Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kikwajuni
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, naomba nitumie nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima na afya, lakini nitumie fursa hii kwa mara nyingine tena Mheshimiwa mama Samia Suluhu Hassan kwa imani yake kwangu kwa kunichagua kuwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nijikite katika hoja kama mbili ambazo WaheshimiwaWabunge wamezizungumzia katika Bunge lako Tukufu kwenye mchango wa mjadala wa Mpango.
Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza ambalo ninataka kulizungumzia ni kuhusu maoni ya baadhi ya Waheshimiwa Wabunge kuhusu jinsi gani ambavyo kasi ya ukuaji wa uchumi wetu haiakisi hali halisi ya maisha ya wnanachi wa nchi hii.
Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa utangulizi kwa kunukuu equation moja ya uchumi ambayo inasema Y=C+I+G+X-M. Ukiangalia equation hii inaweza ikatoa tafsiri nyingi lakini kwa haraka haraka na kwa sababu ya muda nimezichukua kama tafsiri tatu. Ta kwanza inaonesha kwamba kipato na matumizi ni vitu ambavyo vinakwenda sambamba. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mfano leo hii mtu ambaye anafanya biashara anashindwa kupata sehemu nzuri ya kuweka biashara zake na mtu ambaye anaishi katika mazingira duni akiweza kupata uwezo wa kujenga nyumba bora, akiweza kupata uwezo labda wa kukodi sehemu nzuri ya kufanya biashara zake zikawa rasmi zaidi, maana yake ni nini; maana yake ni kwamba ameweza kuboresha maisha yake na hivyo basi kipato chake kimeongezeka.
Mheshimiwa Spika, leo hii tafsiri nyingine ambayo tunaweza tukaiona moja kwa moja hapa ni kwamba uwekezaji wetu katika nchi hii unakwenda sambamba pamoja na kipato chetu. Sekta hii ya uwekezaji na kipato huwa ni muhimu katika msingi wa kuongeza kipato. Ni jambo ambalo haliepukiki na ndiyo maana leo hii tukiangalia sekta ambazo zinaajiri watu wengi kabisa ni kwenye uwekezaji. Hivyo basi, itasaidia kuweza kufanya viwanda vyetu vihamasike, hasa viwanda vile ambavyo vinatumia rasilimali za kilimo, mifugo na uvuvi.
Mheshimiwa Spika, tafsiri nyingine ya mwisho ambayo nimeipata katika equation hii ni kwamba mwelekeo wa matumizi ya Serikali yanachangia vilevile kipato cha wnanachi. Kwa mfano leo Serikali ikiamua kuwekeza katika umeme vijijini au katika miradi ya maji wakandarasi wa ndani wanapata uwezo na wanaweza kuajiri watu wengine na fedha inazunguka.
Mheshimiwa Spika, hoja ya msingi ambayo iko Mezani ni kwamba je, ni kwa kiasi gani mpango wetu huu wa miaka mitano umeweza kuzingatia tafsiri hizi tatu. Wakati huohuo tukiendelea kuhakikisha kwamba tunadhibiti mfumuko wetu wa bei, lakini wakati huohuo tunaendelea kudhibiti fedha haramu isiweze kuzunguka katika uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia mpango wetu una maeneo makubwa matano. Eneo la kwanza linazungumzia kuhusu kuchochea uchumi shindani na shirikishi. Lingine linazungumzia kuimarisha uzalishaji viwandani, kukuza biashara na uwekezaji, kuchochea maendeleo ya watu pamoja na kuendeleza rasilimali watu. Maeneo haya matano ukiangalia kimsingi na ukiangalia nafasi ya sekta binafsi katika kushiriki katika kufanikisha malengo haya ni jambo ambalo haliepukiki. Iwe sekta binafsi kupitia uwekezaji wa ndani, iwe sekta binagfsi kupitia uwekezaji wa nje ambao watatuletea Foreign Direct Investment, iwe uwekezaji wa ubia katika sekta binafsi na sekta ya Umma.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nitumie fursa hii sasa kueleza kwa kifupi kwamba ni kwa vipi Mpango wetu wa Miaka Mitano tumejikita katika kuhakikisha kwamba tunaisaidia sekta binafsi ili iweze kushiriki kikamilifu katika uchumi wa nchi hii pamoja na kuhakikisha kwamba inasaidia kuongeza mzunguko wa fedha katika jamii.
Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza ambalo ni la msingi ni kwamba tutahakikisha tunafanya maboresho ya kisera, kisheria, kitaasisi na kimfumo pale itakapohitajika ili kuondoa vikwazo na kuvutia uwekezaji ikiwemo kwenye masuala ya kodi ili kuimarisha weledi na ufanisi katika kukusanya kodi na kudhibiti ukwepaji kodi bila kutumia mabavu yasiyostahiki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili; tutaendelea kupanua wigo wa vyanzo vya kodi na wigo wa walipa kodi. Sasa hivi nchi yetu ambayo ina takribani watu milioni 55 ukiangalia tax base yake ya watu wenye TIN Number hawazidi watu milioni nne. Kwa hiyo, jambo hili ni jambo ambalo ni la msingi kabisa kuliangalia katika miaka mitano ambayo tunakuja.
Mheshimiwa Spika, tutahakikisha tunakamilisha miradi yote ya kimkakati ikiwemo mradi wa umeme kama alivyozungumza Mheshimiwa Waziri wa Nishati akiwa anamalizia hoja yake kwa Mwalimu Nyerere. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo amezungumza Mheshimiwa Waziri wa Nishati, kwamba suluhisho la kuweza kuhakikisha kwamba tunapata umeme wa uhakika na umeme wa bei nafuu ili viwanda vyetu viweze kupunguza gharama ya uzalishaji, ni kwa kutumia vyanzo mchanganyiko. Kwa hiyo, vyanzo vyote ambavyo vimeainishwa katika mpango huu, ikiwemo vyanzo vya makaa ya mawe, vyanzo vya gesi, vyanzo vya hydro na kadhalika, vitatumika.
Mheshimiwa Spika, lingine ni kujenga mazingira wezeshi kwa wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa ili waweze kurasimisha biashara zao na kukuza mitaji yao, uwezo wao, ujuzi wao pamoja na uzoefu wao.
Mheshimiwa Spika, jambo la tano ni kuongeza matumizi ya maarifa na ujuzi wa teknolojia madhubuti katika sekta ikiwemo sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi na shughuli mbalimbali zinazojihusisha na usindikaji wa bidhaa nchini ili kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja.
Mheshimiwa Spika, tutahakikisha kwamba tunajenga mazingira mazuri kwa sekta binafsi kuendelea kuendesha shughuli za uzalishaji na uuzaji nje wa bidhaa za kilimo, mifugo na uvuvi zilizochakatwa.
Mheshimiwa Spika, mikakati hii yote ambayo nimeieleza ambayo iko kwenye mpango huu…
SPIKA: Ahsante sana. Malizia kwa dakika moja.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: …wa miaka mitano inahakikisha kama nilivyozungumza, kuhakikisha kwamba uchumi wetu unakua, nchi yetu inapiga hatua kimaendeleo lakini wakati huohuo tunaimarisha upatikanaji na mzunguko wa fedha katika jamii yetu.
Mheshimiwa Spika, baada ya hayo machache, naunga mkono hoja. (Makofi)