Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muheza
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HAMIS M. MWINJUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Umenipiga ambush kusema ukweli. Cha kwanza kuongea kwenye Bunge lako tukufu ni kumshukuru Mwenyezi Mungu, pili, kukishukuru Chama changu cha Mapinduzi na kipekee kabisa Rais wangu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambaye aliongoza vikao vyote vya uteuzi vilivyohakikisha jina langu linarudi. Tatu, niwashukuru wananchi wenzangu wa Muheza kwa kunipa imani kubwa. Nne, niishukuru familia yangu na nichukue fursa hii sasa kuchangia Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2021/2022 mpaka 2025/2026. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la mchango ni kuisaidia Serikali kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato. Niseme kwamba nimeusoma Mpango na naona kwamba kuna maeneo mengi ambayo tunaweza kama Wabunge tukachangia na tukaisaidia Serikali kufanya hilo ili iweze kutekeleza miradi ya maendeleo kwa ufanisi kadri inavyokusudia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kwa sababu ya muda sitaweza kuongea mambo mengi, lakini niseme kwamba eneo ambalo nataka kulichangia ni hasa la walionitumia, wananchi wa Muheza. Pamoja na kwamba nchi hii inaonekana kwamba asilimia 65 ya wananchi wa nchi hii wanapata riziki zao kwa kutumia kilimo, wananchi wa Muheza ni takriban asilimia 90 ama zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Muheza kama ambavyo najua wananchi wengine wengi wa nchi hii wanataka kuchangia mapato ya Serikali zaidi ya wanavyofanya sasa hivi. Mazingira yanawapa wakati mgumu. Ningependa kuchukua nafasi hii kuiomba Serikali ijue kwamba haiwezi kukwepa moja kwa moja kwenye mazingira kuyafanya rafiki ili kuwezesha kuingiza fedha zaidi baadaye. Ndivyo biashara zinavyofanywa, unawekeza ili upate zaidi huko mbeleni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni nilihudhuria Mkutano wa wadau wa mkonge na Waziri Mkuu na moja ya vitu ambavyo vilinishangaza lakini kwa wema, ni suala kwamba wakulima wadogo wanazalisha zaidi ya wakulima wakubwa, kwamba katika top four ya wazalishaji wa zao la mkonge nchini wakulima wadogo ni namba moja, wakifuatiwa na Mboni wakifuatiwa na na METL na wengineo wanafuata. Hii inaonesha kwamba mahali ambapo tunafanya kosa labda ni kutotoa macho kwenye kuhakikisha wakulima wadogo wanawezeshwa na kupewa nafasi ya kuzalisha zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hotuba ya Rais Magufuli ya kufungua Bunge la 12 tarehe 13 Novemba, 2020, katika ukurasa wa 27 na 28 Rais anasema kwamba moja ya vitu ambavyo vinatu-cost ni kwamba, naomba ninukuu: “Takwimu zinaonesha kuwa kila mwaka nchi yetu inapoteza wastani wa kati ya asilimia 30 – 40 ya mavuno yake kwa sababu mbalimbali ikiwemo kukosekana kwa miundombinu ya kuhifadhi” mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais pia kwenye ukurasa wa 27 ameweka wazi kwamba lengo la Serikali ni kukifanya kilimo kuwa cha kibiashara, sasa kuna miradi mbalimbali ambayo ilisitishwa, mathalani Mpango wa Marketing Infrastructure Value Addition and Rural Finance - MIVARF kwamba baada ya awamu ya kwanza Serikali haikusaini kuendelea na awamu ya pili. Sijui sababu zake, lakini nafikiri moja ya vitu ambavyo Serikali ingeweza kufanya ni ku- take over kwenye mpango huu, badala ya kuwaacha wale wa-Finland watuendeshee, Serikali ingeendeleza kwa sababu ni Mpango ambao ulikuwa unaonekana una manufaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, post-harvest centres ambazo zilikuwa zinatumika kama masoko zilikuwa zinawekwa mahali kuhakikisha soko la wafanyabiashara wa mbogamboga, kwa mfano maeneo kama Lushoto, linakuwa la uhakika. Miundombinu ya kufikisha kwenye soko lile wale watu wa Finland walikuwa wanahakikisha wanatengeneza. Kwa hivyo, tunaweza kuua ndege wawili kwa jiwe moja. Kwanza tukahakikisha miundombinu ya wafanyabiashara, wakulima kufikisha kwenye soko inapatikana na pia soko la wazi la wafanyabiashara wakulima hawa wa mboga mboga liko wazi. Kwa mfano kulikuwa na barabara ya kutoka Mkatoni kwenda Kwai kule Lushoto au Chanjamjawiri mpaka Pujini kule Pemba hizi zote zilitengenezwa kwa ajili ya Mpango huu. Kwa hiyo tungeweza kuhakikisha kwamba wana soko na miundombinu inatengenezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya vitu ambavyo vinaniumiza moyo ni kwamba hii asilimia 30 mpaka 40 ambayo Mheshimiwa Rais alisema inapotea ni ya wakulima wadogo. Wakulima wa ndizi kule kwetu Amani kwa mfano, ukienda wakati wamvua unaona jinsi ambavyo ndizi zimeoza barabarani kwa sababu zinashindwa kufikishwa sokoni. Kwa hiyo, naomba Serikali iwekeze kwenye kuhakikisha kwamba tunawafaidisha, tunawanufaisha wakulima wadogo na wanaweza kupata masoko…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.
MHE. HAMIS M. MWINJUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)