Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Hai
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, asante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa, lakini kabla ya kusema nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutupa afya na uzima. Kwa sababu ya muda nitachangia maeneo mawili tu kwenye mpango huu, nitachangia eneo la kilimo, lakini nitachangia eneo la viwanda. Na hii ni kubeba azma yetu, ndani ya Jimbo la Hai tumekubaliana kuwa na Hai mpya ya kilimo na viwanda.
Mheshimiwa Spika, Wabunge wenzangu wametangulia kueleza sana azma hii ya kuwa na kilimo cha biashara kama ambavyo imeelezwa kwenye ukurasa ule wa 65 wa mpango huu kwamba, tunadhamiria sasa kuwa na kilimo-biashara. Sasa tunazungumza sana, niombe ifike mahali sasa tuamue kwa dhati kuwekeza kwenye kilimo. Mpango huu unataja kwamba, ni eneo linalotoa ajira kwa Watanzania wengi zaidi ya asilimia 66.3 kwa hiyo, ninaomba sasa hebu tufanye kwa kudhamiria kabisa tukijua ni eneo ambalo linaenda kuokoa uchumi wetu Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na kwa kufanya hivyo niombe tuanze kwa kufanya utafiti wa tathmini ya udongo nchi nzima. Ninajua ziko taarifa hizi, lakini sio kwa maeneo yote na kwetu sisi pale Hai tuliomba taasisi ya TARI Mlingano wakatufanyia tathmini ya udongo ndani ya Jimbo la Hai. Faida ya kuwa na tathmini ya udongo kwenye eneo hili ni kuondoa changamoto wanazokutananazo wakulima.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, nitoe mfano, mkulima wa nyanya anapambana sana na ugonjwa wa kuungua kwa nyanya yake, lakini bila kujua kuungua kwa nyanya kinachosababisha ni aina ya udongo alipopanda. Pengine PH yake calcium iliyoko kwenye udongo sio rafiki kwa hiyo, tukiweza kufanya tathmini ya udongo tukatoa taarifa kwa wananchi itatusaidia sana.
Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni kuwa na mbegu ya hakika. Wananchi wanawekeza kwa nguvu kubwa sana kwenye kilimo, lakini je, tuna uhakika na mbegu wanayoipanda? Lakini pia mifumo ya kudhibiti mbegu zinazoingiziwa barabarani ikoje? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilikuwa naomba sana Waziri wa Kilimo unanisikia. Wekeni mifumo Madhubuti ya kuwa na mbegu zetu sisi zinazozalishwa hapa Tanzania ambazo ni rafiki kulingana na aina ya udongo tuliyonayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni kuwa na maji ya hakika ya kumwagilia. Mikoa mingi ukitazama, Mkoa wa Kilimanjaro, Mkoa wa Mbeya, Mkoa wa Iringa na Mikoa mingine inayofanana na hiyo ina maji ya hakika ya kumwagilia. Tatizo ni miundombinu ya kutufikishia maji kwenye mashamba yale. Kwa mfano kule kwetu Mkoa wa Kilimanjaro na hasa Jimbo la Hai, tunavyo vyanzo vya maji, mifereji mitano. Tukipata mifereji hii namhakikishia Mheshimiwa Waziri wa kilimo tunaenda kuchangia vizuri sana kwenye pato la Taifa na tunaenda kutokomeza umasikini ndani ya Jimbo la Hai.
Mheshimiwa Spika, tuna Mfereji wa Mtambo, Isimila, Kimashuku, Makeresho, Longoi, Metro, lakini pia tunalo bwawa la kihistoria ambalo limefanyiwa utafiti na wenzetu wa China, lina maji ya kutosha, Bwawa la Boluti. Kwa hiyo, nikisema pamoja na mengine kwenye mikoa mingine tuhakikishe tuna maji ya hakika na tuweke fedha nyingi kwenye bajeti inayokuja, ili wananchi walime kilimo cha biashara ambacho hakitegemei mvua kwa asilimia 100.
Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni kuwa na wataalam wa kutosha. Maeneo mengine tumeweza kupeleka watumishi wa kutosha, eneo hili la kilimo na mifugo ninaomba bajeti hii inayokuja tutenge fedha kwa ajili ya watumishi wa kutosha, ili wakatoe ushauri kule wananchi waweze kulima kilimo hiki cha biashara ambacho ndio tunalenga huko. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni kuongeza thamani ya mazao. Na hii ndio dhana yangu ya kilimo na viwanda. Eneo hili linatusababishia umasikini na wananchi kutokunufaika na mazao yao kwasababu, tunalima hatuongezi thamani. Mfano pale kwetu tunazo taarifa kwamba, wapo wakulima wafanyabiashara kutoka nje ya nchi wanakusanya mazao yetu, nyanya, mbogamboga, wanapeleka nchini kwao wanaenda kufungasha. Wakifungasha wanaturudishia sisi kununua nyanya ileile, kununua karoti ileile kwasababu tu, wameongeza thamani ya mazao.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilikuwa naomba sasa kwenye mpango huu Waziri wa viwanda tuhakikishe tunakuwa na viwanda vingi vya kuongeza thamani ili mazao yetu yaweze kuuzika ndani ya nchi na nje ya nchi yakiwa yamefungashwa vizuri.
Mheshimiwa Spika, eneo lingine tuimarishe taasisi zetu, hii taasisi ya TARI, Mlingano na taasisi nyingine zinazofanana na hivyo zijengewe uwezo. Tunao wataalamu wengi ukienda Wizara ya Kilimo pale utakuta wapo wataalamu wengi na wengi wamesoma nje ya nchi. Huko kwenye mashamba makubwa duniani wamesoma huko, lakini wamekaa ofisini pale tunataka watoke ofisini…
SPIKA: Asante sana Mheshimiwa…
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: …aai.
SPIKA: Dakika tano zimekwishapita. (Makofi)
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)