Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mungu kwa fursa ambayo nimeipata kuweza kuchangia katika Bunge lako lakini pia kwa sababu muda ni mfupi niwashukuru sana wachangiaji ambao wamechangia kwenye Wizara yetu ni takriban Wabunge tisa ambao wamechangia. Hoja kubwa ilikuwa ni suala la kupima ardhi yote ya Tanzania kama ambavyo waliomba, lakini pia wakasema wigo wa ukusanyaji wa mapato nao bado hautoshelezi. La tatu likawa ni katika kupanga miji kama ambavyo inaonekana tulivyoanza katika ile Magometi Quarter, Wilaya ya Kinondoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niungane kweli na Wabunge jinsi walivyosema mpaka sasa ni takriban asilimia 25 tu ya ardhi yote nchini ambayo imepimwa. Kwa hiyo asilimia 75 yote inaonekana haijapimwa na mpaka sasa tulichoweza kupima ni viwanja 2,349,626, mashamba 28,312 na kutoa hati 1,559,509, ukiangalia kwa watu wachache kama hao bado ni tatizo kweli. Mkakati tulionao kama Wizara tumeona tutatumia approach moja ambayo inasema fit for purpose ambayo imetumika katika maeneo mengine na imeweza kuleta tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hilo tunachofanya sasa ni kuwajengea uwezo wataalam wetu tulionao. Tunao wataalam wachache, tunatakiwa kuwa na wataalam 2,500 kwa nchi nzima, lakini tulionao mpaka sasa ni 1,400. Kwa hiyo 1,400 hawawezi kukidhi haja katika suala zima la upangaji, upimaji na kumilikisha, lakini tunasema tutajengea uwezo wapima wakati ambao tutakuwa tunawaita para surveyors, watajengewa uwezo ili waweze kusaidia katika hili jambo la upimaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tutatumia vyuo vyetu tulivyonavyo; Chuo cha Morogoro pamoja na Chuo cha Tabora katika suala zima la upimaji. Tumejaribu katika kipindi kilichopita kutumia makampuni kwenye zoezi la upimaji shirikishi, lakini kati ya makampuni 134 tuliyoya–engage ni makampuni 34 tu ambayo yamefanya vizuri. Makampuni mengine yote yameshindwa na mikataba tumewanyang’anya. Sasa tunachofanya ni kuelekeza kwa sababu tayari mikoa yote ina ofisi na ina wataalam wa kutosha waweze kuunga nguvu katika mikoa yao jinsi walivyo kupitia ofisi za halmashauri zote, tumeshatambua wale watumishi tulionao kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kama ni suala la kupima, kupanga na kumilikisha tutalifanya kama operesheni maalum kwamba wataungana ngazi ya mkoa kwa sababu mikoa yote ina vifaa na kuna baadhi ya wilaya zina vifaa. Kwa hiyo tunaunda timu ndani ya mkoa mmoja, wanaanza wilaya moja baada ya nyingine. Kwa hiyo katika hili tumeomba pia ushirikiano wa ma-RAS pale kuweza kuongeza nguvu katika suala zima la kuunda timu kwenda katika wilaya moja baada ya nyingine. Kwa kutumia approach hiyo itakwenda kusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile katika suala zima hilo la kupanga makazi kama tulivyofanya Magomeni Quarter ambayo aliomba Mheshimiwa Mtemvu wa Dar es Salaam linawezekana kwa sababu pia wenzetu wa Morocco, Ethiopia wamefanya hivyo. Ni ule utayari tu wa halmashauri zenyewe kuweza kuwashawishi wananchi katika yale maeneo yakaondolewa yale makazi ambayo si mazuri ambayo ni ya kawaida sana wakajengewa makazi mengine kama ilivyo Magomeni Quarters, halafu wale wanakuwa wa kwanza kupewa kipaumbele kuweza kumiliki maeneo yale ambayo yatakuwa yamejengwa na sehemu nyingine kama ni Halmashauri zinaweza zikatumia kwa kazi nyingine. Kwa hiyo hii pia itatusaidia kuondoa adha ya majengo au nyumba zingine ambazo ziko mjini lakini hazifanani na miji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala zima la ukusanyaji wa maduhuli kama hamjapima, hamuwezi kukusanya, lakini bado tuna madeni mengi ambayo tunadai na tumeweza kusambaza notice na sasa tutasimamia sheria kwa ukaribu zaidi. Ukishapewa notice ndani ya siku 14 unatakiwa upelekwe kwenye Baraza, ukishindwa basi tunanadi vitu vyako na kama umepewa notice miezi sita kinachofuata ni kunyang’anywa ule umiliki bila kupewa taarifa, kwa sababu tayari utakuwa ulishapewa notice. Kwa hiyo hilo litatusaidia pia katika watu. Pia wale ambao wenye viwanja ambavyo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa, kengele imeshagonga ahsante sana.

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika moja.

Waliopimiwa viwanja lakini hawataki kumiliki mwaka jana tulibadili sheria hapa, Kifungu Na. 33 (1) kilibadilishwa kwa hiyo hata kama hauna hati, sisi tunaanza kutoza kodi kwa sababu tulishakupa grace period ya siku 90 uweze kuomba kumilikishwa. Sasa kama hujamilikishwa maana yake tutaanza kutoza kodi katika viwanja vyote na tumeshaanza, uwe una hati au huna hati utakwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo rai yangu ni…

MWENYEKITI: Mheshimiwa, ahsante sana. Shukrani.

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: … wananchi kushirikiana na Halmashauri zote. Na tunatambua namna ambavyo TAMISEMI wameanza na sisi vile vile tunatumia watendaji wa mitaa kuweza kuwatambua wadeni wetu kuweza kukusanya kodi na kuweza kuangalia namna bora ya kupata takwimu sahihi zitakazotuwezesha pia kuweza kupata mapato ya nchi. Ahsante. (Makofi)