Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nominated
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HUMPHREY H. POLEPOLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuungana na wenzangu kuchangia Mpango huu Maendeleo kwa Miaka Mitano kwa kuanza na kuainisha kazi nzuri ambayo imefanyika katika Mpango wa Pili chini ya uongozi wa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi na ningetamka mambo mawili muhimu, kazi kubwa imefanyika katika Mpango wa Pili katika kuimarisha uchumi mkubwa na umadhubuti wake (Macro level economy performance) ambayo ukifanya vizuri hapo inakwenda kwenye uchumi mdogo unaohusisha watu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kimoja cha kipekee kimefanyika hapa Tanzania ni kufanya haya mambo yote kwa wakati mmoja na nitatoa viashiria vichache kuonesha kwamba katika uchumi mkubwa kazi kubwa sana imefanyika katika Mpango wa Pili na tuna kila sababu ya kuendeleza mafanikio hayo katika Mpango wa Tatu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kiashiria kimoja cha ukuaji wa uchumi na katika uchumi mkubwa na ufanisi wake ni ujenzi; tumefanya ujenzi wa bandari kubwa na ndogo, tumefanya ujenzi wa viwanja vya ndege, tumefanya ujenzi wa barabara kote nchini Tanzania, tumefanya ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa, lakini ukiacha ujenzi imefanyika kazi kubwa sana ya kudhibiti mfumuko wa bei kutoka asilimia tano mpaka asilimia tatu kwa maana ya mfumuko wa bei wa jumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi nyingine kubwa imefanyika katika kuimarisha uchumi mkubwa ni kuweka nafuu ya kikodi kwa watumishi katika Pay As You Earn kutoka 12% mpaka 9%. Pia kumepunguzwa kwa kiasi kikubwa sana kwa tozo zenye kichefuchefu katika eneo la kilimo na madini na hapa ni makumi ya tozo ambazo zimefutwa. Kubwa kuliko yote ni uzalishaji wa umeme usafirishaji na usambazaji na hapa kazi kubwa imefanyika kufikia vijiji vyote na tumebakiza kama 2,000. Hoja ninayojaribu kuisema hapa ni kwamba umeme ambao tumezalisha mpaka sasa hivi tuna ziada, tulianza na megawatt 1,300 na sasa tuna 1,600 na hiyo ni ziada ya matumizi ambayo tunayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni kwamba, uchumi mkubwa unakwenda sambamba na uwekezaji na katika sekta binafsi na hapa utagundua kwamba mazingira wezeshi tumeyaweka katika kodi ya makampuni (corporate tax) ambayo tumeipunguza kutoka asilimia 30 mpaka asilimia 20 kwa viwanda vinavyohusika na kutengeneza madawa. Hii itawezesha viwanda hapa Tanzania kuanza kutengeneza dawa na kupunguza changamoto ya upatikanaji wa dawa kama ambavyo imepatikana wakati mwingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tulinde viwanda vya ndani kwa kuweka sera ambazo zitahakikisha kwamba bidhaa zinazoweza kuzalishwa ndani haziagizwi kutoka nje. Hapa napenda kupongeza uamuzi wa Serikali kuongeza kodi katika kuingiza sukari kutoka asilimia 25 mpaka 35 ili viwanda vya ndani viweze kuzalisha na kuuza sukari hapa nchini. Katika uchumi mkubwa pia utaangalia mzunguko wa fedha, wako watu wanapotosha wakati mwingine, lakini ukweli ni kwamba nikitoa kiashiria kimoja tu ya fedha tu zilizowekeza katika mawakala wa benki kutoka mwaka 2013 mpaka mwaka 2019, mzunguko wa fedha ambazo ameziweka mle ndani zilikuwa bilioni 28 tu, lakini mwaka 2019, zimefika trilioni tano, hili ni ongezeko kubwa kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sasa nijielekeze katika ushauri; rai yangu kwa Serikali ni kwamba, tufanye itakavyowezekana, miradi ya uzalishaji wa nishati tuikamilishe kabla Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli hajaenda. Sasa hivi tunatengeneza Stigler’s pale bwawa la Mwalimu Nyerere, megawatt 2,115, hiyo inakwenda tayari. Kwenye hotuba ya
Mheshimiwa Rais ameeleza miradi mingine karibu kumi ambayo itazalisha umeme na kuongeza uzalishaji wa umeme nchini kifani na kwa sababu tunazungumzia a competitive industry economy, yaani uchumi shindani wa viwanda, umeme ni kigezo muhimu sana cha kufanikiwa kwa viwanda nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nilipokuwa nikisoma Mpango, nimeangalia katika ukurasa wa 129, kiashiria cha Serikali hapa kinasema tunataka tuongeze umeme kutoka 1,600 ya sasa mpaka 4,900. Nikizitoa hapa tutabaki na 3,000 nikitoa 2,100 za Stigler’s tutabaki na 1,000, aah jamani! Mheshimiwa Rais ameeleza hapa Ruhuji megawatt 358, Rumakali megawatt 222, Kikonge megawatt 300, Mtwara gesi megawatt 300, Kinyerezi III na IV megawatt 600 na 300 mtawalia; na Somanga Fungu kwa gesi megawatt 330. Naishauri Serikali itazame ile miradi strategic ya kuzalisha umeme katika hii ambayo Rais ameelekeza ili tusije tukafika 2025 tumechukua ile ambayo kwa hakika haitaweza kutuvusha kwa maana hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nieleze tu katika viwanda na kilimo tujikite kwenye eneo moja kubwa, kutehamisha uunganishaji wa wakulima na masoko. Siku hizi Alibaba ni tajiri kwa sababu mtandaoni mtu unaweza kuuza korosho, mahindi na vitu kama hivyo. Nashauri, siku hizi simu hizi za kupangusa kila mtu anazo, lakini pia matumizi ya USSD code, inawezekana mkulima akawa na nyanya Ilula, asihangaike kuchukua lori zima kulipeleka Dar es Salaam, akatazama mle ndani akaona kuna soko, Dodoma au Morogoro… (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. HUMPHREY H. POLEPOLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kengele imegonga, basi nitaleta mchango wangu kwa maandishi. Naomba kuunga hoja. Ahsante. (Makofi)