Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge

Hon. Joseph Anania Tadayo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kupata nafasi hii. Nami pia kwa nafasi yangu kama Mbunge na Mjumbe wa Kamati iliyoleta hoja, naunga mkono hoja ambayo imeletwa kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulipewa kazi hii na wewe ili kuwapa haki wenzetu hawa ambao kwa mujibu wa kanuni tunawaita mashahidi, kuwapa ile haki yao ya kikatiba ya kuwasikiliza. Tuliwasikiliza chini ya kiapo na wakakubali kwamba kweli hizi kauli ni wao walizitoa. Inakuja sasa kuangalia juu ya uhalali wa kauli hizi kisheria kama ambavyo ripoti imezungumza kwamba unasimama, unasema kwamba viongozi wamepewa fedha ili kuruhusu chanjo ambayo si salama iingie. Kwamba kila anayetetea chanjo, kila anayechanjwa ikiwa ni pamoja na mimi kwamba ni hela, ni hela, ni hela. Halafu unafika mahali unajigamba kuwa juu ya kila mtu, kuwa juu ya Bunge, kuwa juu ya Spika kwamba mimi naweza nikafyatua mtu ndani ya Bunge, naweza nikafyatua mtu nje.

Mheshimiwa Spika, sasa ni wazi kabisa kwamba hata bila kusoma sheria, kila mtu anapaswa kuthibitisha yale mambo ambayo anayasema dhidi ya wenzake, kwa sababu kila mtu anastahili jina lake liwe safi kama lilivyo. Kwa maana ya kwamba mimi nimeajiriwa, nafanya kazi ni Waziri wa Sekta au nafasi yeyote ile. Kazi yangu naifanya kwa mujibu wa sheria, sasa kama unasema kwamba mimi nimepewa hela ili nifanye hivi, basi unao wajibu wa kuthibitisha jambo ambalo shahidi wa kwanza, Mheshimiwa Gwajima alishindwa kabisa kufanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, hali kadhalika kwa shahidi wa shauri la pili, Mheshimiwa Jerry Silaa, dai lake kubwa kwamba mishahara ya Wabunge haikatwi kodi. Sasa waraka wa msingi, primary document ya kuthibitisha mshahara wa mtu huwa ni salary slip ile ambayo inatumika kukulipa wewe mshahara. Mmiliki wa ile document ni yule anayekulipa, sasa Mhasibu Mkuu wa Bunge ameshakuja, ameshatoa ile, ametenga ile salary slip ni hii hapa, inakatwa kodi na amesema inakatwa kodi na ametueleza kwamba hata wakusanyaji kodi wenyewe waliwahi kuja wakatazama hili jambo, wakaridhika nalo. Hata hivyo, bado mtu unasisitiza kwamba upo sahihi. Maana yake sasa huu kwa kweli ni uvunjaji sheria wa makusudi tu ambao ndiyo maana Kamati ikafikia hapo kutoa adhabu hizi ambazo mimi naziunga mkono kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni vizuri sisi Wabunge tukakumbuka kwamba baada ya kuchaguliwa tuliapa kuilinda, kuitetea na kuhifadhi Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katiba hii ndiyo iliyoweka hii mihimili ambayo tunazungumzia habari ya kuigonganisha na kuidhalilisha. Katiba hii ndio inayogawa mamlaka na madaraka ya watu kufanya kazi. Pia Katiba hii imetupa nafasi hasa sisi Waheshimiwa Wabunge namna ya kuhoji au namna ya kurekebisha mambo ambayo tunafikiri hayaendi sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Ibara ya 63, kwamba tunayo mamlaka ya kumhoji Waziri yeyote juu ya suala lolote lile ambalo tunaona haliendi sawa. Sasa endapo basi tunadhani kwamba Serikali inakwenda ndivyo sivyo hatuna mamlaka ya kwenda kuwahojia huko kwenye maeneo yetu, kwenye vikundi vyetu vya ngoma au kwenye Makanisa au mahali pengine popote pale. Sheria inatuongoza na kutupa wajibu kabisa wa kuja kuihoji mahali ambapo ni stahiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hali kadhalika, endapo basi mtu ameona kwamba sheria inayotulipa sisi mishahara kama ilivyo kwenye kifungu cha 20 cha ile National Assembly (Administration) Act, haipo sawasawa, basi unataka kuanzisha mchakato wa marekebisho, basi sidhani kama mchakato unaanzishwa hivyo. Sisi ni Wabunge, tunafahamu utaratibu wa kuanzisha mchakato wa marekebisho ya Katiba ili hata ile posho ya mafuta ambayo ukienda kununua mafuta tayari kodi imeshakatwa, kama unataka na yenyewe ikatwe tena sijui mara ya ngapi, basi mchakato wa kisheria upo wa kufanya hivyo, sio kwenda kuchochea wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sasa hivi, hizi kauli za wenzetu hawa wote wawili effect yake pia ni kuwachochea wananchi kuichukia Serikali. Kwa sababu kwa upande mmoja ya Mheshimiwa Gwajima ni kwamba anawachochea wananchi waone kwamba Serikali haijali afya zao, Serikali haijali usalama wao. Kwa hiyo watu wanapokea tu fedha huko wanaleta machanjo ambayo sio sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii nyingine ni kwamba Serikali ina upendeleo kwamba wengine wanakatwa kodi, wengine hawakatwi kodi. Kwa hiyo kauli zote hizi mbili zinakwenda zaidi hata ya makosa yetu ya kikanuni, kuna uchochezi hapa pia. Kwa hiyo ni vizuri kabisa Azimio hili la Bunge likapita kama ambavyo Kamati imelileta. Naliunga mkono, twende hivyo, turekebishane ili tuweze kwenda sawasawa katika kuwatumia wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja kwa mara ya pili. (Makofi)