Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kuniona na nashukuru kwa kunipatia nafasi.

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza nianze kwanza kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maono mazuri na hotuba nzuri aliyoitoa ambayo imetoa matumaini makubwa sana kwa Watanzania na kuonyesha mambo mbalimbali ambayo tunatakiwa tuyasimamie katika kujenga uchumi wetu.

Mheshimiwa Spika, lakini pili nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango kwa kuja na Mpango huu wa Miaka Mitano ambao kwakweli umekuja na majibu mazuri ya mambo mengi ambayo tunayahitaji kama nchi, na hasa nimepitia yale malengo yalivyoandikwa, shahaba za utendaji tulivyoziweka, basi nafikiri ni Mpango mzuri kama tukiusimamia unaweza ukatufikisha mahali pazuri.

Mheshimiwa Spika, Mpango wowote ambao tunakuja nao lazima ujibu masuala mazito ya kitaifa ambayo tunaona kama Taifa ni changamoto; na moja ya jambo la kwanza ambalo ni changamoto sasa hivi ni umaskini ulio mkubwa kwa Watanzania walio wengi. Kwa hiyo katika mpango huu lazima tueleze namna gani tunakwenda kutatua umaskini huu ili Watanzania hawa sasa wakuwe na wawe ni wakulima wakubwa, wawe ni wafanyabiashara wazuri, wawe ni walipa kodi na ina maana tutakuwa tumeongeza idadi ya walipa kodi.

Mheshimiwa Spika, lakini jambo la pili, tunalo tatizo kubwa la kitaifa la ajira, ajira isiyo rasmi na ajira ambazo ni rasmi. Kwa Tanzania sasa hivi watu tulio wengi uchumi wetu ni uchumi ambao sio uchumi rasmi. Kama nchi hii haitupeleki pazuri. Lazima tuchukue hatua za dhati kuhakikisha tunajenga uchumi ulio rasmi ili tupate uchumi ambao ni imara na shindani.

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu ni kuangalia dhana, teknolojia na tija katika nchi yetu, hili bado ni tatizo kubwa; hatuwezi kufika bila kuchukua hatua zinazostahili. Lakini la mwisho ni uongozi bora wenye maono na Rasilimali watu; hili ni eneo ambalo ni muhimu sana. Sasa nimeangalia katika documents zote tatu zinazotakiwa ziuhishwe ili zote zijibu haya tunayoyasema.

Mheshimiwa Spika, cha kwanza ni Dira ya Taifa, dira yetu ya miaka 25 kuanzia 2000 mpaka 2025. Dira ile ina mambo matano ya muhimu ambayo tunatakiwa kuyafanya; na tutakapofika mwaka 2025, tunatakiwa twende tukapime, je Watanzania tumefikia kuwa na kipato cha dola 3000? na kama hatujafikia ni kwa nini? Hili lazima tuliangalie.

Mheshimiwa Spika, nimeangalia Ilani ya Chama cha Mapinduzi, Ilani ya Chama cha Mapinduzi ina vipaumbele sita na vimeandikwa vizuri sana. Vipaumbele vile kwasababu ya muda sitaweza kuvisema, ningetamani niviseme. Lakini unakwenda sasa kwenye mpango, mpango umekuja na vipaumbele vitano. Sasa tunaangalia ilani inasemaje, dira inasemaje na mpango unasemaje katika kutekeleza hivi vipaumbele.Nadhani tuna haja ya kuviangalia vizuri na tuhakikishe vyote vinatupeleka katika kwenda kufikia malengo tuliyokusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu walipa kodi wa kwetu wa nchi hii. Sasa hivi biashara nyingi Tanzania ni zile za wafanyabiashara wa chini na wale wa kati ndio walio wengi. Tunafanyaje sasa kuwasaidia hao wafanyabiashara wadogo wadogo? Kama vile boda boda, mama ntilie na wakulima watoke kwenye hizi biashara ndogo ndogo waende kwenye biashara kubwa ambazo wataweza hata kulipa kodi na wakachangia kwa kiwango kikubwa.

Mheshimiwa Spika, lakini la pili ni kuhusu wakulima wetu. Kilimo chetu hiki hatutaweza kutoka kama hatutaweza kuwahudumia wakulima wetu kama walivyo.

Mheshimiwa Spika, tatu wafugaji, lakini nne ni wavuvi na mwisho ni wachimba madini. Hivi vyote ni vitu muhimu sana, na ndiyo maana Ilani yetu, Mpango wetu huu wa Miaka Mitano useme ni namna gani tunaenda kufanya katika kuhakikisha sekta za uzalishaji zinaongeza uzalishaji. Mkazo katika huu mpango lazima uwe hizi sekta za uzalishaji, sekta za uzalishaji ndizo zitaleta fedha zitakazo kwenda kutumika katika sekta za huduma za jamii na mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hasa sekta za uzalishaji ziko kama hivi zifuatazo; tuna kilimo, mifungo, uvuvi, madini, Utalii na Mazingira, Viwanda na Biashara. Sasa, mpango unatuambia nini katika kufanya haya? Tumeweka mikakati gani katika namna ya kwenda kuyatumia ili haya sasa yote yatupeleke kuhakikisha kwamba ikifika 2025 tumeshaingia kuwa nchi ya kipato cha kati lakini malengo yetu ni kuhakikisha nchi inakuwa ya kipato cha kati ambapo kila Mtanzania pato la kawaida iwe ni zaidi ya dola 3000? Sasa hili ndilo lengo tulilojiwekea miaka 2000 iliyopita.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi ninataka kusema tunatengenezaje hizi ajira? Tunawaondoaje hawa Watanzania hapa tulipo? Tunajengeje viwanda? Hii ya kuandika tutaandika vizuri sana na nimeona mipango ni mizuri, lakini tunajengaje viwanda kama ajenda ya kitaifa? Tuna mfuko wa kwenda kujenga? Na kama haya yahawezekani basi maana yake hatutaweza kuja kuyafikia…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Hasunga.

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, Nakushukuru sana. (Makofi)