenye Mpango wa Kwanza, Mpango wa Pili tumeshindwa kufikia angalau target ambayo tumejiwekea wenyewe ya asilimia 10 ya ukuaji wa uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, target hii iko kwenye Mpango, yaani Serikali wamejipangia wenyewe. Ni sawa na mtu unaenda kuposa ukaambiwa jipangie mahari; ukasema nitatoa Sh.50,000/=. Haya basi lipa, halafu unasema sina. Hapo sasa ndipo tunapoanza kukwama kwenye Mpango wa kuwasaidia wananchi kuwatoa kwenye umasikini. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, twende kwenye pato la kila mmoja. Kwenye Mpango wa Pili ambao ndiyo tunaumaliza, Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi ilisema itahakikisha Mtanzania anaongeza pato lake mpaka Dola 1,500 kwa mwaka ifikapo mwaka 2021. Wakati huo inaingia Awamu ya Tano, kipato cha mmoja mmoja kwa Mtanzania ilikuwa ni kama dola 1,043 na kasi zote, makofi yote na ngonjera zote tunazozipiga, tumejivuta wee, kutoka Dola 1,043, tumefika Dola 1,080; tumeongeza Dola 37 kwa mwaka. Yaani shilingi tuseme kama 6,000/= hivi kwa mwezi kwa kila Mtanzania yaani hizi kelele zote tunazozisikia. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kwa miaka mitano tumeweza kuongeza Dola 37 tu kwenye pato la Mtanzania mmoja mmoja, tafsiri yake, ili tufike kwenye target ya Dola 1,500 kwa kila Mtanzania, tunahitaji miaka 60. Hiyo ndiyo tafsiri. Kwa sababu miaka mitano tumeongeza Dola 37, tukiongeza miaka mitano mingine tutafika Dola 74 au tutashuka, hatuwezi kujua. Kwa sababu ikiisha hii kumi, hatujui atakayekuja atakuwa na kasi gani? (Kicheko)

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Salome kuna Taarifa upokee. Nilishawaambia hali ya hewa itachafuka hapa. Naona dalili za mawingu. (Kicheko)

Ni Mheshimiwa nani? Ni Mheshimiwa Kingu, karibu.

T A A R I F A

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe dada yangu Salome Taarifa kwamba, ukuaji wa uchumi na suala zima la per capita income lazima lijengewe base ambazo zikisha-mature zitakwenda kuleta spill over impact kwa individual citizen. Uwekezaji unaofanywa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi katika kuwekeza katika Sekta ambazo zitafanya transformation kwa mfano Sekta ya Umeme, Miundombinu pamoja na Miundombinu ya Kilimo hicho wanachokisema cha mwaka mmoja kukua kwa hizo dola anazozitaja ni upotoshaji. Nataka nimhakikishie Tanzania na uchumi wake utakwenda kubadilika kulingana na mipango Madhubuti ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

MWENYEKITI: Salome unaelimishwa kwamba hiyo hesabu yako inaweza ikawa hivyo kwa ile lugha ya wenzetu if everything remains constant. Sasa nani kakwambia tunakokwenda ni constant? Kwa uwekezaji anaousema kutakuwa na faster growth. Unapokea Taarifa hiyo?

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Kingu atulie. Tujadili haya mambo, Mheshimiwa Rais ana mategemeo makubwa sana na Bunge hili, tujadili haya mambo tumekwama wapi halafu nitashauri tunatokaje tulipo. Ndiyo maana nikasema kama tumeongeza dola 37 kwa pato la mtu mmoja kwa miaka mitano. Itatuchukua miaka 60 ili tufikie malengo ya pato la mtu mmoja liweze kufika dola 1500. Hapo sasa, if all factors remain constant, hapo ndiyo tutafika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hili jambo hili linasemwa uchumi wa kati, watu wanasema hela hatuna mfukoni na ni very confusing na nashauri tu Wabunge tupewe semina ya uchumi wa kati unavyotakiwa ku-reflect pesa zilizoko mifukoni mwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya kiwango cha umaskini nchini, Serikali hii ya Chama Cha Mapinduzi hasa Serikali ya Awamu ya Tano wakati inaingia madarakani iliahidi kupunguza kiwango cha umaskini kwa asilimia 11.5, kwamba watatutoa kwenye kiwango cha umaskini kutoka asilimia 28.2 mpaka asilimia 16.7. Sasa mpaka tunamaliza mpango huu wametutoa asilimia 28 mpaka asilimia 26 na pointi, sawa na asilimia 1.8. Sasa nina lengo kubwa sana la kuisaidia hii Serikali na mimi bado ni kijana. Kwa mwendo huu tunaokwenda nao kuna mawili; ama hatuwapi nafasi wachumi wetu kutushauri vizuri tuweze kuwa na mpango unaoendana na uhalisia au tunamwogopa Mheshimiwa Rais kumweleza ukweli, tunaamua kumpamba kwa maneno mazuri lakini kiukweli hali ya kiuchumi ni mbaya. Kuna hayo mawili. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili la kusema tumekuja kwenye uchumi wa kati, wananchi hawalielewi kwa sababu hali ya umaskini katika nchi hii ni kubwa. Ni zaidi ya asilimia 26.2, kwa hiyo ukisema tumeenda kwenye uchumi wa kati wakati watu bado ni maskini lazima watu wachanganyikiwe. Matokeo yake, tunavyo-promote kwamba tuko kwenye uchumi wa kati, tunajitoa kwenye level ya nchi inayostahili misaada…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Salome ngoja upewe Taarifa kidogo. Jitambulishe.

T A A R I F A

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naitwa Kingu.

MWENYEKITI: Aaa, bado Mheshimiwa Kingu unaongea tena.

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpa Taarifa dada yangu Salome.

(Hapa baadhi ya Wabunge walzungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Naomba mtulie this is democracy. Naomba kumpa dada yangu Salome Taarifa kwamba nchi kuingia kwenye uchumi wa kati kuna stage. Naomba dada yangu Salome atulie asome principles za ukuaji wa uchumi na masuala mazima ya global economy. Stage za nchi kuingia katika uchumi wa kati haimaanishi kwamba tumeshafika katika bar ya juu ya per capita income of individual na hicho ndicho Serikali ya Chama Cha Mapinduzi inajenga misingi sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tumeingia katika uchumi wa kati, tuko katika class ya chini, ndiyo sasa hivi tunajenga mipango hapa kutaka kuijenga nchi na kupeleka kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Salome pokea.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo Taarifa siipokei na kwa sababu ya muda, naomba niendelee na Mheshimiwa Kingu naomba utulie kidogo, acha hayo mambo. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali tuliyonayo ya kiuchumi mifukoni watu hawana kitu ndiyo inayosababisha watu wasielewe maana ya nchi kuingia katika uchumi wa kati na kwa maana hiyo hata Serikali yenyewe imechanganyikiwa kwenye hilo. Tumeingia kwenye uchumi wa kati tunajisifu. Nchi ikishaingia kwenye uchumi wa kati inaingia kwenye class ya nchi ambazo kuna baadhi ya mambo lazima tukose, tutakosa misaada mbalimbali, misamaha mbalimbali ya kikodi, scholarship za wanafunzi. Tunajikuta kwa sababu ya kukosa, kwa sababu tuko kwenye uchumi wa kati…

MWENYEKITI: Nimekuona Mheshimiwa Kimei. Mheshimiwa Salome subiri Mheshimiwa Kimei…

T A A R I F A

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii. Naomba niseme hivi, fedha iliyo mfukoni haihesabu kama wewe ni tajiri au sio tajiri. Kitu kinachohesabika ni kuna fedha unayopata wewe kama kipato chako, mshahara au umeuza mazao yao inaingia mfukoni kwako unalipa na kodi na kadhalika. Kinachojalisha sana ni zile huduma unazopata kutoka Serikali za bure. Huduma za bure kama elimu, watoto wanasoma bure. Hiyo shilingi ambayo ulikuwa ulipie mtoto wako anaenda shule si umeweka mfukoni? Unaibakiza mfukoni kwako. Ukipata matibabu ambayo yana ruzuku si hela inabaki mfukoni ya ziada? Ukipanda gari ambalo ulikuwa ulipe shilingi 1,000 ukalipa shilingi 500 kwa sababu barabara ni nzuri si hela inarudi mfukoni, si utajiri unaongezeka? Utajiri hautokani na ile hela ambayo lazima uwe nayo. Tuangalie pia kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imetupa huduma gani za ziada ambazo hazilipiwi na ambazo zinarudisha fedha zetu mfukoni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe angalizo moja. Fedha ambayo tunapewa inaenda moja kwa moja kwenye huduma hizi inasaidia zaidi kwa sababu kuna wengine walikuwa wanapata hela wanakunywa tu. Hata hawapeleki watoto shule, wanaacha shule. Sasa watoto wale wanaenda kwa hiyo inakuwa kwa welfare of the society ni kwamba hiyo inakuwa ina-contribute sana. Tusiangalie tu hela ya mfukoni, hela ya mfukoni haina maana! Hela ya mfukoni is not so much important. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Kimei. Actually, ndiyo maana alisema kwamba Wabunge tunahitaji semina. (Makofi)

Mheshimiwa Salome malizia.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, niongeze tu kwenye hilo neno lako ulilolisema, kwanza Taarifa siipokei na awe makini sana kwa sababu ni Mbunge wa Jimbo, unaposema tusiangalie tu hela ya mfukoni tunaongelea habari ya hali ya wananchi kuweza kufanya manunuzi ya bidhaa. Per capita income watu hawana hela. Serikali inajinasibu iko kwenye uchumi wa kati kuna watu wako Muamalili kule Chibe hawawezi ku-afford kununua kilo moja ya unga, yeye alikuwa Mkurugenzi wa CRDB, tunaongelea wananchi maskini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri…

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Sasa naomba nimlinde ili amalizie na sababu yake ni kwamba ni katika walio wachache na wao kutwa nzima ya leo wanachangia wawili tu. Kwa hiyo tuvumilie kidogo tusikilize mawazo ya upande wa pili. (Makofi)

Kwa hiyo, Salome nakupa dakika tano ili umalizie sasa. (Makofi)

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba nishauri yafuatayo: Wameleta mapendekezo ya Mpango. Warudi nyuma kuanzia mapendekezo ya Mpango wa Kwanza na wa Pili kwa sababu tumekwambia hapo. Warudi nyuma wakaangalie tulikosea wapi, kwa nini tuli-project kufika asilimia 10 na tumekwama kwenye saba tangu 2001 katika hali ya uchumi. Warudi hapo. Hiyo ni mosi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ni lazima turudi kwenye mfumo shirikishi wa kiuchumi. Hatuwezi kuishi kwenye Serikali ya matamko, hatuwezi kuishi kwenye Serikali ya miongozo. Ni lazima wananchi, Sekta Binafsi na Serikali tushirikiane kwenye kukuza uchumi na nitatoa mifano miwili. Mfano kwa kwanza ni kuhusiana na hivi vitambulisho vya wajasiriamali. Yalitoka matamko hapa, presidential proclamation kwamba vitambulisho view shilingi 20,000 vikakusanywe. Jambo hilo halikueleweka. Tukienda kwenye hansard Wabunge waliomba ufafanuzi lakini kwa vile ilikuwa your wish is my command, lilikwenda, limekwama! Sasa wamelirudisha mwongozo kwenye Wizara. Mwongozo kwenye Wizara unasema Halmashauri zikatekeleze, wakatekeleze kwa mfumo upi? Ule ule wa Mgambo kupiga mama zetu ili wachangie 20,000? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unayo power ya kuagiza sheria hii iletwe Bungeni ishirikishe wadau, ifanyiwe scrutinization ili iweze kuendana na mfumo halisi wa maisha ya Watanzania. Mfumo huo huo uko kwenye kodi za mabango na majengo. Walitoa kwenye Halmashauri, Halmashauri zika-paralyse. Sasa hivi wamewarudishia lakini kimsingi hawajarudisha, ni vile hawana manpower ya kukusanya zile pesa wamepeleka local government zikusanywe, zinaingia kwenye mfumo wa control number zinaenda Hazina kurudi kwenye Halmashauri ni mtihani. Kwa hiyo lazima tuwasikilize wananchi, lazima Serikali isikilizwe na wananchi ni Bunge. Kabla hawajaenda kwenye hatua hiyo sisi wawakilishi wa wananchi ni lazima tushiriki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, mapendekezo yangu. Iko haja ya kutengeneza Kamati Maalum ya Bunge itakayofuatilia ahadi za Serikali na Viongozi Wakuu wa Nchi hii. Leo Waziri kanijibu hapa, bahati nzuri ulikuwa kwenye Kiti namuuliza ni lazima tupunguze ajali za barabarani, ni lini utaleta marekebisho ya sheria ananiambia sheria iko njiani amefunga makaratasi ameondoka! Sijui njiani ni Kibaigwa, sijui ni Manyoni, hakuna commitment! Watu tuko serious, we are using brain, watu wanafanya siasa ndani ya Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hili Bunge lako ni Bunge makini, Mawaziri wageni mjue tunahitaji, na Kanuni zinasema lazima swali la Mbunge lijibiwe kikamilifu. Tutengeneze Kamati Maalum ya kufuatilia ahadi za Serikali na Viongozi Wakuu. Sasa hivi kila Waziri hapa anasema tutaongozana kwenda Jimboni kwako wanaenda kufanya nini, hatujui. Wakienda wanafanikisha hatujui. Tunataka tufahamu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho na sio kwa umuhimu, Mheshimiwa Mpango mwenyewe amesema kwamba ili tufanikiwe Mpango huu lazima tuwe na utawala bora lazima tuwe na amani, lazima tuwe na utulivu...

MWENYEKITI: Mheshimiwa Salome na Mawaziri wanatakiwa wafuatane nao ni Mawaziri wanawake tu. (Makofi/Kicheko)

Malizia hoja yako dakika tano zinaisha.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasema lazima tuwe na utawala bora, tuwe na amani, tuwe na utulivu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo hayako sawa! Ni kwamba yametulia tumetoka kwenye uchaguzi. Yaliyotokea kwenye uchaguzi mnayajua, hatuwezi kuka kimya. Tutengeneze Tume ya Umoja ya Maridhiano ya Kitaifa. Tukatibu vidonda vya wananchi. Mimi nimefanya kazi ya mahusiano ya jamii. Miradi yoyote itakayokwenda kutekelezwa na Serikali kwa wananchi wenye vinyongo lazima ikwame! Twendeni tukatibu magonjwa. Kuna watu 50 hapa wamepita bila kupingwa kwenye Majimbo, wapo humu! Miradi mikubwa imeelekezwa kwenye majimbo yao unategemea utekelezwaji wa miradi ile utakwendaje? Lazima tutoe vinyongo, watu waseme tuyamalize. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe mwenyewe unajua… kumtangaza Bwana mdogo pale ilibidi waniweke jela, nina kinyongo…. (Makofi/Kicheko)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Spika, muda wako umeshaisha, muda wako umekwisha.

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)