Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge

Hon. Tunza Issa Malapo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Awali ya yote kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu na nataka kuwaambia umma wa Watanzania kwamba Mheshimiwa Gwajima Josephat ameshindwa kuthibitisha mbele ya Kamati, kuleta kielelezo chochote cha zile tuhuma nzito ambazo amezitoa kwa Viongozi Wakuu wa Nchi hii. Alisema ana vielelezo, atakuja kusema, nawaambia hakuja hukusema jambo lolote la msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba Watanzania kwanza watambue hilo, amekuja pale na vituko tu, mara hataki kiti, mara hataki microphone, mara leo nasimama, lakini hakuleta kielelezo chochote, tulimhoji maswali na sisi tulikuwa sober, inawezekana angetusaidia jambo kuna jambo analijua, lakini kwa masikitiko makubwa hajui lolote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, amesema chanjo ya J&J imeletwa kwa sababu watu wamekula pesa. Tukamwambia tunaomba Ushahidi, hana. Akasema watu watakao chanjwa watakuwa vichaa, watakuwa hawazai, sijui tutatembea barabarani tunaongea wendawazimu, tuletee Ushahidi, hana.

Mheshimiwa Spika, akatoka hapo tulipomwambia hivi haya mambo unayoyasema wewe huoni kama unaleta taharuki kwenye nchi. Halafu mbaya zaidi huyo kiongozi aliyeyazungumza haya yupo kwenye chama chako, kwa nini usitafute venue ya kwenda kuongea naye ukamshauri, unakuja kuyatoa mbele ya umma? Kwa masikitiko makubwa alisema hivi; yale ameyasema, atasema akiwa ndani ya Bunge, atasema akiwa nje ya Bunge, atasema akiwa juu ya dari na atakayemsemesha atasema zaidi ya mara mbili.

Mheshimiwa Spika, nakupa taarifa, Mheshimiwa Gwajima alitwambia kwenye Kamati kwamba, ataendelea kusema, sasa kazi kwenu ninyi wenye mamlaka. Yeye amesema ataendelea kusema, amesema mbele ya Kamati na Hansard zipo zimerekodi vizuri sana, kwa hiyo tujiandae. Leo jumatatu, tusubiri jumapili inayokuja hatujui kitakwenda kusemeka kitu gani. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, naomba sasa niongee suala la Mheshimiwa Jerry Silaa. Hapa mkononi mwangu nimechukua salary slip, hii ni ya kwangu mimi Tunza Issa Malapo. Siwezi kutaja mshahara wangu, mshahara ni siri, siwezi kutaja figure, naogopa na mimi ndiyo nitarudi kule kule kwa mwenzangu, lakini nataka kuwaambia Watanzania, nitakupa hii ya kwangu kwa ridhaa yangu uione labda inawezekana hujapata muda wa kuangalia, mimi hii ya kwangu nakatwa kodi. Ni Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tena nakatwa kodi ya kutosha tu, ukilinganisha na watumishi wengine wa umma, sisi Wabunge tunakatwa kodi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulipokuwa kwenye Kamati tunashangaa, huyu mwenzetu haya mambo ameyapata wapi? Tukajua basi angalau atajirudi, aseme labda niliteleza, kama aliteleza basi tumwinue, twende naye, lakini mwenzetu ndiyo kwanza ametuletea vitabu mpaka vimemziba hatumwoni. Sasa yale ya vitabu sisi tukayavumilia kwa sababu, jamani Waheshimiwa Wabunge tunaongea leo tunaongea kwa fact, hivi hili suala la Jerry lilipaswa lifike hapa lilipofika? (Kicheko)

WABUNGE FULANI: Wala, hapana.

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, katika hali tu ya kawaida, kwa sababu binadamu yeyote kukosea ni jambo la kawaida na ndiyo maana tunaenda Misikitini na Makanisani tunaenda kuomba msamaha. Hili suala lake mimi kwa akili yangu ya kawaida tu ndogo, ni kwamba mwenzetu mimi nilichukulia ameteleza, sasa kama ameteleza mwenye mamlaka Mkuu wa Mhimili alimwambia, you just go there, kawaambie watu kwamba niliteleza kwa sababu ushahidi si upo. Hapa hatupigi ramli ndio maana mimi mkononi kwangu nimeshika salary slip, hatufanyi ramli tunaongea vitu ambavyo vipo na vinaonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lilikuwa ni suala la kwenda tu kusema kwamba nimeteleza, lakini kwa nini hawezi kwenda kusema? Ninachoona mwenzetu ana kiburi, yaani amejaa tu, ile wanayosema kunyanyua mabega, kwamba nionekane mimi nakwenda kusema nimekosea, nimefanya hivi, which is not good, katika maisha ya kawaida ya mwanadamu yoyote.

Mheshimwia Spika, sasa Mheshimiwa Jerry anatakiwa, kwanza naunga mkono adhabu aliyopewa, lakini nafikiri, sijajua sijui niseme anatakiwa apate psychological counselling sijui kitu kama hicho. Siongei hivyo kwa maana kwamba namtukana au nini, mimi ni mwalimu na Saikolojia ni somo ambalo tunafundishwa, sometimes mtu unaweza ukakuta anafanya mambo wewe unashangaa, kwa nini huyu mtu anafanya hivi! Hili suala kwa upande wangu naliona ni kubwa, lakini ni dogo, endapo tu yeye angeamua kuli-handle kwa namna ile ambayo mimi naiona.

Mheshimiwa Spika, sisi tunakatwa kodi na ile posho ambayo hatukatwi kodi ina matumizi, kama mimi nimepewa hela ya mafuta ya lita 10, nitalipia kodi hivi nitapata yale mafuta lita 10? Sipati, kwa hiyo ni mambo ya kawaida ambayo yanataka tu uelewa wa kawaida. Nawaambia Watanzania sisi Waheshimiwa Wabunge tunakatwa kodi kwenye mishahara yetu, tena kodi ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)