Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge

Hon. Elibariki Emmanuel Kingu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kukushukuru sana wewe binafsi kwa kunipatia nafasi kuwa msemaji wa mwisho, kwenye hoja iliyoko mbele yetu. Jambo la kwanza ambalo nataka nilizungumze kuna dhambi moja kubwa sana watu wanaifanya kwa sababu tu wanajua kwamba Rais Magufuli amekufa na hawezi kujitetea. Gwajima katika mahubiri yake niliyoyasikia aliyoyatoa kule Kanisani, amesikika akisema toka Rais Magufuli afe mambo yamekuwa yakienda ndivyo sivyo akiwa ananukuu jambo la chanjo ya Corona.

Mheshimiwa Spika, baba wa watu Rais Magufuli amefanyakazi yake ametimiza muda wake Mungu amemruhusu apumzike. Ametenda haki na mema mengi kwenye Taifa hili, Hayati Magufuli aachwe apumzike asihusishwe na mambo ya hovyo. Rais Magufuli alipokuwa madarakani alichokishauri alilishauri Taifa tusiwe na haraka ya kukimbilia chanjo lakini hakuzuia Taifa likijiridhisha lisichukue chanjo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii imekuwa ikitumika kama kichaka, Magufuli, Magufuli, Magufuli, Magufuli muacheni Rais Magufuli apumzike na ninasema huko aliko, kaka yangu Askofu Gwajima anisikilize kwa sababu kama mdogo wangu Ditopile alivyosema, sio mnafiki. Nilimfuata Gwajima kwenye simu yake ya kiganjani nikamuambia haya unayoyafanya ninakushauri unyamaze hayana maslahi na Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nayasema haya kwa sababu, Askofu Gwajima anasema ana Kanisa na anatumikia watu wa Mungu. Neno la Mungu katika Warumi 13:1 linasema: Kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu; kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na ile iliyopo imeamriwa na Mungu. Na ndio maana kwa watumishi wa Mungu wanaomjua Mungu vizuri, Yesu wakati anazaliwa utawala wa Herode palikuwa pana sensa inaendelea Jerusalemu. Yusufu na Mariamu wakiwa ni wasomi wazuri wa Biblia wale watu wakiwa wamejazwa na Roho Mtakatifu wali-comply na agizo la Herode la Serikali tena wakati huo, Jerusalemu iko chini ya utawala wa Rumi wakaondoka kwenda kuhesabiwa kwa kutii mamlaka ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, na wakati huo nayasema hayo kitabu cha Mathayo 2:1 kinaonyesha namna Yesu alivyofanya msafara kwenda kutii agizo la mamlaka tena chini ya utawala ambao tunaweza tukasema kwamba walikuwa chini ya ukoloni. Lakini kama hiyo haitoshi Luka 12:7- 9 neno la Mungu linasema, Mungu huyu anajua idadi mpaka ya nywele zilizoko katika kichwa chako. Sasa kama Mungu anajua idadi ya nywele kwa nini Mariamu hajasema kwamba Herode anatuita kwenda kuhesabiwa, Mungu anajua idadi ya nywele wagomee mamlaka ya wakati huo. Hiki anachokifanya Gwajima ni kiburi kilichojaa, kuvimba na kulewa sifa za dunia na sio sifa za kumuwakilisha Mungu katika madhabahu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninayasema haya kwa sababu, Askofu Gwajima ametoa tuhuma nzito sana kwa nchi na nafikiri haya mambo nimejiuliza maswali. Hivi ni kweli Jeshi la Polisi hawaoni criminality iliyopo kwa statement za Gwajima? Hivi kweli Jeshi letu la Polisi halioni hatari ya kauli za Gwajima kwamba zinaweza zikasababisha hata Serikali ikapinduliwa kwamba Rais ameamua kuuza watu wake? Nimejiuliza maswali nimekosa majibu!

Mheshimiwa Spika, jambo ninalotaka kulisema Askofu Gwajima yuko hapa jirani na ninajua watu watampelekea clip na zimfikie kwa sababu tabia ya unafiki msabato mimi sijawahi kufundishwa, nimefundishwa kuita nyeusi nyeusi kuita nyekundu nyekundu. Kitendo alichokifanya Askofu Gwajima jambo la kwanza, kwa mujibu wa uchambuzi wangu Askofu Gwajima alidhamiria kuichonganisha Serikali ya Mama Samia Suluhu na wananchi ili watu waache kuwa na imani na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kitendo cha Askofu Gwajima kujitokeza hadharani na kuwaambia watanzania kwamba chanjo hii mnayokwenda kuchanjwa haijafanyiwa utafiti, chanjo hii mkiitumia italeta madhara hilo jambo ni it is a very big if not huge is subordination kwa mamlaka za nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema naungana na Mariamu Ditopile, adhabu zitakazotolewa kwa Askofu Gwajima kwa hili, zisiishie hapo hata huyu Halima Mdee aliyekuwa Mbunge wa Kawe hajawahi kutufanyia vitimbi vya namna hii anavyovifanya Askofu Gwajima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili jambo nataka niseme kwa dhati kabisa limetufedhehesha na mimi nilikuwa nashangaa sana kwa nini chama changu mpaka leo wamekaa kimya hawajachukua hatua? Mwanachama anafikia stage ya kufanya haya mambo mazito mpaka Spika unaamua kumuita, Chama cha Mapinduzi kile tunachokijua. What is wrong with my party? Kuna shida gani? Jambo hili ni kutaka kukwamisha mipango. Hivi nilikuwa najiuliza amesema Kilumbe Ng’enda Rais Dkt. Magufuli kama Mungu angekuwa hai mpaka leo, Gwajima angeweza kufungua mdomo wake na kuleta hizi chokochoko? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakuambia Wabunge tuko hapa kama kuna Mbunge anafikiri ya kwamba atatumia forum kwa sababu tu hakupendezwa na Rais Samia kuwa madarakani walahi nakuambia tuta-deal naye. Sisi tuta-deal naye. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nikuambie kama kuna mtu alikuwa anategemea kupata mamlaka Serikalini imetokea bahati mbaya wote hatuwezi kuwa Mawaziri walioko Mawaziri ukaanza kuwachokonoa walahi nakuambia tuta- deal na wewe. Ninasema ikitokea mmoja wetu anataka kujenga umaarufu binafsi badala ya umaarufu wa Taasisi na kulinda mifumo ya Taifa letu, kabla hawajaja kwako tutatwangana makonde huko, tuweke heshima. (Kicheko/ Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalize kwa kusema pamoja na kwamba naunga mkono maazimio yote ya Bunge, nimemshauri rafiki yangu Mheshimiwa Jerry Silaa kwa dhati ya moyo wangu ninalisema moja ya marafiki zangu wa karibu sana Mheshimiwa Jerry Silaa. Na hata tukio lilipotokea nilimuandikia ujumbe anajua, zaidi ya mara tatu na ninalisema from the bottom of my heart tusiposimama kushauriana kwa lengo la kuelekezana sisi bado vijana nina imani Mheshimiwa Jerry atakutafuta, nina imani atakutafuta kwa wakati wake.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba amechelewa chelewa nina imani atakuja, akija baada ya haya wewe mpokee kama baba akiomba radhi mpokee. Kwa sababu, ninajua wakati mwingine kuna mambo yanatokea hapa mtu unashindwa kuelewa huyu ni huyu ninayemjua? Unajiuliza maswali. Lakini baada ya kusema hayo binafsi nikushukuru sana na nikupongeze sana kwa namna ambavyo umesimama kulinda heshima ya Mhimili huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiacha Mhimili huu udharauliwe hata huko nje heshima yetu sisi Wabunge haitaonekana. Baada ya kusema maneno haya ninataka nimtie moyo Rais wetu aliyeko madarakani asije akadanganywa na mtu. Hatuwezi wote kuwa Mawaziri, Mawaziri walioko tuwaheshimu tuwaunge mkono. Hatuwezi wote kuwa Mawaziri ikitokea hatujapata nafasi tusiwe chanzo cha kuanza kulidhalilisha Baraza la Mawaziri la kumdhalilisha Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakuambia Rais Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Spika, nguvu yake kwa umma ni kubwa wananchi wanampenda haijawahi kutokea katika historia ya Taifa, fedha zinapelekwa kwa wananchi kwa kiwango hiki anachofanya Rais Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaomba jambo moja Mungu aendelee kulibariki Taifa letu, Mungu aendelee kuulinda umoja na mshikamano wa Taifa letu. Mungu amlinde Rais wetu na Mihimili yake yote mitatu ukiwemo wewe Spika. Wasalaam aleykum. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, ninaomba kutoa hoja na kuunga mkono hoja. (Makofi)