Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Taifa tunapoamua kupanga katika mipango mbalimbali ya kitaifa, dhamira ni kuhakikisha mipango inatekelezeka kwa lengo la kukuza uchumi wetu, kwa lengo la kuhakikisha tunaongeza pato la Mtanzania mmoja mmoja na kwa lengo la kuhakikisha tunaongeza ajira kwa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe unajua, katika mipango yote suala la Mpango wa Mradi wa Liganga na Mchuchuma ni takribani zaidi ya miaka 20 linaongelewa katika Bunge hili. Liganga na Mchuchuma ilikuwepo katika mipango yote. Lazima tujiulize Serikali ya Chama cha Mapinduzi mna dhamira, mikakati na malengo ya kuhakikisha mnamuondoa Mtanzania kwenye umasikini na mna lengo la kuinua pato la Mtanzania mmoja mmoja au tunafanya kazi kwa mazoea? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu imejaliwa kuwa na madini ya chuma takribani tani milioni 126. Tumejaliwa kuwa na madini ya makaa ya mawe takribani tani milioni 428. Leo tunajenga reli ili ule mradi ukamilike unatarajiwa kutumia shilingi trilioni 17 na katika hizo ziko pesa za mikopo lakini tunaagiza chuma kutoka nje wakati Mwenyezi Mungu ametupa chuma chetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyozungumza kupitia Shirika letu la NDC ambalo lina hisa asilimia 20 na kampuni ya Kichina tumeingia mkataba zaidi ya miaka saba lakini hakuna kinachoendelea katika Mradi wa Liganga na Mchuchuma. Sheria ya Madini, kifungu cha 47(2) kimeweka wazi ukipewa mkataba na leseni unatakiwa utekeleze ndani ya miezi 18. Tuna hisa asilimia 20 kupitia NDC, kuna Mchina ana asilimia 80 amevunja sheria, anafichwa. Kuna interest gani, kuna nini kinajificha huku pesa tunakwenda kukopa nje, tunaagiza chuma kwa kukopa nje halafu kuna mtu tunambeba, tuna madini tumepewa na Mwenyezi Mungu, tuko serious? Halafu tukihoji mnatupa tu maneno, timizeni wajibu wenu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi kule wa Njombe na Ludewa hawaendelezi maeneo yao. Wamesema wapishe eneo la mradi…
T A A R I F A
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UWEKEZAJI): Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ester, upewe taarifa; Mheshimiwa Waziri nimekuona.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UWEKEZAJI): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa mzungumzaji anayeendelea kuwa Mradi wa Liganga na Mchuchuma una vipengele sita. Vipengele vitano vimeshafanyika, kimebaki kipengele kimoja ambacho kinahusu mkataba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii mikubwa ina maslahi makubwa kwa nchi. Unapoingia mikataba na mashirika ya kimataifa lazima uwe makini. Kwa hiyo, majadiliano yanaendelea na yapo katika hatua za mwisho kuhakikisha kwamba mkataba huu unakuwa na maslahi mapana. Kwa hiyo, anavyosema hakuna kinachoendelea siyo sahihi kwa sababu ina mambo sita, matano yameshafanyika, limebaki jambo moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba apokee taarifa hiyo.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ester Bulaya, pokea hiyo taarifa.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sipokei taarifa, najua ni Waziri mgeni. Hili jambo tangu enzi za mama Mary Nagu, vipengele vitano miaka 20 brother? Hii ni taarifa ya sasa hivi ya Waziri na inasema hiyo kampuni haina uwezo wa kuwekeza dola za Kimarekani bilioni 2.9. Shame! Okoeni pesa za Watanzania, tunaagiza chuma kutoka nje, Mwenyezi Mungu ametupa chuma chetu; tunahitaji nini? Halafu unajibu majibu kama hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Ludewa, Njombe, maeneo haya takribani zaidi ya miaka saba wameshindwa kuyaendeleza. Mnasema Serikali ya wanyonge wakati kuna watu kule mnawasimamisha zaidi ya miaka saba hawaendelezi maeneo yao, hawajalipwa fidia, mnamlindwa mwekezaji mnasema maslahi ya nchi; yako wapi wakati huyu amevunja Sheria ya Madini, kifungu cha 47(2) miezi 18 imeisha, like seriously? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba mtimize wajibu wenu. Haya madeni wanakuja kuyalipa Watanzania. Kuna mtu alisema dunia ni chuma, chuma tunacho tunaagiza nje kwa hela za mikopo; kweli? Halafu tunakuja tunafanya mzaha hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Najua Serikali imekwenda kuchukua pesa tena kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwenda kuwekeza kwenye viwanda. Hatukatai kuchukua fedha za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuwekeza kwenye viwanda kama kuna dhamira njema na Serikali mnalipa hizo fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia Ripoti ya CAG, inaonesha hali ya Mifuko ni dhoofulihali, mifuko iko taabani. Ripoti ya mwanzo…
T A A R I F A
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ester Bulaya, upokee taafifa kutoka kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba mpaka leo napoongea hapa kama Waziri wa sekta, thamani ya Mifuko hii ya Hifadhi ya Jamii imeshapanda mpaka shilingi trilioni 11.510. Sasa kama thamani ya Mifuko hii imeshafika shilingi trilioni 11.510 mpaka sasa, hicho ni kiashiria kwamba sekta inakua na siyo inakufa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nani mwenye majukumu ya kusema kwamba sekta inakufa? Ukitaka kuwa na mamlaka ya kusema mifuko inakufa ni lazima ufanye actuarial. Sasa hivi ndiyo tupo kwenye huo utaratibu wa actuarial. Mtathmini ameshaanza kufanya utathmini wa Mfuko ya Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma, manunuzi ya Mtathmini kwa ajili ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa sekta binafsi yameshakamilika. Kwa hiyo, taarifa ya Mthamini ndiyo itakayokuja kutupa uelekeo mzima wa sekta. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mamlaka haya Mheshimiwa Ester ya kusema kwamba mifuko imekufa kabla Mtathmini hajatoa ripoti anayatoa wapi? CAG anafanya ukaguzi wa mwenendo wa fedha, Mtathmini kwa vigezo vya Umoja wa Mataifa na Shirika la Kazi la ILO ndiye atakayetupa mwelekeo wa Mifuko na sekta. Kwa hiyo, Mheshimiwa Ester asubiri, asianze kuwahisha shughuli mapema. (Makofi)
MWENYEKITI: Taarifa hiyo Mheshimiwa Ester Bulaya, unaipokea?
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza amejichanganya mwenyewe, naye amejuaje hiyo thamani kama bado tathmini haijafanywa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tathmini ya kwanza kabla Mifuko haijaunganishwa Mkaguzi Mkuu wa Serikali wa kwenu amesema mifuko haina uwezo wa kulipa madeni yake pamoja na madeni ya wastaafu. Amefanya tena ukaguzi na wewe unajua tarehe moja hapa tulipitisha Sheria ya Kikokotoo ukaliahidi Bunge na wewe ukaponea chupuchupu akaondolewa yule Mkurugenzi mwingine, ukaahidi hapa Bungeni mnakwenda kufanya tathmini ya madeni, huu mwaka wa nne sister, hukufanya. (Makofi)
T A A R I F A
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri wa Nchi, taarifa.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua ni lazima tutoe taarifa kwa sababu watu wasipotoshe mambo humu ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tathmini ya Mtathmini wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii ilifanyika kwa mara ya mwisho mwaka 2016/2017. Tathmini ile tuliifanya baada ya kupata maoni kutoka kwa wadau mbalimbali na walitushauri namna ya kwenda kwenye merging. Tulipitisha sheria hapa ndani kwamba mwaka mmoja, miwili baada ya merging ndiyo sasa tutafanya tathmini yenye uhaliasia wa kujua baada ya merging mifuko yote na sekta inakwendaje. Sasa asichanganye tathmini ya merging na tathmini hii baada ya merging tunakwendaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo masuala mengine ya kupona au kutokupona siyo kazi yake, iko mamlaka ya kutathmini haya yote. Mimi nasimama kama Waziri wa sekta namwambia Mheshimiwa Ester, tathmini ni mbili; ya merging ilishakwisha, tunasubiri ya mwenendo tunaokwenda sasa hivi. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ester Bulaya, taarifa hiyo, ipokee.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, dada yangu atulie tu, hayo mambo mimi hayanihusu ila ninachomwambia, mlipe madeni. Mnakopa hamfanyi tathmini, wastaafu hawalipwi humu ndani kila Mbunge anapiga kelele. Haya, kwa tathmini tu aliyoifanya CAG Serikali mnadaiwa shilingi trilioni mbili na bilioni mia nne kumi na saba, fedha za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo sijazungumzia deni la PSPF, takribani shilingi trilioni 11, mliwaamrisha wawalipe watu ambao hawachangii. Leo kwenye viwanda 12 mmekwenda kuchota tena fedha shilingi bilioni 339 kuendelea kuwekeza huku mnadaiwa shilingi trilioni mbili.
T A A R I F A
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MBUNGE FULANI: Eeeh.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri wa Nchi, tafadhali.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, utanisamehe sana. Unajua ni lazima Bunge hili lielewe mwelekeo wetu ni nini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa sheria, kazi ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya kwanza ni kuandikisha wanachama, ya pili ni kukusanya michango. Huwezi ukakusanya michango ukaitunza benki eti isubiri tu watu watakapostaafu uwape. Kazi ya tatu ni kuwekeza na unapowekeza michango unaongeza thamani ya ile michango muda utakapofika uweze kuwalipa wastaafu kwa kuzingatia sheria na taratibu zinazowekwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, siyo kweli kwamba Serikali inajichoteachotea tu, hapana. Serikali inawekeza kwenye uwekezaji wenye tija ili muda unapofika mafao yaweze kupatikana.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Sasa kama
anataka hiyo michango iwekwe tu benki bila kuongeza thamani utapata wapi fedha? Kwa hiyo, Mheshimiwa Ester aelewe hesabu hizi za hifadhi ya jamii, azielewe vizuri.
MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Halima, haiwezekani taarifa juu ya taarifa. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Ester Bulaya, unapokea taarifa?
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sipokei. Halafu anajua mimi nilikuwa Waziri Kivuli wa Sera na Uratibu wa Bunge, anajua nilivyomkimbiza humu ndani kupitia Sheria ya Kikokotoo na Mheshimiwa anazungumzia michango, anataka nije huko? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta zenu za Kiserikali, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi mliacha kupeleka michango shilingi bilioni 85; Mfuko wa Hifadhi ya Jamii shilingi bilioni 61; Mfuko wa Bima ya Afya bilioni 24 michango mlichelewa ninyi ndani ya siku 30, unazungumzia michango? Nazungumzia mlipe madeni, muwekeze kwenye maeneo ya mikakati. Hizi pesa siyo zenu, ninyi ni wasimamizi, pesa hizi za wastaafu wa taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi hatuoni dhambi kila Mbunge akisimama humu kuna wastaafu wana miaka miwili, wengine miezi sita hawajalipwa halafu hela zao mlizokopa hamlipi, mnachukua zingine mnakwenda kuwekeza, kwanza mmefanya tathmini hivyo viwanda vinalipa; mmefanya? (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipeni pesa za wastaafu wa nchi hii, wamelitumikia taifa hili kwa jasho la damu. Mnataka morali iongezeke kwa hawa waliopo kazini…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Ester Bulaya, muda hauko upande wako, muda umekwisha. (Makofi)