Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aliyenijalia afya niweze kusimama tena ndani ya Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya dakika tano, nitazungumza kwa uchache. Tunapozungumzia Mpango wa Miaka Mitano tunazungumzia Dira ya Taifa. Napozungumzia Dira ya Taifa lazima nitazame wimbi kubwa la vijana ambao wamekosa ajira. Tunapozungumzia wimbi kubwa la vijana lazima tutafute suluhisho kupitia Dira ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ajira ambazo zinatolewa Serikalini lakini bado tunarudi kwenye kilimo kwamba inawezakana ikawa mwarobaini au ikasaidia angalau kwa hili tatizo la ajira. Ukizungumzia kilimo cha Tanzania, nitatoa takwimu ya 2019 – 2020, wakulima ambao walilima 2019/2020 waliotumia mbegu bora ni asilimia 20 tu; waliotumia mbolea za viwandani asilimia 20, hapo ndiyo tunarudi kwenye lengo kweli kilimo ni uti wa mgongo, kitakwenda kutatua tatizo hili la ajira?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunazungumza hivyo siyo kwamba tuna shida ya ardhi kwenye nchi yetu, ardhi ipo na wataalam wapo wanalipwa fedha, shida nini kwenye Serikali yetu ya Tanzania kwenye suala la kilimo? Kama bajeti tunapitisha na mipango inaletwa hapa na inapoletwa naamini kabisa wanakuwa wamewashirikisha wataalam wetu huko chini, shida inakuwa ni nini Zaidi? Kupanga mpango ni jambo moja na kupeleka fedha ni jambo lingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizungumzia 2015-2020, hekta zilizoongezeka kwenye umwangiliaji ni 233,339. Leo kwenye Mpango huu tunazungumzia kwenda kufikia hekta milioni moja na laki mbili. Nilitamani kujua tu kuna miujiza gani utakaotumika hapo wa kufikia hekta milioni moja na laki mbili wakati kwa miaka mitano tunazungumzia laki mbili na thelathini na tatu mia tatu thelathini na tisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo machache tu ya kushauri, kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais nilijikita hapo na leo narudia. Kama tunataka kuboresha kilimo chetu ni lazima kwenye Mpango fedha zitengwe kwa ajili ya kupelekwa kwenye vyuo vya utafiti. Kama kweli tuna nia njema ya kuokoa Taifa letu lazima tutenge fedha za kutosha tupeleke kwenye vyuo vya utafiti. Tukipata fedha za kutosha mbegu zenyewe zitakuwa bora, tukipata mbegu bora lazima tutatenga fedha kwa ajili ya kupima udongo kujua udongo huu unafaa kwa zao lipi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunazungumzia ngano, ukitazama Mkoa wa Rukwa tunalima ngano sana lakini kama tunasema hitaji la Taifa letu ni ngano Serikali imejipangaje kwenye Mpango huu kwenda kupima maeneo ambayo yanaweza kufaa kwa kilimo cha ngano ili iendelee kuzalishwa kwa wingi Tanzania? Utakuta ni wimbo ambao tunauimba tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hivyo, kuna mikoa ambayo inazalisha sana mpunga, Mkoa wa Rukwa ni miongoni mwao lakini ukiangalia kwenye Mpango hapa hakuna kitu ambacho kimetengwa kwa ajili ya kwenda kuongeza uzalishaji wa mpunga na ili twende kwenye viwanda ni lazima tuboreshe raw material. Kwenye raw material mbolea leo Mkoa wa Rukwa mfuko mmoja Sh.65,000 wakati gunia la mahindi Sh.30,000, unaweza ukafikiri hapo huyu mkulima auze gunia ngapi ndiyo anunue mfuko mmoja wa mbolea? Je, kilimo kitakua au kitarudi nyuma?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunazungumzia viwanda nashauri tujue Tanzania tunahitaji viwanda vya aina gani. Viwanda vya kwanza vinavyohitajika ili tupunguze gharama za mbolea lazima tuwe na kiwanda kinachozalisha mbolea Tanzania ili wakulima wapate mbolea kwa bei rahisi. Tukiwa tumepeleka na mbegu bora tunazungumzia sasa kilimo cha uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa pili lazima tupeleke Maafisa Ugani wa kutosha kwenye kata ambazo zinazoongoza kwa kilimo. Leo kuna Maafisa Kilimo wapo mjini, hatukatai haa na mjini wanalima lakini kwa sababu ni wachache basi hao wachache wapelekeni maeneo ambayo wanazalisha, maeneo ambayo wanaendesha kilimo tujue kwamba tuko serious na kilimo hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye miradi ya umwagiliaji tunatambua kwamba Serikali imepeleka fedha nyingi ikiwemo Mkoa wa Rukwa lakini miradi hiyo haifanyi kazi. Lengo la Serikali ni nini? Kabla leo hatujabuni miradi mipya tupeleke fedha tukamalizie miradi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)