Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilindi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji wa mwanzo kabisa kwenye suala la Waheshimiwa au mashahidi kwenye jambo ambalo liko mbele yetu hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mjumbe wa Kamati hii kwa muda mrefu kidogo. Kwa uhakika naweza kusema kwa uzoefu mdogo ambao nilikuwa nao katika Kamati hii nimeshuhudia vituko vya ajabu kabisa kabisa.
Mheshimiwa Spika, Kamati yako inafanya kazi kwa mujibu wa taratibu na kanuni ambazo tumezitunga sisi wenyewe Wabunge na tunategemea kabisa wewe kama Mbunge umeaminiwa na wananchi na siyo Mbunge tu wa Jimbo ni Mbunge wa Tanzania nzima. Mwenendo wako, kauli zako, tabia zako lazima zifanane na nafasi uliyopewa. Kwa hiyo, siku zote unapozungumza lazima utafakari wewe ni nani? Unazungumza na akina nani? Hayo ndiyo yatakayokusaidia kuepuka haya ambayo leo tunayazungumza mbele ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikianza na shahidi namba moja, ndugu yetu Mheshimiwa Josephat Gwajima, mimi namuita ni shahidi kwa mujibu wa taratibu tulizojiwekea. Hakika hakuitendea haki hata mara moja Kamati hii, hakuwa na nidhamu, hakuwa na heshima hata mara moja, hata ujio wake mbele ya Kamati ilikuwa inaonyesha dhahiri kabisa kwamba alikuja kwa kejeli na dharau iliyopitiliza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitoe mfano mmoja tu, tulipomuuliza ni wapi unapotenganisha shughuli za Kanisa na shughuli za Ubunge hakuweza kutoa jibu la moja kwa moja, hakuwa na jibu. Aliiambia Kamati kwamba anazungumza na waumini wake kwenye Makanisa zaidi ya 140 duniani. Tulipomuuliza ni wapi unaweza ukabana taarifa zako kwamba hizi ziwafikie waumini wako na wananchi duniani kwa ujumla hakuweza kutoa majibu hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la kusema kwamba wapo watumishi wamepewa pesa, alipoulizwa hakutoa majibu. Pia tulijiuliza heshima ya chombo hiki na heshima ya mihimili mingine inalindwa na wewe, tulipomuuliza hilo hakujibu hata mara moja.
Mheshimiwa Spika, lakini tupime athari ya kauli zake toka ameanza, mimi niungane na ushauri wa Kamati hii kwamba ukiacha Maazimio leo ambayo mimi naunga mkono vyombo vingine viende vikatazame athari ya kauli zake ni nini. Nani asiyejua hapa kwamba wananchi wa Tanzania wanakufa kwa Corona na ni kiongozi gani wa Serikali amesema kwamba kuchanja ni lazima lakini yeye kauli zake zinathibitisha na zinaonyesha kwamba viongozi wetu wa Serikali wamelazimisha wananchi wachanjwe. Hili jambo kwa kweli halina afya kwa maendeleo ya nchi yetu na lazima tusimame imara tulinde chombo hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la ndugu yetu Mheshimiwa Jerry Silaa mimi na Waheshimiwa wenzangu wajumbe wa Kamati hii tulijiuliza huyu ni Mbunge mgeni kweli, lakini huyu ameshika nafasi kadhaa katika nchi yetu katika nafasi ya kuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam. Pia ulimpa nafasi aombe au arekebishe maneno yake hakufanya hivyo, hii ni dharau kwa Bunge na ni dharau kubwa kwako wewe Spika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini alipofika mbele ya Kamati kwa kuonyesha kwamba alidhamiria alichodhamiria na alisimamia kwa kile alichokuwa amekizungumza alikuja na ushahidi wa vitabu zaidi ya kumi, hakuwa na dhamira ya kuomba radhi.
Mheshimiwa Spika, wewe ni shahidi zimekwishaletwa kesi nyingi tu na kwa sababu Kamati hii ni ya kwako ulisamehe watu wengi hata Kamati imesamehe watu wengi lakini kwa jinsi alivyokuja mbele ya Kamati alikuja na msimamo kwamba alichokizungumza ni sahihi. Jambo hili siyo sahihi hata kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini nikumbushe hakutii wito wa Kamati kwa sababu hata katika taratibu za kawaida unapokuwa una kesi ukipewa summons ya kwanza hupewi summons nyingine hakufika mbele ya Kamati. Kibaya zaidi alipoona kuna wito wa kukamatwa na Polisi aliamua kufika saa 12 asubuhi ndani ya ukumbi wa Kamati kinyume cha utaratibu wa kuendesha shughuli zetu pale. Pia huo ni uvunjifu na ukosefu wa adabu wa Mheshimiwa Silaa. (Makofi/ Kicheko)
Mheshimiwa Spika, tunapochaguliwa tuna taratibu tunapewa mafunzo na watumishi wetu, hata kwenye iPad kuna mada zipo hapa za kuonyesha stahili zetu, Kamati ilimuuliza Shahidi Mheshimiwa Jerry Silaa, je, unajua kwamba allowance hizi hazikatwi kodi? Anasema hajui. Aliposomewa akakiri kwamba leo ndiyo amefahamu kwamba allowance hazikatwi kodi. Sasa leo unawezaje kumuamini na kumpa nafasi hiyo kuwa Mjumbe wa PAP mtu ambaye hajui hata sheria kwamba allowance za kibunge hazikatwi kodi. Kwa hiyo, kwa utaratibu ule ule anakosa sifa za kuwa mjumbe wa PAP. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ili kuweka utaratibu ulio imara na sifa kwa Bunge lako Tukufu wakati mwingine tunapowapa Wabunge nafasi za uwakilishi tuwapime katika viwango tofauti tofauti. Sisi imetuwia vigumu sana kuwazungumza Wabunge wenzetu ambao ni wajumbe wa Kamati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, basi baada ya kusema hayo, nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)