Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kahama Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Niungane na Wabunge wenzangu kwenye kuchangia Mpango huu wa Miaka Mitano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo mawili au matatu kama muda utaniruhusu. La kwanza; juzi Mheshimiwa Rais alipita kule Kahama akiwa anatokea Chato, alisimama Kahama. Haikuwa nia yangu mimi kueleza matatizo yale ya shule na afya lakini ilibidi kuyaongea ingawaje ni mambo ya Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wa shule wajaribu kuja na mawazo mapya. Hivi ninavyoongea Gazeti la Nipashe la leo wanafunzi waliochaguliwa kwenda kidato cha kwanza Mkoa wa Shinyanga ni 20,000 lakini wanafunzi 7,400 hawajulikani walipo na hawajahudhuria. Sijui sasa hata watakaokwenda form one, je watafika form four? Watakaofika labda robo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hili wala siyo la Serikali kutoa pesa. Sheria ilizoweka na utapeli ulioingia shuleni, shule imehama kwenye elimu imekwenda kwenye biashara. Ukiiona orodha ya karatasi ya mwanafunzi kutoka darasa la saba kwenda form one, akikuletea mtoto utamwambia ngoja nile kwanza. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vitu vinavyosemwa mle ndani mwananchi wa kawaida wa kijijini hawezi. Mfanyakazi wa kawaida wa mshahara wa laki tatu, hawezi. Vitu vinavyotakiwa ni kweli vitawezekana au tutaongeza rushwa? Wanakijiji wao wamekataa lakini mfanyakazi itabidi aende kwenye rushwa au aibe ili ampeleke mtoto wake shule.
MWENYEKITI: Unazungumzia joining instructions? Ile karatasi ya…
MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, orodha ya vifaa vinavyotakiwa.
MWENYEKITI: Orodha ya vifaa ili aweze kujiunga na form one.
MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo. Orodha ya vifaa hivyo haina uhusiano wowote na elimu; ni utapeli mtupu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanafunzi wa kijijini kweli anahitaji tracksuit; kweli? Mheshimiwa Waziri yuko hapa na bahati nzuri hizi ni ripoti za Shinyanga, tunaomba na Mheshimiwa Waziri, Uzuri Mheshimiwa Waziri Dkt. Mpango na Waziri wa Elimu wote ni wa Kigoma, watupe na wao ripoti zao kama kweli watu wa Kigoma wanaweza kununua viatu vyeusi. Kiatu cheusi original ni Sh.35,000 mpaka shilingi 40,000, hivi vingine vyote vinapigwa dye na Machinga vinakuwa vyeusi, baada ya wiki tatu vinarudia kuwa vyeupe. Sasa kuna sababu gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado Waheshimiwa hawa, Mheshimiwa Waziri wa Elimu ni Profesa, Mheshimiwa Dkt. Mpango pale ni doctor. Kweli na kutembea kote, leo bado tunahusudu viatu kweli viwe ndiyo chanzo cha elimu cha kwenda kumkabili mtu. Wenzetu wangeliangalia sana. Nusu ya wanafunzi hawakwenda; haiwezekani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili la elimu naona Wabunge wanajaribu kuliongeaongea lakini linahitaji maongezi marefu sana. Ni kweli mwanakijiji unamchukua mtoto wake asubuhi saa 12 unakwenda kumkimbiza mchaka mchaka baadaye anaingia darasani, saa tatu, saa nne. Kwa nini asiende saa tano amemsaidia mzazi wake asubuhi, amefanya na kazi ili aende saa tano amekula. (Makofi/ Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kama tutakataa, tutafanyaje. Huko mwisho hatuna ajira, tunakuja kuwaambia warudi nyumbani baada ya kuwa na degree. Wewe ulimchukua mtoto wangu anakula mihogo na viazi, unanirudishia anakula chipsi, soseji na mayai unakuja kukaa naye vipi nyumbani. Haiwezekani. (Makofi/Kicheko)
MWENYEKITI: Waheshimiwa mnacheka lakini ni ukweli kabisa, these are facts of life. Endelea Mheshimiwa Kishimba.
MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, unamrudisha mtu unamwambia akajitegemee, anajitegemea naye vipi? Sisi kule kijijini hata kuku akila mayai yake anachomwa mdomo na huyo ni yule anayetaga vizuri kama hatagi vizuri kesho yake anapelekwa kwenda kuuzwa. Sasa unanirudishia mtu anayekula mayai mimi nitakaa naye vipi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ni vizuri wenzetu wa Wizara ya Elimu waje na mawazo mapya. Academy za mpira ninyi mnakubali watu wafundishwe wakiwa wadogo, mnakatazaje watoto wetu kulima, kuchunga asubuhi, kufanya biashara za duka ili waende mchana; kwani watapata hasara gani? Hata kama ikitokea akawa mtoro ameshajua biashara kuna ubaya gani? Mtuambie ubaya wake nini. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ninyi wenyewe mna-confirm, Mheshimiwa wa Mipango kule amesema ana watu wana miaka nane hawana kazi, je, familia zao mnazihesabuje na ninyi Serikali mnataka hela yenu. Mimi nilikuja na hoja hapa kwamba na watoto wawe wanalipa. Lakini wewe unang’ang’ania mpaka riba kwa mtoto. Vipi mimi mzazi, umeniacha maskini, mtoto wangu umemharibu; hukumpa elimu, umemharibu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ya Tanzania ukweli ni kwamba mimi natumia gharama kubwa kumwandaa mtumwa atakayeenda kuwa mtumwa wa mtu mwingine. Inawezekana kweli? Kwa nini unakataa mawazo yangu ya shughuli zangu tuka-share pamoja ili mtoto atakaposhindikana, akirudi kwangu mimi siyo mzigo, anajua hata vyakula vyangu na maisha yangu ya nyumbani; tungegombanaje na nani angekwambia kwamba kuna tatizo la ajira. Ilikuwa hakuna tatizo la ajira maana yake mtoto angeona kwamba kazi ya biashara, kazi ya kulima au kufuga inanilipa Zaidi, sitaki hata hiyo ajira, ata-bargain na mshahara. Sasa hivi hawana haja ya ku-bargain mshahara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimnaulishe mwanangu, kila kitu, halafu mimi unipe karatasi nije kwako. Kwa kweli ni kitu ambacho kina matatizo makubwa sana. Uzuri kwa kuwa na Wabunge wengine, miaka mitano mimi nimepiga kelele lakini uzuri na Wabunge wameanza kuliona na najua mpaka mwakani wakati hela imepungua ndiyo tutalijua vizuri zaidi. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala hili la uwekezaji. Mtazamo uliopo tunatazama tu upande mmoja. Juzi kwenye Kamati yangu ya Biashara na Viwanda nilijaribu kuwadokeza kidogo wenzangu kwamba jamani hivi uwekezaji ninyi mnaoujua ni wa viwanda peke yake. Dunia imebadilika, leo ndege yetu inakwenda India asilimia 90 ya wasafiri ni wagonjwa, kuna ubaya gani wenzetu wa uwekezaji wakaongea na watu wa hospitali za India waone kitu gani kinachowakwaza kuja kuweka hospitali zao hapa. Tuwaruhusu, tuwape EPZ ileile ambayo tunaitoa kwenye viwanda, tusiwawekee tena yale masheria yetu ya hapa wenyewe wafanye bila kufuata sheria za kwetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, itatusaidia na wagonjwa wa nchi zingine wanaokwenda India watakuja kwetu, lakini watumie sheria za kwao, tusiwawekee tena yale makorokoro yetu, mara migration, mara hukusoma, mara nini, hapana, itawezekana kabisa na biashara itawezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo mengi sana, kuna maeneo ya vyuo vikuu vya nje, tuwape maeneo au tuwajengee. Kama tunaweza kujenga vitu vyote vikubwa, tuwaulize wanataka nini, ili tuwajengee waweke standards zao, wanafunzi watoe wao nje, wa kwetu nao wakitaka wa- apply kama wanaenda nje, lakini wakiwa hapa hapa nyumbani. Nasi tukitaka kutibiwa kama ni hospitali, badala ya kwenda India, si tuta-apply tunaenda kutibiwa mle mle tu; na watu wa nje watakuja. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri wenzetu wa Uwekezaji mawazo yabadilike sana. Leo kuna biashara kubwa sana ya imani. Tuna viongozi wa dini ambao wana mvuto mkubwa sana. Kwa nini tusitenge maeneo tukawauliza, je, tukikujengea eneo la kuabudia, unaweza kuja hapa kwetu mara moja kwa mwezi? Ili kusudi wale watu wanaokufuata wewe kule wa nchi za jirani wanaweza kuja kukuona hapa mara moja kwa mwezi. Sisi tutapata biashara, hoteli zetu zitapata wateja na maeneo yote ya shughuli mbalimbali yatafaidika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilienda mbali sana mpaka nikasema, hata group lile la Babu wa Loliondo, kuna ubaya gani na wao wakawekewa eneo lao na yenyewe ikawa EPZ. Mtu akitaka kwenda kutazamiwa hali yake, aende kihalali. Si tumeruhusu? (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachohitaji sasa hivi ni kutembelewa. Hotuba ya Mheshimiwa Rais imesema inataka watu milioni tano, je, watu milioni tano tutawapata kutokea wapi ili waje watutembelee? Ni lazima wenzetu wa Uwekezaji wapanue wigo, waache kufikiria upande mmoja. Wakijitahidi hilo, litatusaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kumalizia ni suala hili la permit. Kuna shughuli ambazo huwa hazisomewi, ni za ukoo au mtu anaijua bila karatasi. Mheshimiwa Waziri wa Madini anafahamu, kulikuwa na suala la wakata Tanzanite. Wale watu wanaokata Tanzanite hawana elimu wala cheti, lakini wanafahamu kukata Tanzanite. Swali lililokuwa linatatiza, hawawezi kuja hapa kwa sababu permit yao haiwezi kupatikana maana hawana elimu. Sasa labda niulize wasomi kwa kuwa wamo humu; definition ya elimu ni nini, ni karatasi au ni kuelewa? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana kama mtu umemkuta anakata Tanzanite vizuri na anauza; na yako inakwenda kukatiwa hapo, unashindwa kumwambia aje huku kwa sababu ukimwuliza cheti, anasema sisi hii kazi haisomewi na vyuo vyake havipo. Sasa kweli tukose biashara kwa ajili ya neno “cheti” au “document” na mtu anafahamu? Haiwezekani! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango ni mzuri, naomba sana wenzetu wa Uwekezaji na Mheshimiwa Waziri wa Fedha wafikirie.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)