Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nkenge
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. FLORENT G. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nafasi ya pekee nishukuru kwa nafasi ya kuchangia Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano. Nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kutupa nguvu na sisi wote kuwa hapa kwa ajili ya kujadili Mpango huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango huu ambao umeletwa kwetu ni mpango mzuri na faraja kubwa ni kwamba, katika Mpango huo takribani asilimia 65 unatekelezwa kwa mapato ya ndani ya nchi yetu. Kuna maeneo machache ambayo mimi nataka nijielekeze kwa sababu ya huo muda wa dakika tano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kwanza, tunaona key players ambao watahusika katika kutekeleza Mpango huu ni Halmashauri zetu za Wilaya kupitia Wakurugenzi wetu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Majiji na Miji, lakini pia na Wakuu wao wa Idara pamoja na watumishi wote ndani ya halmashauri hizo. Ni jambo jema kwa kiongozi yeyote kuhakikisha kwamba, mazingira ya wale wote ambao watahusika katika kutekeleza Mpango huu kwa kiasi kikubwa yameboreshwa na changamoto zile ambazo wanakabiliana nazo zimetatuliwa ili waweze kutekeleza Mpango wetu vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme katika eneo hili la Wakurugenzi wa Wilaya pamoja na Wakuu wa Idara limekuwa ni eneo ambalo lina changamoto nyingi sana na hasa kutopewa mazingira mazuri kwa ajili ya kutekeleza mipango mingi ya Serikali. Badala yake unakuta katika eneo kubwa Wakurugenzi wamekuwa wakishughulishwa na shughuli nyingine ambazo hazina tija kubwa kwa Serikali na value for money haipo. Unakuta kuna tume nyingi ndogondogo zimeletwa kutoka ofisi zetu za Wakuu wa Wilaya, kutoka kwenye ofisi zetu za Makatibu Tawala wa Mikoa na kutoka kwa Wakuu wa Mikoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nyingine ukiziangalia natija yake kwa kweli unaona zinamfanya Mkurugenzi badala ya ku-focus kwenye suala la msingi na akajikita kwenye kutekeleza Mpango anashughulika kujibu hoja ambazo kimsingi nyingine unaona tija yake kwa Taifa letu haipo. Kwa hiyo, niombe sana mazingira wezeshi ya Wakurugenzi wetu wa Halmashauri za Wilaya pamoja na wasaidizi wao ambao ni Wakuu wa Idara ziweze kutolewa na waweze kutekeleza Mpango huu, ili tuweze kufikia malengo mahususi ya ndani ya miaka mitano tuwe tumefikia malengo yote ambayo yameainishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu la pili katika eneo hili, ni kwenye sekta ya ardhi. Mwaka 2000 Serikali ilikuja na mpango mzuri wa retention scheme ya fedha ya kodi yote ilikuwa inatolewa katika viwanja na mashamba, ikawa inakusanywa inapelekwa serikalini, lakini asilimia 20 inarudi.
Hiyo fedha ilisaidia sana katika kupanga na kupima maeneo yote kupitia Serikali zetu za Halmashauri za Wilaya, lakini mwaka 2011 Serikali kwa kuona ubora wa kazi ile iliongeza ile percentage ya retention scheme ikawa asilimia 30 na kazi zilizendelea kufanyika kwa ubora zaidi, zikapangwa na maeneo yakaainishwa, fursa za uwekezaji zikija zinakuta eneo tayari limeshapangwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme mwaka 2015/2016 retention scheme hiyo ilitolewa na Wakurugenzi wa Wilaya waliendelea kuhangaika kudai zile fedha zitoke Wizara ya Fedha, hakukuwa na majibu. Mwaka 2017 yakatolewa maelekezo kwamba, retention scheme ilifutwa katika hotuba ya bajeti ya mwaka 2015/2016 kupitia Wizara ya Fedha na Mipango. Zile fedha kazi ilikuwa inafanyika kipindi hicho haikutolewa maelekezo, sasa hizo kazi zinafanyika kupitia bajeti ipi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka leo Halmashauri za Wilaya kupitia Idara ya Ardhi, zimebaki zimekatwa miguu, kazi hizo hazifanyiki kwa ufanisi. Tunatambua kazi nzuri ambayo Wizara ya ardhi imefanya kwa kutatua migogoro, lakini kwenye suala la kupima na kupanga na kudai fedha ambazo zinatakiwa ni masuuli ya Serikali yake, imebaki ni giza. Tuwaombe kwa muktadha huo hiyo retention scheme irudi na irudi katika asilimia 40 ili hizo kazi zifanyike kwa kuzingatia dira ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru. Naunga mkono Mpango ni mzuri kwa ajili ya maslahi ya Taifa letu. (Makofi)