Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tabora Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniruhusu nichangie hoja hii ya mpango na kwa sababu muda ni mchache nitajikita kwenye mambo mawili tu, nayo ni elimu na lugha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni zao la shule ya ufundi, tulisoma sisi kutoka Moshi Technical, kutoka Ifunda tukaenda technical college, tukatengeneza watu wanaoitwa FTC (Full Technician Certificate) na hawa ndio waliojenga viwanda, waliofanya kazi kwenye viwanda mpaka vilipokufa, lakini sasa elimu ya ufundi imekuwa hadithi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaongelea uchumi wa viwanda, kama hakuna mafundi wa kutengeneza mitambo ndani ya viwanda hivyo, vitakufa. Ni sawa na magari yetu haya, kama hatuna garage ya kupeleka na mafundi wakawepo huko, magari hayawezi kuwa magari. Tulikuwa na mfumo mzuri sana wa elimu, kutoka shule za sekondari ufundi, form one mpaka form four unasoma umeme, unaenda technical college unasoma umeme, unamaliza FTC unarudi tena kusoma engineering, umeme miaka kumi mtu huyo anafanya kazi kiwandani kwa kujiamini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili limekufa toka marehemu Mungai alipofuta vyuo vya kati hapa akafuta na FTC, sasa tunafanya nini tunaendelea kukuza VETA na nashukuru sana VETA zinatengeneza mafundi wa vijijini, kwa hiyo uchumi utakwenda vijijini watatengeneza magari kule, watatengeneza mavitu ya umeme na kadhalika, kwa hiyo, watapata hela vijijini na uchumi utakua vijijini. Hata hivyo, hawa hawatafaa kiwandani, wako chini au ni wa ngazi ya chini ya ufundi unaoitwa artsan. Baada ya artsan kuna FTC halafu ndio kuna engineer pale juu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa kazi ndiyo huwa unafanyika hivyo, engineer anafanya kazi na watu technicians 25, technician mmoja na Artsans 25, ndipo unakuwa mfano wa ufundi. Sasa viwanda hivi ambavyo tunakusudia vikuze uchumi, lazima tuwe na elimu ya ufundi ambayo itaendana sawasawa na uchumi tunaoutaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba chuo cha ufundi kianzishwe upya, DIT, sio chuo cha ufundi sio technical college imekuwa academic institute, Dar es Salaam Institute of Technology haitengenezi watu wa FTC blue color tunatengeneza white color. Kwa hiyo, degree, narudia tena degree, hazitatusaidia kukuza uchumi na ndio maana ziko nyingi mtaani zinatafuta kazi. Tunataka technicians, fundi sadifu na fundi mchundo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye hatua ya pili, lugha ya kufundishia, kote duniani, hakuna nchi iliyoendelea kwa kutumia lugha ya watu wengine. Tunataka Kiswahili kitumike kwenye lugha ya kufundishia, shule ya msingi mpaka secondary school. Hivyo wanafunzi watakuwa na fursa ya kujifunza taaluma, sio kujifunza lugha. Tunataka Kiingereza, Kifaransa, Kijerumani, Kichina vifundishwe kama lugha katika shule zetu, lakini lugha ya kufundishia elimu iwe Kiswahili. Na- declare interest nitaleta katika Bunge lako hoja ya…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Maige, ku-declare interest ni nini kwa Kiswahili? (Kicheko)
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia tena, nataka kuelezea maslahi yangu ya hapo baadaye kwamba, nitaleta hoja binafsi kama Kiswahili kiwe lugha ya kufundishia elimu yetu. Nilifanya research ndogo au tafiti mdogo tu utafiti mdogo wa Kiswahili kinafaa kufundishia au hakifai, watoto wanielezee jinsi ya kupanda muhogo, darasa la saba wote wakapata, lakini wote nikawaambia andikeni sasa Kiingereza, wakaandika wote wakakosa, hakuna hata mmoja aliyepata hata chini ya 20 hawakupata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lugha ya mama ndiyo inayomfundisha mtoto, tafiti nyingi zimefanyika, watu wengi wanapinga Kiswahili kutumika kama lugha ya kufundishia, hawasomi tafiti zilizofanyika, lakini pia wanakumbuka mambo ya nyuma. Nimekaa Uingereza miaka saba, watu wote mtaani kwangu wanaongea Kiingereza lakini hawajui kusoma wala kuandika. Hapa ndivyo ilivyo, watu wengi wanasema huyu mtoto anaongea Kiingereza kama maji kasoma, kumbe hajui chochote, lazima Kiswahili kitumike kama lugha ya kufundishia. Sasa hivi limekuwa jambo gumu sana, tunasoma darasa la kwanza mpaka la saba Kiswahili, halafu tunabadilisha kama masafa ya redio kutoka Kiswahili kwenda Kiingereza. Watoto wakifika kidato cha kwanza, wanaanza kujifunza Kiingereza kwanza na wakati huo wanasoma masomo, wanafeli, watoto wengi tumewaacha nyuma sio kwamba hawana elimu…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)