Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kutambua na Kuenzi Mchango wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa Utumishi wake Uliotukuka Pamoja na Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Hon. Ali Hassan Omar King

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Jang'ombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kutambua na Kuenzi Mchango wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa Utumishi wake Uliotukuka Pamoja na Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kupata nafasi hii. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema aliyetupa uhai, lakini pia nikushukuru wewe kwa kunipa hii nafasi. Ingelikuwa inaruhusiwa katika Bunge lako, ningelisema kwamba kitendawili na halafu wangeliniitikia tega, mtanikumbuka, mtanikumbuka, hicho ndio kitendawili ninachokipiga. Maana yake mtajua thamani yangu wakati mie mwenyewe sipo na mtanikumbuka kwa mazuri hamtanikumbuka kwa mabaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, mtu mwenye kusema maneno hayo huyo ni mtu ambaye anahesabiwa mwenye maono. Je, hivi sasa hivi hatumkumbuki? Tunamkumbuka. Sasa ili tuone kama huyu mtu ana maono tulinganishe katika historia na watu wenye maono duniani ambao waliishi kwa maono na wakafanya maono. Mwenyezi Mungu alimwambia Musa nenda kwa mja wangu ambaye huyu utamkuta nimempa hekima na elimu, fuatana naye umsikilize atakwambiaje. Musa akaenda akamkuta Hidhri, Hidhri akamwambia tutafuatana, lakini naomba nitakachofanya usiniulize mpaka nitakapokuja kukwambia mwisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, Hidhri akakuta Jahazi akaitoboa, Musa akalalamika akasema unatoboa jahazi ambayo wenyewe wanafanyia kazi katika bahari zao, akamwambia nilikwambia usiniulize utajua nini maana yake mwisho. Akakuta kijana, Hidhri akamuua, Musa akasema unaua nafsi? Akamwambia nilikwambia usiniulize, nilikwambia huwezi kusubiri kufuatana na mimi. Akafika Hidhri akaomba chakula mahali wakanyimwa, lakini katika mji ule ulikuwa unajengwa ukuta, baada ya kunyimwa chakula na maji Hidhri akamwambia Musa, tujenge ukuta, Nabii Musa akalalamika akasema khaa! hawa watu jambo waliotufanyia sio zuri, ndio wewe unasema kwamba tuwasaidie? Akamwambia hapa ndio mwisho wetu mimi na wewe, hadha firakun baini wabaina, saunabi-ukabitaawil maalam tastatwii alaihi swabra.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nakwambia maono yangu, ile safina au jahazi niliyoitoboa ilikuwa ya maskini, maskini hawa wakifanya kazi kwenye bahari, lakini mbele kule wanakokwenda kuna mfalme kila jahazi mpya anaichukua yeye, tumeitia aibu ili aiache, hilo ono la kwanza. Kijana tuliyemuua wazazi wake walikuwa ni waumini lakini tulikuwa tunahofia atawaingiza katika shirki, watampenda mtoto zaidi kuliko kumpenda Mungu, kwa hiyo tumetaka kufanya hivyo ili kuona hivyo. Mwisho, ukuta tumejenga ni wa mayatima wawili chini yake kumewekwa hazina.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tulinganishe tunaingia katika madaraka, Rais Dkt. John Pombe Magufuli Hayati, alisema nazuia mikutano ya siasa kwa mtu ambaye aliokuwa hajashinda jimbo wala hana nchi, nazuia mikutano watu wakalalamika, lakini je, haya maendeleo ambayo tumeyapata sasa hivi tumeona reli na miradi yote ambayo imefanyika ingelikuwa tunafanya siasa katikati tungefikia maono haya? Mtanikumbuka, huo ni uono wa kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tuangalie katika kubadilisha Sheria za Madini, kuna watu walikaa hapa wakasema tutashtakiwa, ndiyo wale waliokuwa wakilalamika kwamba wanataka waambiwe palepale. Je, sasa hivi hatumiliki rasilimali zetu wenyewe? Tunamiliki, sasa haya ni maono, namzungumzia Dkt. John Pombe Magufuli katika maono. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nije katika jambo moja ambalo niliseme la kumuenzi Hayati. Walikuwa wakifanya uzalendo, uadilifu na uwajibikaji kwa sababu wanamstahi na kumwogopa Dkt. John Pombe Magufuli Hayati, ameshafariki na hayupo, lakini kama wale ambao waliokuwa wanakuwa wazalendo, waadilifu na wanachapa kazi na wawajibikaji kwa sababu ya mama Tanzania, basi bado mama Tanzania ipo, hiyo ndio njia ya kumuenzi Rais wetu Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alikuwa ni mja wa Mungu, hivyo kama kuondoka kwake sisi tutarudi tena tuanze kula rushwa, tutakuwa tena wavivu na wazembe? Atakayefanya hivyo hataidhuru nchi yake, atajidhuru yeye mwenyewe. Kwa hiyo, hiyo ndio njia ya kumuenzi Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)