Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Priscus Jacob Tarimo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Niendelee kuwashukuru wapiga kura wangu wa Moshi Mjini kwa namna wanavyoendelea kuniunga mkono na kunitia moyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajaribu kwenda kwa harakaharaka kutokana na muda, lakini nianzie kwenye kilimo. Kwenye kilimo mpango ulioletwa ni mzuri lakini unahitaji kujaziwa mambo mengi ambayo mengi wameyataja Wabunge wenzangu lakini na mimi niongezee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukisema tunaweka nguvu kwenye kilimo na tunaendelea kutegemea kilimo cha maji ya mvua, tutakuwa tunapoteza muda. Wakati tatizo la mabadiliko ya tabianchi linaendelea kuwa kubwa, tukitegemea kilimo bila kuwa na mpango madhubuti wa umwagiliaji tutakuwa tunapoteza muda. Bwawa la Nyumba ya Mungu lililoko kwenye Mkoa wa Kilimanjaro lilijengwa miaka ya 67, lina faida kubwa pamoja na kuzalisha umeme, kuna samaki lakini mabwawa kama haya yanaweza kutengenezwa ili kusaidia umwagiliaji ili kilimo chetu kiwe chenye tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sijaona mpango wa kilimo cha large scale. Block farming kwa ajili ya kuwasaidia wakulima wadogo ni kizuri lakini kama tunataka kilimo kilete tija ni vizuri tuwe na sera pia ambazo zitasaidia wakulima wakubwa waweze kuwekeza katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna eneo ambalo nadhani Wizara inabidi ilifanyie kazi zaidi. Nadhani suala hili Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo alishaliongelea siku za nyuma kwamba ni lazima Sera ya Viwanda iwe na mwingiliano wa karibu na Sera ya Kilimo. Kwa mfano, sasa hivi tuna matatizo ya mafuta ya kula lakini tunaona tumefeli kwenye alizeti kwa maana ya kwamba demand yetu imekuwa kubwa kuliko supply. Hata hivyo, Kigoma kuna mawese huoni kinachofanyika ambacho kitaleta tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mwaka tunaagiza sukari lakini mwenzetu wa Kilombero amesema wanatupa sijui tani za miwa 40 kila msimu. Juzi tu Mheshimiwa Waziri wa Kilimo alikuwa na kikao na wakulima wa ngano kwa maana ya kwamba tunaagiza ngano nyingi. Kwenye haya mazao ambayo demand yake ndani tayari ni kubwa kwa nini kusiwe na mpango wa muda mfupi na wa muda mrefu mpaka miaka 20 kuhakikisha tunakidhi soko la ndani la mazao haya ikiwa ni pamoja na kuweka viwanda vyake? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo miradi ambayo inaenda kukamilika. Nimejaribu kuangalia sijaona mpango ulionyooka wa ku-support SGR kwa mfano. Ningefurahi sana kama ningeona tayari kuna juhudi za kuongea na nchi kama Congo kuhakikisha kwamba watatumia SGR kwa ajili ya kusafirishia mizigo yao itakapokamilika. Hii ikiwa ni pamoja na kuangalia namna ya kuunganisha Bandari ya Dar-Es-Salaam kwenye viwango vyake, kuna mtu amesema hapa na kuitangaza ili kwenye hii miradi ambayo inaenda kuiva karibuni tuone ni namna gani itaingiza fedha ili kusaidia mipango hiyo, sijaliona. Mimi nilitegemea sasa hivi kuwe kuna economic diplomacy ya kuangalia nchi kama za Rwanda, Burundi, Congo, tunatafuta njia gani watapitisha mizigo yao yote hapa kwetu, hiyo ni pamoja na ATCL. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye utalii nako bado kuna matatizo. Kwanza niseme tu wale wafanyabiashara wa utalii na Mkoa wa Kilimanjaro ni mmoja wa maeneo hayo, wana kilio kutokana na janga hili la corona. Biashara zao zimekwenda chini sana, wanaomba Serikali iwaangalie japo hata kwenye tozo ili kuwapunguzia makali. Hata hivyo, kuwepo kwa ATCL nilitegemea kuwepo kabisa na mkakati wa kuunganisha na baadhi ya mashirika ya kimataifa, ili i- promote utalii kwa ndani ili sasa tuanze kupata fedha kutika kwenye mashirika haya ya kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mikopo hasa kuwainua wafanyabiashara wadogo, nilishasema kwenye kuchangia hoja mwanzo kwamba tuangalie uwezekano wa kumkopesha mtu mmoja-mmoja. Pia hapa kwenye umri tuliojiwekea hasa kwa vijana, sina shida sana na akina mama, tumesema vijana ni miaka 18 mpaka 35, lakini vijana wa Kitanzania wenye miaka mpaka 45 wana nguvu ya kuweza kufanya kazi na kuzalisha. Tujaribu kuangalia sheria zetu kwa nini vijana sasa miaka 36 mpaka 45 hawakopesheki kwenye fedha hizi ili kuchangia kwenye pato la Taifa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la TARURA, huwezi kusema kilimo bila kuwa na miundobinu iliyo sawa. TARURA wamepewa jukumu, najikita kwenye kuishauri Serikali itafute namna bora ya kuipatia TARURA chanzo cha mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)