Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Jang'ombe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Spika, ahsante. Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu.
Pia napenda kukushukuru wewe kwa kunipa hii nafasi ambapo Wabunge wengi sana wamezungumza kuonyesha hisia na kuonyesha kushangazwa na vitendo vya Wabunge wenzetu ambavyo vimetokea na zile comedy zote zilizojitokeza. Nafikiri kuna neno moja tu hapa tukisema, tutaliweka sawa hili. Kuna msemo mmoja unasema Khalif Tunraf; wewe ukitaka ujulikane, upate umaarufu, basi wewe nenda kinyume tu.
Mheshimiwa Spika, kule kwetu kuna mtaa mmoja unaitwa Mchambawima; na ni kwa sababu huyo mtu hicho kitendo alikuwa akikifanya wima, kwa hiyo, alikuwa maarufu mpaka jina la mtaa lipo.
MBUNGE FULANI: Mchambawima! (Makofi/Kicheko)
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Eeh, kwa hiyo, hapa sasa hivi, kwa hivi tunavyoendelea, kwa watu kutaka umaarufu, tutapata wachambawima wengi tu, kwa sababu mtu ukitaka upate umaarufu, basi nenda kinyume. Ukienda kinyume utapata umaarufu; na ndicho kinachotafutwa hapa. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, mamlaka yaliyowekwa yanapaswa yaheshimiwe. Kama tutakwenda hivi kuchezeana na tutaachiana kama hivi, tutakuja kufika mahali pabaya. Amezungumza hapa Mufti wa Kigoma, Mheshimiwa Kilumbe Ng’enda, kwamba mamlaka anatoa Mungu na Mungu ndio anayempa mtu mamlaka na hakuna mamlaka mengine yeyote ambayo hayatoki kwa Mungu. Sasa akitokea mtu akiwa ana dharau mamlaka, hapo moja kwa moja huyo mtu sio wa kumchezea, wala sio mtu wa kucheza naye. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Gwajima ameeleza kwamba Serikali au watu ambao wameshughulika na chanjo wamepewa pesa; huu ni uongo unaoidhalilisha Serikali, unachochea Serikali na wananchi; na kwa nafasi yake kama Mbunge ina maana kwamba moja kwa moja analidhalilisha Bunge kwa sababu yeye amezungumza kama Mbunge. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi sikubaliani naye anaposema kwamba yupo katika mahubiri, alikuwa hayupo katika mahubiri. Ukitazama mtiririko, leo kimesemwa hiki, siku ya pili yeye ndio anajibu. Leo kimefanywa hiki, siku ya pili anajibu, leo kazungumza Waziri wa Afya, anasema pia atamfyatua. Kazungumza Naibu…; alikuwa anajibu hoja kwa matukio ya Serikali siyo mahubiri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tukipata wahubiri kama hawa, nafikiri kuna kesi moja. Kuna kisa kimoja cha Askofu Kibwetere aliwafungia watu Kanisani akawachoma. Kuna Askofu mwingine aliwapeleka watu pale uwanja wa ndege, aliwaambia watapata visa pale, wakalala wiki mbili pale. Sasa wahubiri kama hawa wakati mwingine lazima tuwatazame. Itakuja mahali, yaani ni timing bomb. Bomb litakuja kulipuka!
Mheshimiwa Spika, leo katika familia huko watu hawataki kuchanja kwa sababu ya maneno ya watu. Watu hawataki kufuata taratibu za nchi kutokana na maneno ya watu. Sasa mimi niseme moja kwa moja, naunga mkono hoja ya Kamati; na zaidi vyombo vya usalama, hili jambo linatuharibia. Vyombo vya usalama navyo vichukue hatua kali zaidi. Chama chetu nacho kiangalie kifanye nini katika hili kwa sababu hawa watu watatuharibia nchi, nasi hatutaki kufikishwa mahali pabaya. Hapa tunapokwenda, tunakwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikija katika suala la ndugu yangu Mheshimiwa Jerry Silaa, ni kweli alikuja mbele ya Kamati, lakini mimi mwenyewe nashangaa kwamba kweli tufikie katika hatua hii Wabunge hatujui kama tunakatwa kodi! Au ndiyo tunarudi kule mchambawima! Halafu unakuja mbele ya Kamati, yaani mambo yote yanakuwa ni ya vituko vituko. sasa hii, nahisi adhabu iliyopendekezwa na Kamati naiunga mkono. Pia huku kwenye PAP nako tukutazame, ndiyo mwakilishi wa aina hiyo ndiyo tunampeleka huko. Sasa ni lazima tutazame na lazima tuangalie. Sisi kama Wabunge tukianza kuchafua hali ya hewa tutafika pabaya. Tupunguzeni kutafuta umaarufu jamani! Tupunguzeni kutafuta umaarufu, hili litatuharibia na tutaiharibu nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja ya Kamati, lakini zichukuliwe hatua nyingine zaidi kwa sababu tunakwenda kuharibu usalama wa nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, nashukuru.