Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Manyoni Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii nikushukuru sana kwa nafasi uliyonipatia. Pia nimshukuru sana Dkt. Mwigulu pamoja na timu yake kwa kuja na huu Mpango mzuri sana. Mapendekezo yangu yatajikita kwenye usimamizi wa miradi ya kimkakati. Wewe mwenyewe unatambua kwamba tumefanya mambo makubwa sana katika nchi hii katika miradi ya kimkakati ukiwepo ununuzi wa ndege zaidi ya 10, ujenzi wa reli ya kisasa, lakini vile vile tunategemea kuanza ujenzi wa bandari mbalimbali hapa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, hapa Dodoma tumekuwa na miradi ya kimkakati mingi sana. Hivi karibuni wenzetu wa Jiji la Dodoma wamemaliza ujenzi wa hoteli kubwa sana ambayo itakuwa five star haya yote ni maendeleo makubwa sana ambayo yameletwa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi. Sasa hoja yangu ni kwamba, katika hii miradi ya kimkakati ambayo ni uwekezaji mzuri sana kwa nchi yetu, lakini nalitazama katika upande wa usimamizi. Kwa sabbau tayari tuna sera ya Public Private Partnership, Sera ya Ubia kati ya Serikali pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo hususan Private Sector, lakini tuna sheria ya ubia kati ya Public Sector and Private Sector. Nadhani ni muda muafaka sasa sisi kama Serikali tuangalie jinsi gani tunaenda ku-capitalize kwenye hii sera ili tuweze kuisadia Serikali.
Mheshimiwa Spika, nataka kushauri kwa mfano, tuna mradi mkubwa hapa Dodoma wa hoteli, hoteli ya five star, je, tunaenda kutumia business modal gani kuhakikisha kwamba ile hoteli inaenda kufanya kazi vizuri. Kwa nini tusiingie kwenye huu ubia sasa wa Private Sector na Public Sector tukaangalia ni maeneo gani ambayo Private Sector wana uwezo nayo tukawaachia, halafu yale maeneo ambayo sisi tuna uwezo nayo tukayafanyia kazi. Hilo ni la kwanza ningependa kuishauri Serikali.
Mheshimiwa Spika, lingine, tuna miradi mingine ambayo ni mikubwa tunaifanya. Sasa hivi tunasisitiza suala la Public Private Partnership, naomba nimshauri Waziri kwa nini wasiunde task force ikaenda kupitia miradi yetu yote ile mikubwa wakaja kuishauri Serikali kuja na business modal ya jinsi gani tunaweza ku-manage hii miradi. Kwa nini tusiende kwenye ile management contract kwamba eneo ambalo Serikali tuna uwezo nalo tutalifanyia kazi, lakini yale maeneo ambayo Serikali hatuna uwezo nayo, nashauri tunahitaji kuchukua maamuzi magumu ili kuhakikisha kwamba Private Sector na yenyewe ili iweze kukua tunahitaji kuigawia sehemu ya ile miradi ili waweze kuisimamia. Kuna faida nyingi katika hili.
Mheshimiwa Spika, kwanza, tunaenda kukuza ajira; Pili, tunaenda kukuza mahusiano kati ya Public Sector na Private Sector; na Tatu, itatufanya sisi tulale. Badala ya Waziri wa Fedha kulala anawaza kwamba sijui mradi huu haufanyi vizuri, una-transfer risk, unampelekea mtu mwingine, kazi yetu inabaki kukusanya kodi lakini vile vile kuangalia gawio letu mwisho wa mwezi.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii, naomba kwamba Serikali ichukue haya maoni yangu na iyafanyie kazi. Ahsante sana. (Makofi)