Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilombero
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kupata nafasi hii kama ya bahati nasibu kuchangia mpango wetu ambao lengo la mpango huu ni kuwa na uchumi wa viwanda ambao unaenda sambamba na kilimo. Na unavyosema kilimo katika nchi yetu huwezi kuacha mikoa mikubwa ile ambayo inajishughulisha na kilimo na mkoa mmojawapo ni Mkoa wa Morogoro ambao unashikilia takribani asilimia 7.7 ya ardhi ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, sasa sisi kwa kifupi kabisa tunaomba Mheshimiwa Waziri kwamba, katika mkoa tulikaa tuna mpango mkakati wa maendeleo ya kilimo, mifugo na uvuvi Mkoa wa Morogoro. Kitabu hiki kina kila kitu, kimeelezea fursa mbalimbali ambazo zitasaidia sana Mheshimiwa Waziri kufika katika malengo yake ya mpango. Na tumesema fursa zilizopo katika mpango huu tukiunganisha mpango na kitabu ambacho mwaka 2020 tulikiombea kura kwa wananchi, yaani Ilani ya Uchaguzi.
Mheshimiwa Spika, kama kweli tunataka mpango huu ufanikiwe katika kupanga ni kuchagua mara zote nimegusa kwa mfano suala la kilimo cha miwa tu peke yake. Nimesema kuna miwa Kilombero tani takribani 300,000 zinalala zinasalia na ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Baba yangu Profesa Mkenda, tuliendanaye ameona hali halisi. Wawekezaji wale katika Kiwanda cha Ilovu cha Kilombero cha sukari kwa mfano kwa sasahivi wanatafuta takribani bilioni 400 kukuza, kupanua kile kiwanda kiweze kuchukua miwa ile tani 300,000 ambayo miwa hiyo tani 300,000 ikichakatwa itazalisha tani elfu 30 mpaka 35 za sukari.
Mheshimiwa Spika, nchi yetu leo inaingiza tani 40,000 za sukari, tukiweza kuchakata miwa ile ambayo ipo yani sidhani kama kuna mpango ambao unaweza kwenda kutuelekeza sehemu nyingine kwenda kupanda miwa, kuanzisha mradi mpya, lakini huku kuna watu akina Balozi Mpungu Mwenyekiti wa Bodi wanatafuta bilioni 400, bilioni 500 wapanue kiwanda kitumie miwa ambayo tayari ipo ya wananchi na nchi yetu isiingize tena sukari. Maana hapa keshokutwa tunaenda kwenye uhaba wa sukari watu wataanza kuingiza sukari, tunaingiza tani 40,000 wakati miwa inabaki tani 300,000. Kwa hiyo, nisisitize tu Mkoa wa Morogoro una fursa nyingi. Kwenye kitabu humu tumesema kuna mashamba 12 makubwa. Tunahitaji bilioni 100 tu kwa mwaka huu akitutafutia Mheshimiwa Waziri tuta-push mpango wetu.
Mheshimiwa Spika, tuna hekta zinazofaa kwa kilimo milioni 2.2 tunatumia asilimia 43 tu, 900,000 ndio tunazolima. Tuna hekta zinazofaa kwa umwagiliaji 323,000 zinafaa kwa umwagiliaji tunalima 28,000. Sasa kam kweli tuna mpango tunataka ku-boost uchumi wetu wa nchi yetu na tunasema uchumi wa viwanda tunauunganisha na kilimo basi Mkoa wa Morogoro utazamwe, Wizara na wasimamizi wote wa sera watusaidie kupata fedha kuongezea halmashauri zetu fedha ili tuweze ku-deal na kilimo.
Mheshimiwa Spika, nimesema kwenye miwa, kuna mpunga, amesema hapa brother wangu, pacha wangu Mheshimiwa Kunambi. Upande wake sasa hivi jeshi linatengeneza mradi mkubwa sana wa umwagiliaji. Kwa hiyo, kwa nafasi hii nilikuwa naomba baadaye nitamkabidhi kwa sababu, dakika ni chache, nitamkabidhi Mheshimiwa Waziri kitabu hiki atusaidie.
Mheshimiwa Spika, mwisho kuna miradi mkakati, sisi Halmashauri yetu ya Mji wa Ifakara ime-qualify na tumeomba takribani miaka miwili mitatu iliyopita kwamba, kama malengo mojawapo ni halmashauri zijitegemee, sisi tume- qualify kupata soko pale Mjini Ifaraka ni mji mkubwa sana. Kwamba, soko lile tukipewa zile fedha tulizoomba takribani bilioni tano zitarejeshwa ndani ya miaka mitano na halmashauri yetu itapata mapato makubwa. Tunaomba hilo Mheshimiwa Waziri nalo alifikirie.
Mheshimiwa Spika, la pili. 2018 Mheshimiwa Rais, Hayati, alivyokuja kule kuna kiwanda kikubwa kilikuwa cha chuma, cha vifaa vya reli kina hekta 250-kina majengo, ma- hall kabisa na mashine zipo ndani yake. Tangu kimerudishwa kile kiwanda kipo idle.
SPIKA: Kiwanda cha Mang’ula?
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, cha Mang’ula cha chuma kimekuwa pori. Kuna wawekezaji wamepatikana huko nimemwambia Waziri wangu Mheshimiwa Profesa Mkenda amenisaidia kuna baadhi amewaona, Mheshimiwa Profesa Mkumbo pia, tuwasaidie tuwaruhusu kama wako tayari kuwekeza hata wakiwekeza kiwanda kidogo cha miwa watatumia hiyo miwa tani laki tatu.
SPIKA: Ahsante sana.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)