Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Ummy Ally Mwalimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili na mimi niweze kuchangia Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama na kuongea katika Bunge lako la Kumi na Mbili, nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehma lakini wapiga kura wa Tanga Mjini kwa kunirudisha Bungeni. Nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini kwamba naweza kumsaidia kusimamia na kuratibu shughuli za utawala na maendeleo katika Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nimpongeze Waziri wa Fedha, ndugu yetu Mheshimiwa Mwigulu kwa kuwasilisha Mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano. Katika hatua hii, niwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa maoni na ushauri kwa sababu nimeona Waheshimiwa Wabunge wengi pia wamechangia moja ya vipaumbele vitano vya Mpango wa Taifa wa Maendeleo ambao ni kuchochea maendeleo ya watu. Katika maoni ya Waheshimiwa Wabunge, niseme kwamba tumepokea na ufafanuzi mkubwa au zaidi tutautoa tarehe 19 - 21 wakati tutakapowasilisha bajeti ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niruhusu niguse maeneo makubwa matatu au manne. Eneo ambalo Waheshimiwa Wabunge wameliongelea ni kuboresha miundombinu ya elimu ya msingi na sekondari. Tunakubaliana na nyie kwamba bado tuna uhaba wa vyumba vya madarasa, madawati, maabara za sayansi pamoja na nyumba za walimu katika Halmashauri zetu, katika Majimbo yetu lakini pia ni lazima tukubali kwamba kazi kubwa na nzuri imefanyika katika kipindi cha mwaka uliopita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwaeleze tu Waheshimiwa Wabunge kwamba katika bajeti yetu 2021/ 2022, tunatarajia kuendeleza ujenzi wa madarasa ikiwemo kukamilisha maboma ya vyumba vya madarasa 2,695. Pia tutajenga maabara za sayansi takribani 1,280. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, aidha, tumefanya tathmini na hili ni juzi tu, ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia kwamba hataki kuona mtoto wa Kitanzania akisoma chini ya mti akifundishwa katika shule yenye mwalimu mmoja au shule yenye walimu wawili. Kwa hiyo, tumefanya tathmini tuna upungufu wa madawati takribani 1,048,000. Katika bajeti yetu inayokuja tumepanga kununua au kutengeneza madawati 710,000 ili kuweza kutatua changamoto hii ya madawati. Pia tumeona tusiwaache walimu, ni lazima tujenge nyumba za walimu hususani katika maeneo ya pembezoni au maeneo ambayo yapo kidogo mbali na miji mikuu. Kwa hiyo, katika bajeti pia tutajenga nyumba 100 za walimu ili kuhakikisha kwamba tunaweka mazingira mazuri kwa walimu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda naomba nisema kwamba tukijadili bajeti yetu tutaeleza mambo gani makubwa ambayo tutayafanya katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia watoto wetu. Kubwa ni commitment ya Serikali kuhakikisha tunatoa elimu bora na sio bora elimu kwa watoto wa kitanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la pili ni watumishi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na Mikoa ikiwemo changamoto ya uhamisho wa walimu. Katika hili, nakubaliana na Waheshimiwa Wabunge, kila mtumishi wa Halmashauri anataka kwenda kufanya kazi Halmashauri za Mijini, nani atafanya kazi katika Halmashauri za Vijijini au za pembezoni? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunafahamu mwalimu au muuguzi au daktari anayo haki ya kuhama kama mtumishi mwingine wa umma, lakini lazima tuangalie kule vijijini na pembezoni nani anaenda kufanya kazi. Kwa hiyo, hili tumelipokea kwamba Waheshimiwa Wabunge wamelitolea maoni, tutahakikisha kwamba tuna-review case by case lakini tutatoa mwongozo mahsusi kwa ajili ya ku-make sure walimu wanapenda kufanya kazi katika Halmashauri za pembezoni. Kubwa ni kuhakikisha kwamba tunakuwa na incentive kwa walimu na watumishi wa afya ambao wanafanya kazi katika Halmashauri za pembezoni, kwa hiyo hili tutaliangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni uboreshaji wa huduma za afya ya msingi. Kwenye hili tunapokea maoni na ushauri wa Wabunge kuhusu utolewaji wa huduma. Tunakubaliana na Waheshimiwa Wabunge kwamba bado tuna uhaba wa zahanati, vituo vya afya, pamoja na Hospitali za Halmashauri. Sasa hivi tumeamua kushusha badala ya kuwa Hospitali za Wilaya tunaenda kuwa ni Hospitali za Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, kipaumbele chetu cha kwanza katika kuboresha huduma za afya ya msingi, tunaangalia utoaji wa huduma katika ngazi ya zahanati, kituo cha afya pamoja na ngazi ya Hospitali ya Halmashauri. Kwa hiyo haya mambo tarehe 19 mtakuja kuyaona katika bajeti yetu.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine, nafahamu Wabunge wengi wanataka tujenge zahanati na vituo vya afya, tunaona tujikite kwanza kumaliza zahanati na vituo vya afya ambavyo vimejengwa na havijakamilika. Tumeonyesha katika bajeti yetu tuna vituo vya afya 52 ambavyo tunatakiwa kuvikamilisha lakini pia tuna hospitali za Halmashauri 68 ikiwemo kuhakikisha tunaviwekea vifaa tiba na vifaa pamoja na upatikanaji wa dawa na watumishi ili huduma bora za afya ya msingi ziweze kutolewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumepokea ushauri wa kuboresha huduma katika ngazi ya msingi especially huduma za kinga. Hili tumelipokea, ni kweli tukiweza kuzuia wananchi wengi wakawa wana afya bora kabla hawajaenda katika ngazi ya rufaa maana yake pia tutaokoa fedha nyingi za Serikali.

Mheshimiwa Spika, katika suala la afya pia katika bajeti inayokuja Mheshimiwa Rais Samia amenielekeza, haikuwepo kwenye bajeti hii, lakini sasa ametafuta rasilimali fedha, Halmashauri zote 24 ambazo hazina Hospitali za Halmashauri tunaenda kujenga Hospitali za Halmashauri katika Halmashauri hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, muda umeisha lakini nataka kusema suala la TARURA tumelipokea ikiwemo kuongeza bajeti ya TARURA. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana na mimi naunga mkono hoja. (Makofi)