Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Hawa Subira Mwaifunga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia mapendekezo ya Mpango huu. Naomba pia nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuniwezesha kusimama siku ya leo nikiwa na afya tele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijikite kidogo kwenye sekta ya viwanda. Nilikuwa napitia hapa kwenye sekta ya viwanda; katika ukurasa wa 32, nilikuwa nasoma hapa kati ya mwaka 2015 – 2019, kuna viwanda vipya 8,477 vimeongezeka. Katika viwanda hivyo wameonyesha viwanda vikubwa, viwanda vya kati, viwanda vidogo na viwanda vidogo kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ongezeko la ajira katika kipindi cha mpaka mwaka 2015 lilikuwa ni 254,786; lakini 2015 – 2019, ajira zimeongezeka kufikia 482,601. Sasa ukiangalia ukurasa wa 33 Mpango unasema baada ya Serikali kuomba Mifuko ya Hifadhi ya Jamii wameweza kutengeneza viwanda 35 ambavyo katika viwanda hivyo vimetengeneza ajira 250,000. Sasa nataka nifahamu kwanza je, hivi viwanda 35 ni tofauti na viwanda 8,477 na kama siyo tofauti, je, ajira zilizoongezeka ni ngapi? Ni hizi 227,000 zinazoongezeka katika 482,000 ama 250,000 ni ajira tofauti na hizi nyingine na 227,000. Hapa kidogo nimepata changamoto na nikaona bora niulize ili wakati Waziri anakuja ku-wind up atuambie exactly kati ya 2015 - 2019 ni ajira ngapi zimetoka kwa Watanzania kupitia sekta hii ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya viwanda, mwaka 2015 - 2020 ndiyo ilikuwa slogan ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi, lakini tunaona ni kwa namna gani bado hatukutimiza lengo ambalo tulikuwa tumekusudia, kama ambavyo mipango ilikuwa ilikuwa inaonyesha. Leo Serikali ilikuwa na viwanda vilivyobinafsishwa na mpango wa Serikali ulikuwa vile viwanda vilivyobinafsishwa kwa wale watu ambao walikuwa hawaviendelezi, viwanda vile vichukuliwe na Serikali. Nilitegemea sasa, baada ya Serikali kuzungumza na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, ingekwenda moja kwa moja kwenye vile viwanda vilivyokuwa na tija wakawapa watu na viwanda vile vikawa havifanyi uzalishaji wangevichukua ili kuendeleza tija iliyokuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natolea mfano, Kiwanda cha General Tyre, Serikali ina ubia asilimia mia moja, kiwanda kile ni cha Serikali. Kuna Kiwanda cha Urafiki, kiwanda hiki kilikuwa kinazalisha vizuri sana, demand ya nguo za urafiki huko uraiani ni kubwa kuliko tunavyofikiria. Cha ajabu, Serikali ina ubia wa asilimia 49 na mchina ana ubia wa 51, tuliishauri Serikali hapa kwa nini tusichukue kiwanda kile sisi wenyewe ili tuweze kupata faida, lakini pia kuongeza ajira kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka ya nyuma Kiwanda cha Urafiki kilikuwa kinaajiri Zaidi, kipindi ambacho hatujaingia ubia na Wachina, lakini tangu tumeingia ubia na Wachina, kiwanda hiki, ajira zimepungua kutoka zilizokuwepo zimepungua kwa asilimia zaidi ya 70. Leo ninapozungumza kiwanda kile haki-operate na hata kama kinafanya kazi walioko pale ni wale viongozi wakubwa tu na kiwanda hiki ni cha kwetu sisi Watanzania, kwa nini tusiwekeze kwenye kiwanda hiki ili kuleta tija kwa sababu tayari Serikali ina ubia wa kutosha katika kiwanda kile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuishauri Serikali, viwanda vyote ambavyo tunadhani na tunaona na tunajua kwamba viwanda hivi vilikuwa vinaleta tija kwa Taifa, vinatoa pato kubwa kwa nchi, Serikali iweze kuvirejesha. Hii Mifuko ambayo Serikali inakwenda kuchukua fedha, fedha hizi ni za Watanzania, je, hivi viwanda vilivyowekezwa kuna uhakika gani kwamba, fedha hizi zitarudi kwenye Mifuko kwa wakati ili Watanzania wanaostaafu waweze kupata fedha zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na changamoto kubwa sana kwa Watanzania wengi katika Mifuko hii kulalamikia mafao yao, lakini leo tumechukua fedha tumekwenda kuwekeza kwenye viwanda 35, lakini kwenye Mpango vinaonyeshwa viwanda vitatu sijui vinne, hatujaonyeshwa hivyo viwanda 35 vyote ambavyo vimewekezwa, lakini tangu uwekezaji umefanyika, je, tumeona kuna tija katika uwekezaji na fedha hizi za Watanzania hawa zitarudi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana Serikali, badala ya kupelekapeleka tu fedha kwenye maeneo ambayo hayana tija, tuangalie viwanda hivi ambavyo tunaamini vina tija. Leo kiwanda cha General Tyre kifufuliwa nawaambia Watanzania wengi wana magari, tukaamua moja kwa moja hakuna kuagiza matairi kutoka nje, nawaambia hivi, kile kiwanda kitakuwa kina tija, kitaleta ajira, lakini pia kitaongeza mchango mkubwa kwenye pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna viwanda ambavyo vilikuwa ni viwanda vya magunia, sasa hivi hata haya magunia ya sulphate ambayo tunatumia wakulima kuweka vitu vyetu wanasema hayafai. Kwa nini viwanda vile visifufuliwe ili magunia yetu ya kizamani yakarudi ili tuweze kupata vifungashio ambavyo vinatakiwa kuliko ilivyo hivi sasa, vifungashio vya sandarusi ambavyo watu wa mazingira wanapiga marufuku. Kiwanda hiki kingefufuliwa kingesaidia kuondoa tatizo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna Kiwanda cha Nyuzi ambacho kilikuwa katika Mkoa wa Tabora peke yake. Kiwanda hiki ni kiwanda cha muda mrefu. Kilianza kujengwa hata mimi sijazaliwa lakini baada ya hapo kiwanda hiki, baada miaka 10 toka 1975 - 1985 kiwanda hiki kilianza kufanya kazi. Baada ya miaka kumi mwaka 1995, kiwanda hiki kilikufa na kilipewa mwekezaji; mwekezaji huyu ameshindwa kukifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu alifika pale, Naibu Waziri wa Kilimo kaka yangu Mheshimiwa Bashe alifika pale, waliona hali halisi na ukweli uliopo. Serikali wawekeze kwenye viwanda vyenye tija, Tabora tunalima pamba, Mikoa ya Kanda ya Ziwa inalima pamba, ni rahisi kuchukulika pale na kupeleka Tabora kutengeneza nyuzi zetu kama ilivyokuwa hapo zamani. Ili kuipa uhai TABOTEX Watanzania wa Kanda ya Ziwa na Mkoa wa Tabora waweze kupata ajira lakini Serikali iweze kuongeza mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mpango lakini pia mpango bila afya bora hatuwezi kufika. Hapa tumeona Mpango umesema kwamba vifo vya mama wajawazito wakati wa kujifungua vimepungua kutoka 432 hadi 321. Vifo hivi ni vingi sana na vifo hivi vinatokana na umaskini wa wanawake wengi ambao hawana uwezo wa kulipia gharama za matibabu. Vifo hivi ni vifo ambavyo vinajulikana ambavyo vimesajiliwa kwenye hospitali; niambie vifo vinavyotokea kwa watu wanaojifungulia nyumbani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengi sasa hivi kutokana na gharama ya kujifungua wanawake wengi wameamua kujifungulia nyumbani. Hata hivyo, wanawake wengine wanapokwenda katika hospitali, anapofika maeneo ya hospitali hana uwezo wa kulipia ile hela wakati akisubiri apate msaada wa hela, wanajifungua wakiwa njiani. Hayo tumeyashuhudia na tumeyaona. Kwa hiyo, vifo vya akina mama wajawazito wakati wa kujifungua bado ni vingi, hatuhitaji hii takwimu, tunachohitaji katika Mpango huu vifo viondoke kabisa na siyo kupungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukizungumza sana kuhusiana na masuala ya afya, elimu na maji lakini miaka 61 ya uhuru wa Tanzania bado tunazungumzia afya, maji na elimu. Hebu ifike mahali tukiwa tunaingia kwenye Mpango hizi biashara ziwe zimeshakwisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ni nchi tajiri ambayo hatupaswi kwa sasa kukaa kuendelea kuzungumzia mipango ya afya. Afya tungesema sasa tunaboresha ama magonjwa ya mlipuko kama Corona na magonjwa mengine yanayotokea ndiyo tungekuwa tunazungumzia sasa lakini siyo afya ya uzazi, mtoto, mama wala ya mwananchi yeyote; hizo zingekuwa ni historia. Toka miaka 61 ya uhuru mpaka leo bado tunazungumzia matatizo ya afya, tuache. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)