Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza, napenda kuipongeza Serikali kwa commitment kubwa inayofanya katika sekta ya habari, mawasiliano na teknolojia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajielekeza kuzungumzia namna tunaweza tukaboresha mifumo ya kutumia huduma za fedha kwa njia za kimtandao. Kama tunavyofahamu, kutokana na changamoto kubwa ya ajira vijana wengi wamejielekeza katika kufanya ujasiriamali wa kimtandao ambao kwa kiasi kikubwa unatumia huduma za fedha za kimtandao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma za fedha za kimtandao zimewekwa pamoja na sababu nyingine, ili ziweze kumrahisishia huduma mfanyabiashara. Nafahamu hizi huduma za kifedha za kimtandao zinahusisha tozo ambazo zina kodi ambayo ni muhimu sana katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Serikali. Pamoja na dhamira hizo ambazo ni njema sana tozo kwa ajili ya kutumia huduma za kifedha kwa mitandao ni kubwa mno na hivyo inasababisha vijana wengi wasiweze kuwa na mazingira mazuri ya kufanya biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano. Leo hii ukiwa unatuma pesa shilingi 5,000/= tu kwa mtandao wa simu gharama yake ni shilingi 750/=, unaweza ukaona ni ndogo lakini ni 15% ya pesa ya mtu. Anayetoa shilingi 50,000/= anakatwa shilingi 2,700/= ni 5.4%; anayetoa shilingi 200,000/= anakatwa shilingi 3,700/= ni 1.9%. Kwanza unaona yule ambaye ni maskini kabisa wa chini ametoa shilingi 5,000/= anakatwa 15% ya pesa yake, yule ambaye anatoa shilingi 300,000/= anakatwa 1.9% ya pesa yake. Sasa hawa vijana ambao wanaanza biashara wataweza vipi kupambana katika soko hili la kimitandao? Hawana ajira, wanaamua kujiajiri kwenye mitandao na gharama zinakuwa kubwa kiasi hiki? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ukiamua kwa mfano leo unaamua kutuma ada kutoka Tigo Pesa kwenda NMB gharama yake kwa Sh.140,000/= unakatwa Sh.6,000/=. Kama una watoto watatu gharama yake ni Sh.18,000/=, kwa uchumi upi wa Mtanzania? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama ni kubwa mno, kijana anafanya kazi kwenye mtandao ili apate faida ya shilingi 10,000/= na shilingi 20,000/= lakini yote inaliwa kwenye tozo za huduma za fedha za kimtandao. Naomba Serikali iangalie upya hizi tozo ili ziweze kuleta unafuu kwa vijana ambao wanapambana kwenye mitandao ili kuweza kupata kula yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda kwenye huduma za internet, natambua tafiti zinaonesha Tanzania ndiyo ina tozo ndogo kabisa kwenye data, katika ukanda wote wa East Africa, lakini tatizo lipo kwenye upandishaji holela wa huduma za data (internet). Wiki moja iliyopita ukitoa shilingi 8,000/= kwa Tigo ulikuwa unapata GB 16, yaani kesho asubuhi watu wameamka wameweka 8,000/= wanunue GB 16 wanapewa GB tatu, hawajapewa taarifa kwamba huduma gharama yake zinaongezeka. Halafu sasa MB 300 unapata kwa Sh.1,000/= yaani kwa mfanyabiashara uki-post post mbili, hela imekwisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, shilingi 3,000/= unapata GB moja wakati shilingi 3,000/= ulikuwa unapata mpaka GB 5. Watanzania hawakupewa taarifa ya upandishaji wa gharama hizi yaani kampuni ya mawasiliano anaamka anaamua kupandisha gharama za mitandao kama anavyopenda. Pato la mtu mmoja-mmoja ni shilingi elfu moja na kitu, lakini unamfanya Mtanzania atumie gharama ya shilingi 3,000/= kwa siku kwenye huduma ya mawasiliano, sio sahihi. Naomba Serikali iangalie upya ili inusuri vijana hawa ambao wanatumia mitandao ya kijamii kujipatia kipato chao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ni la pili kutoka mwisho, sisi tunapolipa huduma, tunaweza kulipa huduma kupitia Master Card Visa pamoja na PayPal kulipia malipo nje ya nchi. Leo mimi kijana wa Kitanzania nikiamua kufungua website kutaka kutangaza bidhaa watu wa nje ya nchi waweze kununua kwenye website yangu hawawezi kulipa kupitia Master Card, PayPal, Visa au Credit Card hela iingie moja kwa moja kwenye benki yangu, lakini mimi nina uwezo wa kuwalipa wale wa nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa vijana tunawahimiza ubunifu, lakini ubunifu wao hauwezi kuwasaidia kwa sababu watu wa nje hawawezikuwalipa kwenye akaunti zao za benki. Naomba BoT na Wizara ya Fedha iangalie suala hili kumnusuru kijana huyu wa Kitanzania na kumwekea mazingira mazuri ya biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)