Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. MARTHA N. GWAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi hii. Kwa vile ni mara yangu ya kwanza naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia mpaka kufikia siku ya leo. Pia naomba niishukuru familia yangu kwa support waliyonipa kipindi chote. Naomba nikishukuru Chama changu Cha Mapinduzi kwa kurudisha jina langu na kuniwezesha kuwa hapa lakini mwisho, naomba niwashukuru wapiga kura wangu akinamama wa Mkoa wa Singida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba na mimi kuchukua nafasi hii kuchangia Mpango huu wa Miaka Mitano tunayoiendea. Kwanza naomba nimpongeze Waziri kwa hotuba nzuri lakini maelezo mazuri yanayohusiana na Mpango huu ambao naamini yamejikita kwenye kusaidia wananchi na hasa wale wenye kipato kidogo. Mchango wangu kwa siku ya leo nitauelekeza kwenye kilimo ambapo najua wachangiaji wengi wameshachangia, lakini kwa sababu ni suala ambalo linagusa mtu wa chini, kwa hiyo tunaliongelea mara kwa mara na tunaamini kwamba yule mtu wa chini ndiyo mlengwa hasa ambaye anapata shida na ndiyo mwenye kipato cha chini. Kuna usemi wa three knows wanasema; no pharmacy, no food, no future.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwa mimi ninayetoka Mkoa wa Singida naomba nijikite kwenye zao kubwa la alizeti. Hili zao, wewe mwenyewe ni shahidi kipindi cha nyuma kama miezi mitatu iliyopita tumepata uhaba wa mafuta. Pia tuna mashamba ya kulima, tuna watu wenye nguvu za kulima ili hii alizeti itosheleze sisi kwa mwaka mzima na hata kupata ziada ambayo itasababisha sisi tukasafirisha kwenda kuuza. Kwa hiyo naomba pamoja na Mpango mzuri wa Wizara ya Kilimo, hili zao la alizeti tulipandishe hadhi liwe kama zao la korosho na mazao mengine ya kitaifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivyo? Tukipandisha hadhi hili zao tutakuwa na guaranteed market lakini pia tutakuwa na guaranteed price kama yalivyo mazao mengine kama korosho, lakini pia litatusaidia sisi Watanzania na watu walioko nje ya Tanzania. Kwa kulipandisha hadhi tuhakikishe kwamba mbegu bora zinapatikana ambazo tukikamua mafuta ya alizeti tutapata mengi ukilinganisha na sasa hivi mbegu zilizopo mafuta yanayotoka ni 40% tu. Tukipata mbegu bora tukapata bei bora ya mbegu ambayo mkulima wa chini anaweza ku-afford kununua, itasaidia hili zao listawi lakini pia tuuze kwa Mkoa wetu wa Singida lakini hata na mikoa mingine ya jirani waweze kulilima na kupata faida kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni utafiti ambao utasaidia, siyo tu kwa Mkoa wa Singida najua Mkoa wa Singida zao linastawi vizuri, lakini utafiti ukifanyika ina maana hata na mikoa mingine itaweza kulima hili zao la alizeti. Mwisho wa siku hatutapata hii aibu ya kuagiza mafuta nje ambapo tunatumia pesa nyingi sana kuagiza na wakati hizo resources tungeziweka kwa wakulima wetu, tungewa- empower wananchi wetu, wakalilima na wakapata masoko, huu uhaba wa mafuta hautakuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni zao la vitunguu ambalo linapatikana Mkoa wa Singida. Nalo hilo tulipandishe hadhi, tukipandisha hadhi litatusaidia tutalima Singida na mikoa mingine watalima pia. Kwa hiyo kwa upande wa kilimo nilitaka nijikite kwa hilo. Tuna SIDO wanaweza wakatusaidia kutoa elimu kwa wakulima wetu kwa viwanda vyetu vidogo vidogo ambavyo vikitaka kusindika mafuta na vitataka kufanya shughuli nzima za uzalishaji Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine naomba niongelee suala la…
SPIKA: Samahani Martha lipandishwe hadhi kwa kufanyaje?
MHE. MARTHA N. GWAU: Kuwa zao la Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine naomba niongelee suala la usafiri. Tunajua uwekezaji ndiyo kila kitu kwa sasa hivi na ndiyo unasaidia pato la Taifa na ajira kwa vijana wetu. Usafiri wa anga ni kitu muhimu sana ambacho mwekezaji anakiangalia, awe wa ndani awe wa nje. Kutoka Dar es Salaam mpaka Singida ni masaa 12 kwa gari, sasa tukifungua viwanja vya ndege, tukapata ndege, mwekezaji atatumia saa 1.30 kufika Singida kuona fursa zilizopo ambazo ataweza kuwekeza. Sio tu mwekezaji wa nje lakini hata mwekezaji wa ndani, mtu wa Mwanza atakuja Singida mara moja, ataona fursa, ataondoka, nami wa Singida nitaenda Mtwara, nitaona fursa naondoka, kwasababu ya usafiri ambao ni ndege itakuwa ni rahisi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipongeze kwa kweli Shirika la Ndege, mikoa mingi imepata ziara hizo na viwanja. Tunaiomba Serikali kwa mikoa ambayo ya kimkakati kama Singida itusaidie uwanja wa ndege ili tuweze kupata fursa watu wote waone mazao yetu, tuna uchimbaji wa madini, tuna zao la alizeti, tuna mambo mengi ambayo yanaendelea Singida, tukipata kiwanja cha ndege na ndege itatusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho la kumalizia, ni suala la usafiri wa treni. Tuna treni yetu ya Singida ambayo ilikuwa inasaidia wakulima wetu kusafirisha mazao kwa bei rahisi kutoka sehemu moja mpaka nyingine. Kwa hiyo, hiyo ilikuwa inampa fursa mwananchi wa Singida kujua soko liko wapi. Kama liko Mwanza, atapeleka mazao yake akauze kule, kwa sababu ulikuwa ni usafiri affordable lakini pia na bei kidogo ni nzuri. Kwa hiyo naomba Serikali iangalie hili la kufufua treni ya Singida ili itusaidie kwenye suala zima la kusafirisha mazao yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, nataka niwakaribishe wote Mkoa wa Singida, tuna uzinduzi wa kitabu cha uwekezaji kwa mkoa, tarehe 23 Januari mje mjionee fursa mbalimbali ambazo Waheshimiwa Wabunge mnaweza kupenda kuwekeza na niwakaribishe sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nikushukuru sana kwa nafasi hii. (Makofi)
SPIKA: Martha umesema tarehe 23 Januari.
MHE. MARTHA N. GWAU: Samahani ni tarehe 23 Februari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)