Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Halima James Mdee

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niungane na wote ambao walisema kuna umuhimu kama Taifa kupima ardhi yote. Wakati wa Uchaguzi Mkuu CHADEMA tulisema is very possible kupima ardhi na kutoa hati kwa wananchi kwa sababu kuna potential kubwa sana kupitia kodi ya ardhi kwa nchi kuweza kupata mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na wote ambao wanaitaka Serikali ije na mpango mahsusi wa kuhakikisha sekta binafsi ya Tanzania inashamiri. Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mpango kwenye tathimini ya mpango wake wa 2011-2015 na mpango unaokuja anakiri kuna changamoto ngumu sana kwenye sekta binafsi, ushiriki wao hauridhishi. Lazima tujiulize maana lazima unapofeli ufanye tathmini kwa nini ni ngumu kwenye eneo hili muhimu tunalotarajia lichangie zaidi ya 40 trilioni kwenye mpango wetu huu mpya tumeshindwa kulivutia kuwa ni sehemu muhimu wa maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimsikia ndugu yangu hapa akisema wasiosikia na wasikie, wasioona na waone, ndugu yangu tunapofanya tathmini ni muhimu tuwe wakweli pia. Mimi niwashauri Wabunge hawa kwa sababu ni mkongwe kidogo, tukija na mentality ya kusifia SGR, Stigler’s Gorge na madaraja ya Dar es Salaam, hatuwezi kulisaidia taifa kwa sababu hivyo vitu vitatu is no longer breaking news. Stigler’s Gorge ilianza kuzungumzwa miaka mingi sasa hivi inajengwa asilimia 25, SGR tulianza kuzungumza tokea enzi hizo iko kwenye mipango imeanza kutekelezwa kidogo na nyienyie Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kikubwa, Waziri, Mheshimiwa Dkt. Mpango katika Kitabu chake cha Maendeleo; tathmini yake mwenyewe kwenye kitabu chake, amekiri kwa maneno yake na nitarejea na mengine jana walirejea Waheshimiwa Wabunge. Katika ukuaji wa uchumi bado hatujafika, pato la kila mtu bado hatujafika, mapato ya kodi ya Serikali kwa mwaka vis-à-vis pato la taifa bado hatujafika, uwiano wa mapato kwa pato taifa bado hatujafika, kiwango cha umaskini bado hatujafika, uwekezaji wa mitaji kutoka nje bado hatujafika, uzalishaji wa umeme bado hatujafika, usambazaji wa umeme bado hatujafika, vifo vya kina mama na watoto na huduma za maji vijijini bado hatujafika, kilimo bado hatujafika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali, Mheshimiwa Mwigulu tuliza mzuka, kama Serikali yenye wataalam wa uchumi na wa kupanga wanaweka mipango, wanashindwa kutimiza malengo, afadhali mengine wanaweza wakawa wamefika kidogo, inakaribia lakini mengine ni mbingu na ardhi then tuna shida na wataalam wetu. Wakati tunaelekea kwenye Mpango wa Tatu lazima tufanye tathmini, nimesema hivi mimi ni mkongwe unanisoma vizuri, Wabunge hapa wakati wa maswali asubuhi, swali la maji ulitoa maswali ya nyongeza mpaka unataka kutoa maswali ya ziada ya nyongeza huku umesimama lakini mimi niliyekuwepo wakati wa Mpango wa Kwanza huu wa miaka mitano (2011-2016) kati ya mwaka 2012-2014 asilimia 27 ya manunuzi ya nchi yalikwenda kwenye maji. Fedha iliyotumika kwa miradi ya maji kwa CCM hii hii kwa kipindi hicho tu na siyo maneno yangu mimi, ni maneno ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali aliyefanya special auditing akasema kati ya shilingi 2.7 trilioni zilizokuwa injected 49 percent ya miradi haifanyi kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mnapokuja hapa SGR, Stigler’s Gorge, what is that! Ndiyo maana watu wanatushangaa, lazima tu-move. Serikali ikiwa madarakani aidha umechaguliwa au umeingia kiunjanja, ni jukumu lako wewe kuhudumia wananchi. Kuhudumia wananchi siyo hisani viongozi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukianza kuamini na kuwa na mentality kwamba kuhudumia Watanzania ni hisani, ndiyo maana kuna vijana wadogo hapa wanatushangaa tokea wako primary wanaona wazee wazima tunaongelea Stigler’s Gorge, wanakuja secondary wanaona tunazungumzia SGR, wanakuja Bungeni wanakuta ngoma ile ile, wanajifunza nini kutoka kutoka kwetu?

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, (SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. HALIMA J. MDEE: Umeshaanza Mheshimiwa Jenista.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Halima Mdee, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Jenista Mhagama.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, (SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, sijui tumsaidieje Mheshimiwa Halima Mdee, hii miradi yote ambayo ya vielelezo, ni miradi ambayo kwa maamuzi thabiti ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi, utashi wa kisiasa wa Rais John Pombe Joseph Magufuli, ndani ya miaka mitano tu ya Serikali yake miradi hii imeanza kutekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama ilikuwa haijatekelezwa siku za nyuma si imeanza sasa kutekelezwa! Kuanza kutekelezwa kwa miradi hii kunaonyesha ni kwa kiasi gani Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuleta maendeleo endelevu ya Taifa la Tanzania. Kwa nini Mheshimiwa Halima asikubali jambo hilo? (Makofi/Kicheko)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Halima Mdee, unaipokea taaria hiyo.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Jenista alikuwepo kwenye Serikali zote hizi, Magufuli alikuwepo kwenye Serikali zote hizi…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Halima Mdee, ngoja kidogo, kwa Kanuni zetu hawa ni Waheshimiwa kwa hiyo wataje vyeo vyao.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Jenista alikuwepo kwenye Serikali zote hizi, Mheshimiwa Magufuli alikuwepo kwenye Serikali zote hizi na Serikali ya Awamu ya Tano iliahidi kwenye Mpango uliopita kupunguza kiwango cha umaskini kutoka asilimia 28 mpaka asilimia 16, mmeweza kupunguza kwa asilimia 2 tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nachotaka kusema hapa mentality ya kufikiria unapotoa ama unapotekeleza wajibu ni hisani, ndiyo haya unafikiria likijengwa daraja pale eti wananchi wa Tanzania wamesaidiwa, hawajasaidia kwa sababu mnakusanya kodi. Ninachowashauri hapa tukiwa tunaelekea Mpango wa Tatu tufanye tathmini tuone tumekosea wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kila mtu anajisifia, ooh, kuna ujenzi, sikiliza miaka mitano ya Mpango huu ujenzi imepewa trilioni 8 sasa kwa nini sekta ambayo mmewekeza trilioni 8 isikue? Hiki kilimo ambacho kila mtu anakizungumzia hapa na jana amezungumza aliyekuwa Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Muhongo kwamba kama tunataka hiki kimuhemuhe cha kusema nchi yetu ni tajiri kiwe reflected kwa wananchi kule chini tuwekeze kwenye maeneo yanayogusa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kilimo average ya kutoa bajeti ya maendeleo ni 17 percent kwa miaka mitano iliyopita. Hotuba ya Mheshimiwa Dkt. Mpango mwenyewe anasema eti miaka mitano kwenye kilimo tumetoa shilingi bilioni 188, hatusemi Serikali ilime, hapana, tunasema itengenezwe miundombinu wezeshi. Nchi hii ina utajiri wa umwangiliaji, hivi tutapoteza nini kwa mfano, hawa wakulima wetu wadogo wadogo tukisaidia kuweka mifumo thabiti ya umwagiliaji? Leo ni aibu asilimia 90…

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, (SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Halima Mdee, kuna taarifa.

WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Bashungwa, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Jenista.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, (SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee, Halima ni Mbunge mbobezi na mzoefu na anajua uchambuzi wa bajeti unavyokwenda. Uchambuzi wa bajeti unavyokwenda na unavyopangwa kwa utaratibu wa circle lakini utaratibu wa Serikali, bajeti ya kilimo haihesabiwi kwenye fedha zinazopelekwa kwenye Wizara ya Kilimo peke yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bajeti ya Kilimo, Halima anajua, ningemwomba Halima anapoweka hii hoja mezani aeleze bajeti ya kilimo iliyokuwa budgeted kwenye Wizara ya TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu, achukue bajeti zote za kisekta zinazoenda kuzungumzia sekta ya kilimo kwenye sekta mtambuka fungamanishi, akizichukua zile zote atakuja kupata bajeti halisi ya kilimo ambayo ilikuwa imetolewa na Serikali katika kipindi anachokisema.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Halima Mdee, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, siwezi kuipokea kwa sababu mimi nafanya rejea ya hotuba ya Mchumi mwenyewe wa nchi, Waziri Mpango. Sasa kama Mchumi wa nchi anasema tumetenga shilingi bilioni 188 mimi ni nani? Mheshimiwa Jenista Mhagama ni nani wa kubishana na Mchumi? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nachoshauri kupanga ni kuchagua. Tuna nia ya kusaidia Watanzania wenzetu lazima tuangalie sekta zinazogusa wananchi walio wengi.

MBUNGE FULANI: Muda hauishi? (Kicheko)

MHE. HALIMA J. MDEE: Sekta hii tumeipuuza sana lakini bado kwa heshima kubwa inachangia pato la Taifa kwa asilimia 26.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Halima, hiyo ni kengele ya pili.

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumpa taarifa Mheshimiwa.

MHE. HALIMA J. MDEE: Gwajima tulia.

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumpa taarifa kabla hajamaliza.

MWENYEKITI: Ngoja, ngoja. Mheshimiwa Halima Mdee, kengele ya pili imeshagonga.

MHE. HALIMA J. MDEE: Sawa namwambia atulie.

MWENYEKITI: Ahsante sana. (Makofi)