Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ndanda
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na historia ndefu ya elimu ya Wilaya ya Masasi, naomba kiambatanisho namba 1 na 2 vipokelewe kama mchango wangu wa maandishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kudidimia kwa elimu Wilaya ya Masasi. Wakati Tanganyika tunapata uhuru mwaka 1961, kiwango cha elimu literacy rate katika Wilaya ya Masasi kilikuwa asilimia 85. Kiwango cha juu kabisa kuliko Wilaya zote za wakati ule; hii haikuwa kwa bahati tu bali ilitokana na juhudi za dhati za wamisionari (wazungu) wa Kanisa Anglikana kwa kiwango kikubwa tangu mwaka 1876 na wale wa Kikatoliki kuanzia mwanzo wa karne ya 1900. Vijiji vyote vikubwa vilikuwa na kanisa (mtaa – Kianglikana au Paroko Kikatoliki). Na vitongoji vilikuwa na makanisa madogo (Anglikana) au vigango (Kikatoliki) vilivyosimamiwa na walimu au Makatekisti.
Vijiji hivi vyote na baadhi ya vitongoji palikuwa na shule za Wamisionari. Shule za Serikali kwa maana ya shule za Serikali ya Mitaa (district council/native authority) zilikuwa mbili tu Wilayani, middle schools nazo zilianzishwa miaka ya mwanzo mwa 1950 Chiungutwa na Mbemba. Shule hizi zote za vijijini za misheni zilipokea wanafuzi wa dini zote mbili kuu, kikristo na kiislamu. Hivyo ni dhahiri mtandao wa shule hizi za misheni ulikuwa mkubwa Wilayani Masasi, kiasi cha kuwezesha kufikisha asilimia hii kubwa ya 85 wakati tunapata uhuru. Ukaguzi wa hizi shule ulikuwa wa makini na ukifanywa na wamisheni wenyewe (wazungu) na hivyo elimu kuwa bora.
Vivyo hivyo, shule za sekondari na za ualimu katika Wilaya ya Masasi zilikuwa za misheni, sekondari ya Chidya ya Anglikana na Ndanda ya Katoliki pia Chuo cha Walimu wa kike pekee Ndwika na vyuo vya wakunga Lulindi cha Anglikana na Ndanda cha Katoliki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu masomo ya juu, wanafunzi waliotakiwa waendelee na masomo zaidi walitoka katika shule hizi mbili za misheni kwenda katika shule kuu mbili za misheni za Minaki (Anglikana) na Pugu (Katoliki). Pia waliweza kwenda shule za Serikali za Tabora, Tanga na kadhalika na baadaye Makerere.
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwango vya juu vya nidhamu, uadilifu na uwajibikaji (commitment) ndiyo ishara kuu na misingi ya uendeshaji wa shule hizi za misheni kufuatana na maadili ya kidini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mafanikio, Makatibu Wakuu, viongozi Ikulu wawili wa kwanza baada ya kupata uhuru, Dunstan Omari na Joseph Namatta walisoma Chidya hata baadae kufika Makerere wakitokea Minaki. Pia enzi za ukoloni Dunstan Omari alikuwa District Officer wa kwanza Mwafrika. Rais Mstaafu Benjamin Mkapa pia ni zao la shule ya misheni ya Ndanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya wengine waliofanikiwa kupata uongozi wa juu katika Awamu ya Kwanza kutoka shule za Chidya, Ndada na Ndwika ni kama ifuatavyo:-
1. Mzee Fredrick Mchauru – Katibu Mkuu Wizara mbalimbali na Mshauri wa Rais
2. Nangwanda Lawi Sijaona – Waziri
3. Mama Thecla Mcharoru – Katibu Mkuu UWT
4. Yona Kazibure MSc (Physics) wa kwanza Makerere – Chief Engineer Radio Tanzania.
5. Mama Anna Abdallah – Mwenyekiti UWT
6. Beda Amuli – Architect Mwafrika wa Kwanza Tanzania
7. Mama Kate Kamba - Katibu Mkuu UWT
8. Yuda Carmichael Mpupua – Naibu Katibu Mkuu na Chief Agricultural Officer
9. Dkt. Isaya Mpelumbe – Director of Veterinary Service na Kamishina wa Kilimo na Mifugo
10. Alex Khalid – Katibu Mkuu
11. Major Gen. Rowland Makunda – Mkuu wa Navy kuanzia vita vya Idi Amin
12. Philip Magani – Chairman/Managing Director CRDB
13. Paul Mkanga – Katibu Mkuu
14. Dkt. John Omari – Fellow of the Royal 1 Surgeons wa kwanza Tanzania
15. John J. Kambona – Director of Fisheries Tanzania na FAO Headquarters Rome.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia walimu wa kwanza kutoka Makerere walifundisha shule maarufu za Serikali za sekondari tangu ukoloni kama vile Tabora, Old Moshi, Tanga ni Curtius Msigala, Joseph Banali, Peter Nampanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya siasa na hatima. Tangu shule zile za misheni kuwa chini ya Serikali mbali na nyingine nyingi kujengwa, kwa jumla kiwango cha elimu Wilayani Masasi kimezidi kuporomoka. Ufaulu katika shule zote za awali na sekondari umezidi kushuka. Ufaulu wa shule za awali kuingia sekondari umekuwa mdogo na Wilaya kuwa mojawapo ya zile za chini kabisa nchini inashangaza hata shule maarufu kongwe (tangu mwaka 1923) ya Chidya haijapata hadhi ya kuwa high school hadi leo, kuna nini? Hili ni jambo lisilokubalika na viongozi, Wabunge, Madiwani na watawala wanawajibika kuelewa awareness na kuhimiza kulifanyia kazi kwa nguvu zao zote wakishirikiana na wananchi kurekebisha hali hii mbaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mwanaharakati aliyeandika kitabu How Europe Underdeveloped Africa, si vizuri mwingine akaandika kingine. How Tanzania Underdeveloped Masasi.