Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nyamagana
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitumie nafasi hii kukushukuru wewe, kulishukuru Bunge lako, na kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa namna ambavyo ameendelea kutupa nafasi ya kuwepo hapa ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze kwa uamuzi mzuri wa kuamua kuleta maazimio haya mawili ndani ya Bunge kwa sababu kubwa mbili. Moja ni kumuenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ambaye alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kumpongeza mama yetu Samia Suluhu Hassan ambaye leo ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna maneno mazuri sana ya kusema leo, lakini ukweli ni kwamba inawezekana kulingana na vitabu vitakatifu yako mambo yameandikwa kwenye vitabu hivi vitakatifu, na sisi kama wanadamu tunaoishi tusioijua leo wala kesho na mipango yote kama ambavyo Mheshimiwa Makamu wa Rais ambaye leo jina lake limeletwa mbele yetu na ametuambia mambo yote mazuri yanatoka kwa Mungu, hatuna shaka ya kwamba kipindi alichohudumu Dkt. John Pombe Magufuli ndio wakati wake aliopewa na Bwana kutenda yale aliyoyatenda na sisi kama Watanzania tuyaone na ikiwezekana tufate dira hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumesikia tamko hapa, Azimio la Kumpongeza Mheshimiwa Rais, mama yetu Samia. Hakika ni kwamba huwezi kutenganisha shughuli iliyofanywa na Dkt. John Pombe Magufuli na mama yetu Samia Suluhu ambaye alikuwa Makamu wa Rais. (Makofi)
Kwa msingi huo, hatuna shaka mama aliyepokea kijiti hiki amekipokea kutoka kwa mtu sahihi, na kwa sababu ya maandiko amekipokea wakati sahihi na hatuna shaka atalivusha taifa hili kama ambavyo wengi tunayo matumaini makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba sisi kama Watanzania na sisi kama Wabunge tunafahamu lindi kubwa ambalo tunapita sasa. Lakini mimi niombe kutumia nafasi hii, nafasi ambayo leo tumepata mabadiliko ya uongozi bila kutegemea, ni wakati ambao sisi kama taifa na watu tuliopewa dhamana, ni wakati sasa wa kutenda sambamba na yale tunayoamini kwamba yatakwenda kuwasaidia Watanzania walio wengi na maskini.
Tumejionea mfano amesema hata Mheshimiwa Dkt. Mpango hapa asubuhi namna ambavyo umati tuliouona kwenye kila mkoa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alikopita, ni ishara ya kwamba watu wanatamani kuona changamoto zao zinasemewa na kutatuliwa kwa kina na kwa vitendo.
Hatuna shaka mama ambaye naamanini sana. Na tumpe heshima hii ya kumuita mama, tusiseme tu mwanamke kwa sababu tunaamini ni wakati wa wanawake lakini tukimpa mama tunakuwa tunamtengenezea heshima na uzito mama huyu ambaye kwa mara ya kwanza katika taifa letu amepata nafasi hii na ninaamini anakwenda kutengeneza historia ambayo itajengwa na itakaa kwenye vizazi na vizazi kwa sababu inawezekana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimemsikia siku moja akihojiwa na TBC, ni namna gani anawaza na kufikiria kama ipo siku nchi hii itapata Rais mwanamke. Mama huyu kwa hekima akasema kama imetokea leo kwa mara ya kwanza Makamu wa Rais ni mwanamke, kwa nini huko mbele isiwezekane? Jambo lolote chini ya jua linawezekana kama tu Mungu amekupangia safari hiyo.
Kwa hiyo inawezekana hakujifikiria yeye akafikiria watu wengine kwenye vizazi vinavyokuja; lakini hakika kumbe Mungu alimpangia yeye na hakika amempa. Tumuombee dua, tumuombee mapenzi makubwa, lakini kikubwa zaidi tuendelee kumuombea hekima, busara na uchapaji kazi ambao utatupa dira na kutuonesha Watanzania. Safari iliyoanzishwa na Dkt. John Magufuli ndiyo kwanza sasa imeanza kwa sababu imepokelewa na mama, na wote tunaamini mama akiachiwa familia watoto hawawezi kufa njaa, na vivyo hivyo, Tanzania haiwezi kubaki kama ilivyokuwa, tutakwenda kwenye wakati ambao tutavuka salama, na tena salama kuliko wakati wowote. Bwana ambariki sana Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan na aendelee kumpa mapumziko mema huko aliko Dkt. John Pombe Magufuli.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, naunga mkono maazimio yote mawili. Ahsante sana. (Makofi)