Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makete
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru kwa kupewa nafasi ili niweze kuwasilisha mambo machache ya kuishauri Serikali. Vilevile niishukuru Serikali kwa Mpango huu wa Miaka Mitano na hata huu wa Mwaka Mmoja ambao umeletwa mbele yetu kwa ajili ya kuujadili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie mambo matatu. Jambo la kwanza ambalo nataka kulizungumzia ni kwenye sekta ya elimu. Kwenye sekta ya elimu nataka kuzungumzia jambo moja. Rais wetu tuliye naye kwa sasa alikuja na mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba, kila shule inakuwa na madawati. Mpango huu ambao Rais alituletea hatujauona nini ambacho Serikali inapanga kwenda kukifanya kuhakikisha kwamba, kila mwaka shule zinakuwa na uhakika wa madawati kuliko kuwa na huu mtindo wa zimamoto. Sijaona mpango wa kuona Serikali na sekta ya viwanda wakijadiliana kwamba, wana uwezo wa kujenga angalau kiwanda kimoja cha kimkakati Mkoa wa Njombe au mkoa wowote ambao unatoa malighafi kama mbao, ili Serikali iweze kupata madawati kwa uhakika kwa ajili ya shule zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukulia mfano mwaka 1985, Mwalimu Nyerere aliamua kujenga kiwanda cha Mgololo kwa ajili ya karatasi, ili shule zetu ziwe na uhakika wa kupata madaftari. Kiwanda hiki kilifanikiwa, lakini kwa sasa kwenye hili suala la madawati hatuoni jitihada zozote ambazo zinafanyika za makusudi za Serikali kuona inajenga kiwanda ambacho kinaweza kikasaidia kupata furniture mbalimbali kwa ajili ya Serikali yetu na kwa ajili ya shule zetu. Sisi watu wa Mkoa wa Njombe tuko tayari ku-offer maeneo kama haya ya viwanda kusaidia Serikali yetu iweze kupata haya mambo ya madawati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo nataka nichangie; wewe ni Mbunge wa Kongwa, NARCO ilianzishwa kwa ajili ya kuendesha hifadhi za Taifa, lakini tumeona NARCO ikijikita kwenye kutatua tu migogoro. Miaka inaenda, miaka inarudi hifadhi ya Kongwa pale toka Nyerere alivyoiacha ng’ombe ni walewale inawezekana na idadi imepungua, hakuna ng’ombe wanaoongezeka. NARCO inafanya kazi gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu, wewe kwako Kongwa pale, kuna eneo kubwa ambalo hata Watanzania wangetengewa tu sehemu kidogo tu wapewe vile vitalu wafuge, angalau tungeona kwamba, kuna jitihada zinafanyika. Leo ukienda pale Ruvu mradi wa zaidi ya bilioni
5.7 wa machinjio ya kisasa umekufa. NARCO wapo na mambo yanaendelea, wamejikita Misenyi, wamejikita Kagera kwenye kutatua migogoro ya wafugaji tu, lakini NARCO haina mkakati wowote ambao tunauona kwenye Mpango hapa ukurasa wa 89, Kuendeleza Ranch za Taifa. Maeneo yamebaki ni makubwa, hayana msaada wowote kwa Watanzania, ni vema wananchi wangegawiwa, waweze kufuga ili Serikali iweze kukusanya kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ni kwenye sekta ya wafanyabiashara. Hivi ninavyozungumza wafanyabiashara Makete, akina mama mafundi cherehani wanaambiwa wawe na mashine ya EFD. Ni masikitiko makubwa kwamba huyu mtu ana kitenge anashona anaambiwa awe na mashine ya EFD. Kodi now is not to collect they are just trying to grab it kitu ambacho siyo kizuri kwa sababu wananchi wetu wana uchumi mdogo, wana tozo nyingi lakini pili ukamuaji wake umekuwa ni wa tofauti. Hata ng’ombe unayemkamua unatafuta jinsi ya kumkamua, unamlisha, unazungumza naye lakini sisi TRA yetu hawafanyi jambo hilo, wanakusanya kodi kwa nguvu. Pia naendelea kusisitiza tozo ni nyingi na zimegeuka kero kwa wafanyabiashara wadogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasihi na naomba TRA watafute mazingira bora na salama. Mbona Rais ametusaidia vitambulisho vya wajasiriamali vimeondoa kero za wafanyabiashara wetu kukamatwa mitaani na mgambo, watafute njia sahihi ya kukusanya kodi. Nashauri wakusanye kodi kwa utaratibu siyo kutuma tax force kama Mheshimiwa Nape alivyosema, wanaenda wanakamata maofisi ya watu na kompyuta za watu, huyo mtu utegemee kesho akusaidie tena kulipa kodi? Ni jambo ambalo linasikitisha, tunaomba TRA wasaidie wafanyabiashara wetu wadogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kama ambavyo leo tuna vitabu vinavyoonyesha kwamba Wizara ya Kilimo kuna tozo ambazo imeziondoa kwa maana kwamba ni tozo kero, ndivyo tunavyotamani kwamba keshokutwa kwenye Bunge linalofuata au Bunge la mwakani tuje na kitabu kutoka TRA kinachosema hizi tozo ambazo ni za hovyo kwa wafanyabiashara zimepungua kwa sababu wafanyabiashara wetu wanaumizwa. Vijana wadogo ajira mtaani hamna wakitaka kufungua biashara TRA wameingia, watu wa OSHA wameingia, watu wa Bima wameingia, watu wa lift wameingia yaani hadi kukagua lift kukagua ni Sh.400,000 kwa mwaka, lift? Sasa huyu mtu ata-survive vipi na tunatamani tuendelee kukusanya kodi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali hii nchi itajengwa na wenye moyo ambao ni sisi lakini kama mkiendelea kubomoa wafanyabiashara wadogo hatuwezi kukusanya kodi. Mwisho wa siku tunachoomba Wizara husika watuletee takwimu kama idadi ya wafanyabiashara inaongezeka au inapungua kwenye taifa hili. Kwa sababu kila siku wafanyabiashara wanalia kutokana na changamoto za tozo, wapunguze tozo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, mchango mwingine nitaleta kwa maandishi lakini kwa kweli Watanzania wana matumaini makubwa na Mpango huu, naunga mkono hoja. (Makofi)