Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muhambwe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichukue nafasi hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwepo kwenye Bunge letu Tukufu. Pia nawashukuru wapiga kura wa Jimbo la Muhambwe kwa kuniwezesha kurudi kwa mara ya pili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita kwenye kitu kimoja tu ambacho napenda nikichangie kama kuisaidia Serikali yetu katika kuinua kipato. Hivi karibuni kwenye hotuba hii ambayo mimi binafsi naiona ni nzuri sana, kumekuwa na maelezo mengi sana ya Waheshimiwa Wajumbe na Wabunge kwa ujumla ya kuelezea jinsi ambavyo hawaridhiki na fedha iliyotengwa kwa ajili ya TARURA na wakawa wanapendekeza kwamba sasa tuangalie uwezekano wa kuhakikisha kwamba tutachukua pesa kutoka TANROADS.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe ushauri. Kwanza kabisa, hakuna kosa kubwa tutakalofanya kama tutakapojaribu kuondoa hiki kidogo ambacho wanacho TANROADS kwa njia yoyote ile. Isipokuwa kitu ambacho tunaweza kufanya ni kuhakikisha tunatafuta vyanzo vizuri na sahihi kwa ajili ya TARURA. Tunajua umuhimu wa TARURA kwa barabara zetu kuanzia vijijini mpaka barabara kuu na tunajua jinsi ambavyo wana-struggle, ukweli ni kwamba bajeti yao huwa ni ndogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona nije tu na mpango na niutoe kwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha auangalie kama utaweza kufaa. Mwaka 2020 kwenye kipindi kama hiki niliweza kuhudhuria kwenye Kamati ya Bunge ya Bajeti na nikaitoa kama proposal, ni jinsi gani tunaweza tukatumia sekta ya mawasiliano kuhakikisha kwamba tunapata fedha za kutosha kwa ajili ya kuwasaidia TARURA kuweza kufanya shughuli zao kwa ajili ya wananchi wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi hicho ambacho bado nasimamia kwenye wazo langu hilo, tuliwapendekezea watu wa Wizara ya Fedha kwamba tuongee na makampuni ya simu, tuweke tozo kidogo kabisa ambayo itawezesha TARURA kupata fedha. Tukawapa pendekezo; na nitaomba mnisikilize kwa makini, tuliwaelekeza tukawaambia bwana, tukiweka senti 25 kwa kila megabyte moja; sasa hivi Watanzania waliosajiliwa kwa kutumia line za simu wako milioni 50; na kati ya watu milioni 50, watu milioni 24 imesomeka kwamba wanatumia mitandao ya internet kwa njia mbalimbali na shughuli mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikasema tuchukue tu sample ya watu milioni 10, tusichukue yote milioni 24, tuchukue watu milioni 10 ambao wanatumia internet, nikasema tuweke tozo ya senti 25, isifike hata shilingi moja, tuweke senti 25 kwa kila megabyte moja. Nikasema kwamba kwa gigabyte moja ambayo ni megabyte 1,000, tukiweka hapo kwa senti 25, tutakuwa tumechangia Serikali shilingi 250 kwa gigabyte moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilienda mbali zaidi na nitaleta hiki kitu kwa maandishi kwa sababu najua itaisaidia Serikali. Kwanza kabisa, niwahakikishie Serikali, tusiwe waoga, hayo makampuni ya simu yamekuwa na ushirikiano mzuri sana na Serikali na yamekuwa yanachangia sana kwenye Serikali na hawawezi ku-complain. Isitoshe hakuna bei elekezi ya mtandao mmoja kwenda mtandao mwingine katika kutoa huduma kwa wateja wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukitumia watu milioni 10 ambapo kila mmoja anatoa shilingi 250, let’s say kwa wiki moja, tuchukulie tu kwamba kwa wiki moja mtu atatumia gigabyte moja, tutakuwa tumetengeneza shilingi bilioni 2.5. Uki-manipulate hiyo hesabu kwa muda wa mwezi ni shilingi bilioni 10 na kwa mwaka mzima ni shilingi bilioni 120 kwa bajeti ya shilingi bilioni 273 ya TARURA tutakuwa tumewaongezea kiasi cha pesa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Sawa. Mheshimiwa kengele imegonga lakini tufafanulie jambo moja. Hiyo senti 25 inalipa kampuni kwa ile gigabyte iliyoniuzia mimi au unapendekeza nikatwe mimi halafu kampuni ya simu ikusaidie kukusanya?
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza mteja ndiyo akatwe senti 25 kwa megabyte moja halafu zile kampuni wazipeleke Serikalini kama fedha ya Serikali. (Makofi)
MWENYEKITI: Haya, ahsante sana Mheshimiwa, muda wako umekwisha.
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)