Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Nashon William Bidyanguze

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kwanza kumpongeza Mheshimiwa Mpango kwa taarifa nzuri aliyoleta mbele yetu na naomba nichangie eneo la kilimo na uvuvi kama muda utanitosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nichukue nafasi hii niwashukuru Wanajimbo la Kigoma Kusini kwa kunichagua, lakini pia nikishukuru Chama Cha Mapinduzi kuweza kurudisha jina langu ili niweze kupeperusha bendera ya kutetea Jimbo la Kigoma Kusini ambapo nilishinda kwa kishindo na pia Mheshimiwa Rais alipata kura nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niwashukuru familia, hawa watu kama wasingeweza kunipa support nisingeweza kufika hapa nilipo; mke wangu pamoja na watoto lakini zaidi sana ndugu yangu mmoja ambaye anaitwa Gervas; Mkurugenzi wa World Worth. Huyu mtu alilfika kwenye mkutano wa kampeni wakati mimi nazindua tarehe 11 Oktoba, 20. Aliwaambia wananchi, mkimchagua huyu bwana Bidyanguze mimi nitamchangia milioni 50 kuongezea kwenye Mfuko wa Jimbo wa Serikali. Jambo la ajabu sana, kwa hiyo nataka nikwambie kuanzia sasa tayari katika Mfuko wa Jimbo ule ambao nilifadhiliwa na mwanaume yule tayari nilishapeleka milioni 12 mifuko ya cement 600 ya thamani ya milioni 12. Huyo mtu lazima nimpongeze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nichangie Mpango huu kwenye eneo la kilimo. Kilimo ni kweli ndiyo uti wa mgongo, lakini kwa bahati mbaya sana naomba nishauri Serikali, bado haijaweka miundombinu mizuri yaani ile ambayo inatamanisha wananchi waweze kupenda kilimo. Serikali bado inasaidia tu wale ambao wameitikia kilimo, mimi najiuliza wako vijana wengi wanaingia shule za sekondari wanamaliza vyuo vikuu, wote hawa plan yao ni kuajiriwa. Naamini Serikali haina uwezo wa kuajiri wote hao, sasa tufanyeje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri Serikali ije na mpango wa kushawishi wananchi, hawa vijana ambao ni kundi kubwa, waweze kupenda kilimo. Kilimo wanakikimbia, si tunao majimboni kule, wapo ambao wamesoma wamemaliza vyuo vikuu lakini hawana kazi, lakini ukiwaambia twende tujiajiri kwenye kilimo hawana habari na hicho kitu. Sasa nadhani katika eneo hili la kilimo, yuko mchangiaji mmoja amezungumza vizuri na sikumbuki vizuri, hivi tathmini ya wanafunzi ya wanaokwenda kujifunza kilimo kusoma masomo ya kilimo hivi ni wangapi? Naona kama ni wachache sana, kwa sababu gani? Kilimo wanakikimbia na wale ambao wanalima wanakwenda kuchoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nadhani Wizara ya Kilimo ije na mpango ambao utatengeneza ushawishi ili watu waweze kulima. Kilimo kimetafsiriwa kwamba ni kwenda na jembe la mkono kwenda kulima, mtu aliyesoma hawezi kwenda kulima kwa kilimo hicho. Kwa hiyo tunatakiwa Serikali ije na mpango wa kusaidia kutoa mashamba maana mashamba yenyewe kuyapata ni kazi. Mashamba yapatikane kwa njia nyepesi kama vile ambavyo Serikali inahamasisha uwekezaji tuhamasishe uwekezaji ndani ya kilimo kwa watu wetu hawa vijana, tukishafanya hivyo, watu watakipenda kilimo, lakini mwisho wa siku lazima kilimo kile Serikali iweke utaratibu wa kupata masoko kwa ajili ya mazao hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mkulima kwa kiasi fulani, niliwahi kulima maeneo ya Tanga kule, lakini tuliwahi kupata mahindi mengi wakati fulani nadhani ilikuwa elfu mbili kumi na ngapi sijui, lakini Serikali kwa sababu ya kuhitaji kutunza chakula ndani ya nchi ilikataza watu kusafirisha mazao nje ya nchi. Hata hivyo, yenyewe Serikali haikuwa tayari kuyanunua. Sasa wewe fikiria, mtu amekwishalima na amekwishavuna, asafirishe akauze, apate fedha anazuiliwa na Serikali ni jambo jema, lakini basi yanunue hayo mazao. Kwa hiyo nafikiri kwenye eneo la kilimo tukilifanyia kazi ni sehemu nzuri sana ya kuajiri watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ufugaji pia; ufugaji ni kama kilimo. Sisi Kigoma tunalo Ziwa Tanganyika lina samaki wengi sana lakini elimu haipo ya uvuaji wa samaki, ni eneo moja ambalo kama Serikali ingejikita kufundisha na kutoa nyenzo kwa ajili ya watu waweze kuvua, nadhani vijana wetu hawa ambao wako katika shule na wanaingia kwenye shule na vyuo vikuu wangeweza kujikita baada ya kutoka kule, kuja kuingia kwenye habari ya uvuaji wa samaki. Habari hii ni ajira kubwa sana na ingeleta tija kubwa sana na fedha nyingi kwenye kuongeza kwenye pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nafikiri hili nalo lazima tuliangalie sana, kuliko kufikiria tu kwamba lazima mtu asome awe nani. Nasema hivi, watu wengi sasa hivi wanafikiria kila mtu awe Mbunge, wanafikiri kwamba kwenye Ubunge kidogo kuna nafuu, lakini Jimbo la Kigoma Kusini, Jimbo la Mwibara na mengine, hivi wote kama watafikiria kuja huku ni kwa nini? Ni kwa sababu inaonekana kidogo Mbunge akirudi kutoka Bungeni, anakuja amevaa vizuri, anaonekana anafaa. Kwa hiyo, nadhani Serikali iwekeze katika kilimo na uvuvi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. NASHON W. BIDYANGUZE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kuchangia hayo. Ahsante (Makofi)