Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Flatei Gregory Massay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi hii. Nianze kutoa mchango wangu katika Mpango huu wa mwaka mmoja na miaka mitano na nataka kwenda kwenye kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi ukiangalia kilimo cha umwagiliaji katika nchi yetu tunalima hekari 461,376. Kilimo cha uhakika duniani kote lazima utumie umwagiliaji na ukimwagilia maana yake una maji ya uhakika na unaweza kunyeshea na mazao yakaiva kwa uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia hali halisi kwa sasa Tanzania mvua zinanyesha na hapa Dodoma unaona mchana kutwa mvua imekuwa ikinyesha, lakini hakuna namna yoyote tunayofanya, kama nchi kuweza kuzuia maji haya. Nashauri katika Mpango huu, Serikali ije na mpango mzuri iweke hela kwenye kilimo, wananchi waweze kutengenezewa mabwawa ili haya maji ambayo yanatoka katika mbingu yanapokuja ardhini yaweze kutiririka kwenye mabwawa, yahifadhiwe na badaye wakulima wetu waweze kunyeshea mashamba na Tanzania tutaokoka kwa kuwa na mashamba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mvua hizihizi ndiyo zinazoenda kuharibu barabara. Tumekuwa tukilalamika hapa tangu hotuba ya Rais kwamba TARURA iongezewe fedha, lakini tungekuwa na namna ya kuzuia haya maji yaende kwenye mabwawa badala ya barabarani, ni wazi ni rahisi sana kuweza kutumia maji haya ambayo yapo katika nchi yetu kufanya kilimo cha umwagilia. Maji haya yanaharibu barabara. Yanapoharibu barabara maana yake ni kwamba Serikali hiihii pia tunaanza kuilaumu itafute pesa za kutengeneza barabara, kumbe tungeweza kuwa na mpango mzuri wa kuhifadhi maji yanayotiririka, ili maji haya yakaweza kunyeshea mashamba na wakati huohuo tutakuwa tumezuia maji haya yasiende kwenye barabara kuleta uharibifu. Kwa hiyo, nadhani Waziri Mpango na Serikali yake waone namna gani kusaidia kuweka fedha ya kutosha katika uwekezaji kwenye kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia bajeti zote zilizopita hazikuonesha wazi kabisa kwamba tumewekeza kwenye kilimo. Kwa mfano leo, AMCOS na mashirika madogo madogo ya wakulima yamekuwa yanakopeshwa ili kulima lakini wakati huo wanawekewa insurance ya pembejeo hizo, lakini wakati huo wanaenda kudaiwa wakati ambapo Serikali huku hatujawawezesha bado kwa kuwawekea namna nzuri ya kupata mavuno kwenye mashamba yao. Ni lazima tuhakikishe kwamba tunapowakopesha wakulima, wakati huo tumeshawawekea mazingira mazuri ya wao kuzalisha, vinginevyo tutakuwa tuna madeni na tunawadai hawa wenye AMCOS lakini hawataweza kulipa. Nadhani masuala haya yanapaswa kuangaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi, pembejeo. Leo hii Tanzania kama nchi, pembejeo zetu zote tunatoa nje. Kwa mfano, mbegu zetu nyingine zinatoka Kenya, Uganda lakini ombi langu kwa nini tusianzishe mashamba ya mbegu katika nchi yetu ili mbegu zisitoke nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema wakati nachangia kwenye Hotuba ya Rais, mbegu zinatoka nje kwa gharama kubwa, ikija hapa kwetu tunauziwa shilingi 13,000 mpaka shilingi 15,000 kwa mfuko. Ni wazi kabisa kwamba mwananchi wa kijijini kule kwa kupanda eka nyingi anahitaji kuwa na investiment ya kutosha. Tukiwa na mashamba ya mbegu hapa nchini ni wazi kwamba mbegu zitakuwa za bei nafuu na zitaongeza ubora katika uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu ya barabara katika nchi zote ndiyo inayosaidia uchumi wa nchi kupanda. Katika Mpango huu, naomba muangalie barabara kubwa zinazoleta uchumi katika nchi hii. Kwa mfano, kuna barabara ambayo kila siku tumekuwa tukiisema hapa, hii ya Karatu - Mbulu - Dongobesh - Haydom - Simiyu - Bariadi.

Kwa hiyo, barabara kama hizi zikifunguliwa na zikaonekana kwenye Mpango, kwa sababu, ukiangalia kwenye Ilani ya Chama ipo, kwenye Hotuba ya Rais ipo, lakini namna ya kuweka mpango sasa hii barabara ianze kujengwa ndiyo inakuwa kigugumizi, kwa hiyo, kupanga ni kuchagua. Ukipanua hili eneo la Tanzania kama nchi ukawekeza hela kujenga zile barabara za upande ule, kwa hiyo, unapozunguka nchi hii mazao yanatoka kijijini kwenda viwandani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii nikuambie ukweli viwanda vyetu vipo, lakini ukimuuliza Waziri wa Viwanda atakuambia hakuna malighafi, lakini nenda kijijini kwa mfano Haydom utakuta alizeti ipo. Itafikaje kiwandani, haiwezekani kwa sababu barabara za kule ni mbovu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika ni kidogo sana, naunga mkono hoja. (Makofi)