Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Yahaya Omary Massare

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nami nichangie mawazo kidogo katika rasimu hii ya mpango 2021/2022 – 2025/2026, hasa katika suala zima la kilimo.

Mheshimiwa Spika, wananchi wetu wanategemea sana kilimo, lakini hata makusanyo ya serikali kupitia viwanda vyetu ambavyo vinatoa kodi kubwa ambayo tunategemea kwenda kukusanya mazao, kwa maana ya malighafi itategemea kilimo.

Mheshimiwa Spika, naomba niishauri Serikali kuhusu suala la mbegu ambalo limekuwa nichangamoto kubwa na ni kubwa kweli kweli. Sisi Mkoa wa Singida ni wakulima wazuri wa alizeti, lakini mbegu nzuri ili mwananchi avune na apate kile ambacho anategemea, kulingana na mwaka mzuri wa mvua nzuri inauzwa Shilingi 35,000 kwa kilo moja. Lakini akishavuna gunia zima anauza Shilingi 60,000 na si Zaidi ya Shilingi 70,000. Maana yake ni kwamba, ataweza kununua kilo mbili kwa kuuza gunia moja ili aje alime.

Mheshimiwa Spika, Serikali iliangalie hili kwa macho mawili . Unapomuuzia mkulima mbegu kwa bei kubwa hauchechemui uchumi hasa kilimo. Sasa, ni namna gani mpango huu utaenda kuangalia, kwa hii miaka iliyobaki, kuona sasa Serikali inaweka mkono wake kwa maana ya ruzuku katika mbegu ili wananchi wanunue mbegu kwa bei nafuu, uzalishaji uwe wa kutosha na mazao yawe bora?

Mheshimiwa Spika, kuchechemua uchumi ni pamoja na miundombinu. Barabara zetu za vijijini, barabara zinazounganisha mkoa na mkoa bado kunachangamoto kubwa kabisa tunapoenda katika mpango huu wa miaka hii ya kumalizia mpango huu ambao umebaki.

Mheshimiwa Spika, sisi wa Mkoa wa Singida ni miongoni wa watu wanaosononeka kwa kutounganishwa na mikoa mingine. Ni kweli tumeunganishwa na Mikoa ya Dodoma na Tabora lakini hatujaunganishwa na Mikoa ta Mbeya na Simiyu mpaka hivi tunavyoongea. Tumeshamaliza daraja ambalo ndilo lilikuwa kikwazo, Daraja la Sibiti, na leo limemalizika, lakini hatua mipango ambayo Serikali inaenda kuchechemua uchumi kwa wananchi hawa ambao ni wazalishaji wakubwa. Hebu tuje sasa na plan ambayo barabara hizi; barabara ya Mkiwa kwenda Makongorosi ambapo barabara kubwa iliyobaki ina kilomita 412 kutoka Mkiwa mpaka ilipoishia kandarasi inapoendelea sasa. Sasa, hawa wananchi unategemea nao washindane na wenzao? Hawawezi kwa sababu mahali pa kutembea masaa matatu unatembea masaa kumi na tatu.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali ije na mpango mahsusi. Tunapokwenda kwenda na standard gauge, tunapokwenda kutengeneza Bwawa la Nyerere. Tuna vijana wasomi wanaotolewa na vyuo vikuu vyetu, sasa wanakwendaje kuingia katika ajira hasa hii ambayo tunaitegemea wakajiajiri. Kilimo ukishalima, ukishavuna unaingia barabarani unatembea masaa mengi barabarani ili ufikishe mazao hayo sokoni.

Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali yangu hii sikivu chini ya Mheshimiwa Rais mama yetu Samia Suluhu Hassan ambaye ameonesha dhamira njema kabisa kwa maneno yake na sisi Watanzania tuko nyuma yake tunaamini si miongoni wa wale watakaotia ulimi puani, kufata nyayo za aliyekuwa Rais wetu, Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa haya ambayo aliyaanzisha hasa suala zima la miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi naomba sasa mawaziri ambao wako humu wamsaidie Mheshimiwa Rais kuona zile changamoto kubwa ambazo ndio kero ya wananchi zinatatuliwa.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo yote na changamoto lakini na pongezi zipo, Serikali hii imejenga miundombinu mizuri sana hasa katika vituo vya afya, katika huduma zote za afya na elimu. Bado suala hili tu, kidogo maji, lakini na miundombinu ya barabara zinazounganisha mikoa na mikoa. pia barabara zetu za vijijini ni za kutolea macho mawili. Kama Waheshimiwa Wabunge wengi walivyoshauri namna ya kuiongezea TARURA pesa; ni namna gani tuongeze na ni wapi muangalie ambako hakuna shida, wengine wameshauri kwenye mafuta. Busara itumike na TARURA waongezewe pesa ili barabara nyingi za vijijini ziweze kufanya kazi vizuri…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Massare.

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana naunga mkono hoja.