Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi ili niweze kuchangia Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa. Kwa kuanza kuchangia moja kwa moja niende kugusia upande wa upatikanaji na uongezaji wa uchumi katika Taifa letu kutokana na mpango huu na hatutoweza kukwepa suala la kuongeza uchumi wetu bila kuongelea wafanyabiashara. Suala la wafanyabiashara na Serikali, kuweka mahusiano mazuri kati ya mfanyabiashara na Serikali, lakini vile vile kuna malalamiko kati ya wafanyabiashara, haya tuweze kuyaangalia kama Serikali, kwamba mfanyabiashara anakuwa na kodi nyingi, lakini vilevile makadirio yake ni makubwa sana ambayo wakati mwingine hayana uhalisia.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, nitaenda kuongelea kwamba tunafanyeje, kwa hiyo naanza kwamba na hizo ambazo ni kama changamoto. Pamoja na hayo lakini mfanyabiashara huyu anapata changamoto nyingize za wachuuzi ambao wanafanya ujasiriamali au tunaita Machinga’s mbele ya maeneo ya wafanyabiashara hawa. Simaanishi kwamba Wamachinga au wachuuzi watolewe, lakini kuwepo na utaratibu mzuri kama Serikali kuweza kuwezesha hawa vijana ambao ni wengi wanajikita kuweka biashara barabarani kuna wengine ni akinamama wana-risk hata maisha yao kwa kukaa karibu kabisa na barabara, wakati mwingine magari yanapita na vijana wetu ambao ni wengi wameenda kujiajiri kwenye kazi ya uchuuzi ambayo ukiiangalia haina tija kwenye Taifa kwa namna nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nishauri Serikali iweze kuangalia ni namna gani tunaweza tukaboresha upande wa kilimo kama ambavyo Wabunge wengine waliopita wameongelea suala la kilimo kwa aina mbalimbali ili tuweze kuwa na kilimo ambacho kina tija na kinamnyanyua mwananchi mkulima wa chini kabisa huyu aweze kuwa na maisha mazuri. Hawa vijana wote na akinamama watatoka huku kwenye kuchuuza hizi biashara ambazo hazina tija kwa Taifa na kwenda kuwekeza kwenye kilimo ambacho kitakuwa na maslahi katika maisha hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kuna suala la hizi kodi zinakuwa ni nyingi; kuna biashara inaweza ikawa biashara moja lakini mtu ana kodi kama kumi. Ukiziangalia zile kodi zinalandana, kuna kodi ya mabango, biashara bila matangazo ambayo tunataka huyu mfanyabiashara tupate kodi kutoka kwake ni sawasawa na bure. Naongelea mabango yale mfanyabiashara anaweka kwenye duka lake au kwenye jengo lake. Yale mabango yapo upande wa TRA, kwa hilo bango mfanyabiashara anatakiwa achajiwe, bado napata shida kidogo, kama mfanyabiashara huyu anatangaza tu biashara yake labda Neema Saluni ili mtu aweze kujua mle ndani kunatolewa hiyo huduma, aingie ili kupata ile huduma nayo anatakiwa akatwe kodi. Sasa tunategemea huyu mfanyabiashara atangaze vipi ile biashara yake ili aweze kutuletea sisi kodi. Kwa hiyo kama Serikali, naomba iweze kuangalia upande huu, kuna vitu vingine ni vya kuondoa tu ili sasa huyu mfanyabiashara ajitangaze vizuri na aweze kufanya biashara yake na kodi ije kama kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile Serikali iweze kuangalia sheria za kodi ambazo pengine inakuwa ni changamoto kubwa sana kwa wafanyabishara hawa. Hata Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, shemeji yangu, naomba aweze kufuatilia Bodi ya Rufaa za Kodi ambako kule kuna malalamiko mengi ya wafanyabaishara hawa, wakiwa wanalalamika ili wakate rufaa kwa ajili ya zile kodi zimekuwa tofauti na jinsi ambavyo walitakiwa kukadiriwa. Kwa hiyo naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha aweze kwenda kuiangalia bodi hii ili aweze kujua malalamiko haya ya wafanyabiashara ni yepi ili tuone je, tunayaboresha kwa namna gani ili sasa kama Taifa tuweze kuangalia upande huo wa wafanyabiashara tunaweza tukapata vipi kuinua uchumi wetu na pato la Taifa, maana wafanyabiashara bado ni kiini kizuri katika ukuaji wa uchumi wetu. Vilevile naomba pia Serikali iweze kuangalia investors ambao ni wa nje na wa ndani, waweze kukaa kuangalia ni namna gani wataweza kuweka mazingira mazuri ili watu waweze ku-invest, watu waweze kuwekeza katika nchi yetu, kuangalia sheria kanuni na taratibu ambazo zingine zinaweza zikawa zinamfunga sana investor ambaye anashindwa ku- invest kwa kadri ambavyo alikuwa anategemea na akaamua kuondoka na tukakwama kwenye kuingiza mapato kwa ajili ya kuinua uchumi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo hivyo kama tutaweza kuruhusu wawekezaji wa nje na wa ndani tunaangalia kabisa tunaweza tukainua pato la vijana pamoja na akinamama, wakapata ajira katika makampuni ambayo yatakuwa yamefunguliwa na viwanda mbalimbali, akinamama hawa ambao wengi wanajitoa kufanya biashara za uchuuzi, wakati mwingine zinahatarisha maisha yao barabarani. Kwa hiyo, naomba Waziri wa Fedha aweze kuliangalia kwa upana huo kwa ajili ya kuweza kuinua uchumi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)