Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia machache kuhusu Mpango wa Tatu wa Maendeleo ambayo ni hoja iliyoko mbele yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mipango hii inatengenezwa na inapangwa na mara nyingi kila mwaka tunakaa hapa tunaijadili na baadaye tunaitafsiri katika pesa, tunaipangia bajeti. Kwa hiyo, tunasubiri utekelezaji wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mwingine mipango hii haitekelezwi jinsi inavyotakiwa. Nami napenda niungane na Kamati ya Bajeti. Kamati hii imetoa mapendekezo kwamba kuna haja kubwa ya kuwa na mfumo mzuri katika ufuatiliaji na usimamizi wa mipango yetu, yaani ile tunaita monitoring and evaluation. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu mimi ni Mjumbe wa LAAC karibu miaka mitano, kwa hiyo, tunapata nafasi nzuri ya kukagua miradi ya maendeleo. Miradi iliyo mingi haitekelezeki na nyingine inachukua muda mrefu kwa sababu au Serikali haipeleki pesa au hakukuwa na uhalisia wa miradi hiyo. Kwa hiyo, nashauri kwamba tunapopanga mipango kwanza, miradi iwe ya uhalisia ambayo inaendana na bajeti yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia miradi hii isimamiwe; kuwepo na sera. Serikali ilete sera. Kamati ya Bajeti mimi jana nimeisikiliza sana, nimeona hili ni jambo la msingi sana, kwamba watuletee sera na sheria ili tuweze kuwa na kitengo kizuri ambacho kinafanya ufuatiliaji. Sijasema kitengo hakipo, kipo lakini hakina tija kwa sababu hakuna sheria yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mara nyingi Serikali haitakubali kuleta hii sera kwa sababu Serikali haipendi kufuatiliwa. Nakumbuka wakati tunaanzisha Kamati ya Bajeti, Spika na Naibu walisimama. Kwa hiyo, naomba nikutume, msimamie jambo hili, pale ambapo Serikali itakataa, wale waliokuwa kwenye Bunge wanakumbuka ilivyokuwa mbinde kutengeneza Kamati ya Bajeti; Serikali ilikuwa haitaki na inawezekana katika hili pia haitaki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nashauri Bunge lisimame, mlete sheria. Wakati ule iliposhindikana Bunge lilitunga sheria na Serikali ikashituka ikaleta sheria, kwa hiyo, tukaweza kuunda Kamati ya Bajeti. Bila kuwa na Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini, hii miradi ambayo tunakaa hapa tunapanga haitatekelezeka ipasavyo. Kwa hiyo, hiyo ni hoja yangu ambayo nimeona ni ya msingi ili hata tukikaa hapa tukaandaa mambo, tukapanga na baadaye tukapeleka pesa katika miradi hii, kama hakuna ufuatiliaji na usimamizi; na ifike mahali kama ikibidi tuwe na kamati ndani ya Bunge ambayo kazi yake itakuwa ni kufuatilia kuona kama je, kuna discipline katika bajeti?
Je, Serikali inatimiza tunavyowaelekeza au hakuna discipline kila mtu anafanya anavyotaka? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, napenda kushauri kwamba kama Serikali ikishindwa kuleta, basi naomba Bunge lisimame kabisa liweze kuhakikisha kwamba hiki kitu kinatekelezeka kwa sababu tumekishauri kwa muda mrefu na bila mafanikio.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda sasa niende katika mipango hii na bajeti zetu kuchochea maendeleo ya watu. Unapowaeleza Watanzania kwamba uchumi ni wa kati au uchumi ni mzuri, una maana gani? Kwa sababu Watanzania wetu hawa ambao tunawaita wanyonge; na hili neno “mnyonge” mimi linaniudhi sana. Kwa sababu gani? Ina maana tunataka kuwaambia Watanzania wakubali unyonge na umasikini, yaani waubebe mgongoni, wauwekee na mbeleko kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania sio wanyonge, Watanzania wakipangiwa mipango mizuri, wakaelekezwa, wanaweza wakafanya kazi yao vizuri na nchi yetu ikapata maendeleo. Kwa hiyo, hayo mambo ya kuita Watanzania wanyonge, kwa kweli inanikera sana. Watanzania sio wanyonge, ni watu ambao wana uwezo mkubwa sana kuweza kufanya kazi zao; wakielekezwa vizuri wakawekewa sera nzuri, wanaweza kuendeleza maisha yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, unaposema uchumi kwa mtu wa kawaida anapata maana gani? Maana tuna vijana wasomi hapa wapo wengi, ambao kazi yao ni kutuandikia ma-book hayo. Hayo ma-book yapo, ni yawasomi, lakini Watanzania wa kawaida wanachohitaji ni maisha yao ya kila siku. Wanahitaji mahitaji yao, wanataka kupewa nguvu ya manunuzi kwanza, waweze kuwa na uwezo wa kuendesha maisha yao ya kila siku. Unapomwambia mtu uchumi umekua nyumbani kwake, anaangalia tangu asubuhi anaweza kumudu maisha yake!
Kwa hiyo, hapo uchumi tuuchukulie katika kuhakikisha watu wetu wanakuwa na uwezo wa kumudu maisha yao ya kila siku. Pia mipango hii na uchumi iendeleze maisha yao na huduma za kijamii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, nilitegemea kwamba mipango ya mwaka huu itaangalia maji. Upo ukosefu mkubwa wa maji katika nchi hii. Maswali ya maji yakiulizwa hapa wewe mwenyewe ukiwa hapo unaona watu wanavyonyanyuka, kila mtu anaongelea maji katika jimbo lake. Kwa hiyo, nilitegemea kwamba mpango huu ungeweza kufikiria namna nzuri ya kuweza kuhakikisha kwamba tunaondokana na adha ya ukosefu wa maji katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, unakumbuka mwaka 2020 tulikuja na pendekezo hapa kwamba Serikali ifikirie namna ya kupata pesa kidogo kutoka kwenye mafuta, tufanye re- investment kama tulivyofanya kwenye REA ili kupunguza matatizo makubwa sana yaliyopo ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niligombea Jimbo Bukoba Vijijini huko tulikuwa tunapambana na Mheshimiwa Rweikiza, lakini Jimbo la Bukoba Vijijini lina matatizo makubwa sana ya maji.
(Hapa kengele ya kwanza ililia)
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Itakuwa kengele ya kwanza hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, matatizo makubwa ya maji katika jimbo lile; ukiliangalia lina Kata 29, lakini almost asilimia 55 watu hawana maji. Kwa hiyo, wanapotupa takwimu kwamba kuna maji ya kutosha watu milioni 25, mimi sikubali, kwa sababu ukienda Mkoa wa Kagera kwa mfano, tuna mradi wa maji pale Bukoba Manispaa, ndio mzuri. Nenda Kyerwa, Karagwe, Bukoba Vijijini, Ngara, Biharamulo na kusema ukweli Mkoa wetu wa Kagera hata haukutokea katika mpango. Nimesoma kuona kama kuna Kagera imeandikwa mahali popote pale, hakuna, labda kama itakuja kwenye bajeti ya kisekta. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaangalia matatizo makubwa. Ukosefu wa maji unasababisha magonjwa. Wanawake wanalalamika. Badala ya kujenga uchumi wao, wanashinda kwenye mahospitali. Maji yanaleta magonjwa mengi; Typhoid, Amoeba sijui na vitu gani na vitu vingine vinaitwa UTI. Kwa hiyo, unakuta watu wanahangaika, badala ya kufanya shughuli za uchumi, wanakwenda kwenye matibabu. Kwa hiyo, tunaomba hoja ya maji iwekwe kipaumbele ili tuhakikishe tunasaidia wanawake kuwatua ndoo kichwani.
Mheshimiwa Naibu Spika, niongee kidogo kuhusu kilimo. Pamoja na mambo mengi, lakini nimegundua kwamba hakuna hata wataalam wakusaidia kilimo. Kwa sababu unapolima; na binadamu sisi tuna tabia ya kufundishwa na kukumbushwa kila wakati. Kwa hiyo, hakuna wataalam, hakuna extension officers wa kilimo na hata wa mifugo. Unaweza kwenda kwenye Wilaya moja; kwa mfano Wilaya ya Muleba; mimi natoka Wilaya ya Muleba. Unaweza kukuta kuna mtu mmoja tu ambaye ni Afisa Mifugo na watu wanafuga; wana ng’ombe wa maziwa, lakini wale extension officers hawapo. Tunaomba Serikali ichukue hatua ya kuajiri extension Officers ili wakulima pamoja na kilimo chao lakini wapate utaalam wa kuwasaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho niongee kuhusu ushirika. Tunapoongea kilimo ni lazima tuangalie na namna ya kusaidia ushirika. Ushirika unasaidia wakulima. Huko nyuma ushirika ulikuwa unasaidia hata kutafuta pembejeo; mbegu, lakini pia ushirika ulikuwa unasaidia katika malipo ya wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa wakulima wa kahawa kwa mfano Mkoa wa Kagera wamepata shida sana sana ya malipo. Mtu anauza kahawa zake, anakaa miezi sita hajapewa fedha.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)