Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busanda
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kunipatia nafasi ya kuongea katika Bunge hili kuchangia katika Mpango huu wa Maendeleo wa Miaka Mitano na wa Mwaka Mmoja. Ni dhahiri kwamba, ukurasa wa tano umeonesha wazi kwamba, nguzo za Mpango huu wa Maendeleo zimejikita kwenye sehemu tatu; ya kwanza ni utawala bora. Utawala bora sina mashaka kwa namna ambavyo unaendeshwa sasa kwa sababu ya haki na uwajibikaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nguzo ya pili ni ukuaji wa uchumi; ukuaji wa uchumi tumeuona kwamba, uchumi unakua, lakini kuna mambo kadhaa ambayo tunatakiwa tuyapitie. Wabunge wengi wameeleza juu ya kilimo, ni kweli kabisa kwamba, Watanzania zaidi ya asilimia 75 wameajiriwa kwenye kilimo na bajeti tunayoipeleka kwenye kilimo ni ndogo sana. Kama hiyo graph ya ukuaji wa uchumi ni linear maana yake tunapoondoa tu kuwafanya wale wasihusike katika uchangiaji wa pato la Taifa, lazima uchumi wetu utaonekana haukui haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo iko hoja tunataka kuongeza bajeti, lakini sisi tunaotoka vijijini kule watu wamezalisha mchele haujauzwa hadi leo upo, mahindi yapo yamezalishwa hayajauzwa. Maana yake kuna hoja ya masoko hapa haijakaa vizuri ndani ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ndugu zangu wanaitwa TMX, wameshughulika na suala hili, lakini kila mmoja ana mpunga ndani, ana mahindi ndani na biashara haifanyiki. Kwa hiyo, tunapokwenda kwenye hoja hii, lazima tutafiti tujue kwamba, tuna masoko ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuna udongo wa kila aina mahali tunapoishi. Hii Wizara ya Kilimo inatakiwa ipewe fedha kwa ajili ya utafiti. Kuna mahali fulani niliwahi kuishi wakaniambia hapa hapahitaji mbolea udongo wake una madini mengi sana, maana yake hawana elimu ya kutosha kujua nini wanatakiwa kufanya kwenye kuzalisha. Kwa hiyo, niseme tu wazi tunahitaji kuchangia kwa kiwango kikubwa kwenye Wizara ya Kilimo, ili tuweze kufanikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kwenye ukuaji wa uchumi, ukiangalia vipaumbele kwenye ukurasa wa 101 inasema wazi kwamba, tutachochea uchumi shirikishi na shindani, lakini ukirudi kwenye ukurasa namba 64 kwenye Mpango huu, utagundua kwamba, kuna mahali fulani sekta binafsi haikuhusika vizuri kuna vitu ambavyo vilikwenda vya kichefuchefu. Ukiangalia Clause 3(iii), utagundua kuna habari ya ulipaji wa kodi imeandikwa pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninakotoka Katoro nina wafanyabiashara zaidi ya 5,000 pale Mjini Katoro, wana ugomvi na TRA kuanzia asubuhi hadi jioni. Nina mashaka sasa kama tunataka kukuza uwekezaji na uchumi, hiyo ni katika kipaumbele cha tatu, inaonekana kuna tatizo kati ya TRA na wafanyabiashara, tutakuzaje sasa uwekezaji na uchumi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima sasa hivi tuanze kutengeneza kama ni ushirikishi na shindani tuhakikishe kwamba, TRA wanafanya urafiki na hawa wafanyabiashara wasiwakadirie vitu ambavyo havipo. TRA wamekuwa wanarudi nyuma miaka mitano halafu wanamwambia mtu sasa unatakiwa kulipa milioni 300; milioni 300 na yeye mtaji wake ni milioni 150, kimsingi huyu amefilisika. Kwa hiyo, niombe sana hoja yetu ya msingi ni kuhakikisha kwamba, sasa uchumi wetu unaweza ukakua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona madini yatakua kutoka asilimia 5.2 kwenda asilimia 10. Tumeona kilimo kinatakiwa kichangie kutoka asilimia 27, bahati mbaya inaonekana mpaka baada ya miaka mitano hakitakuwa kimechangia sana ukiangalia kwenye kumbukumbu ukurasa 104, lakini niseme tu wazi ni lazima tuhakikishe kwamba sasa hivi masoko yapo, lakini tukiendelea kuzalisha na masoko hayapo tutakuwa tumefanya mchezo wa kuigiza na uchumi wetu hautaweza kupanda kwa sababu, wananchi hawatazalisha sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)