Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Livingstone Joseph Lusinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtera

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kupata nafasi hii ya kufungua dimba. Namshukuru sana Mungu kwa ajili ya vipawa na vipaji vingi alivyotujalia. Awali ya yote, nitoe pole kwa familia ya Mheshimiwa Hayati Dkt. Magufuli, Mama Janeth pamoja na Watoto; Joseph, Michael pamoja na Jesca. Tunawapa pole sana. Vile vile tumpe pole Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli tukupe pole na wewe kwa sababu ulishindwa hata kuchukua hela yako ya utani kwa namna ambavyo ulikuwa umeguswa, maana yule ni mtani wako, ulitakiwa pale uzuie shughuli zisiendelee mpaka upewe chochote; lakini kwa sababu alikuwa mtu wako wa karibu ukashindwa kufanya hata utani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa ya kusimamia msiba wa Kitaifa. Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Waziri Jenista Mhagama na timu yako akiwepo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, tumeona namna ambavyo Kamati yenu imefanya kazi kubwa sana; na kwa kweli tutakuwa wachoyo wa fadhila tusipokushukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kusimamia msiba ule ambao umetupa heshima kubwa kama Taifa kwa namna ambavyo tumemzika Kiongozi wetu kwa heshima kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tutoe pole kwa yule Bwana aliyepoteza mke na watoto pale Dar es Salaam kwa kukanyagwa kwa ajili ya wingi wa watu waliofika kushuhudia msiba ule. Tunawapa pole sana Watanzania wote kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu imejaa mambo mengi. Imesheheni vitu vikubwa sana, imesheheni tulikotoka, tuliko na tunakokwenda na hatuna mashaka kwa usimamizi thabiti wa Rais aliyepo sasa Mheshimiwa Samia pamoja na timu aliyoipanga kwamba mambo haya yanakwenda kufanyika. Kazi tuliyonayo, Bunge lako ni kuendelea kuwashauri, kuwatia moyo na kuwaunga mkono kuhakikisha kwamba haya yaliyokusudiwa yanafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, rai yangu ni kwamba, tungetengeneza vijitabu vichache, siyo Ilani mpya, lakini vya kukumbusha zile ahadi za Waheshimiwa Viongozi walikopita. Ziwe katika kitabu kimoja cha Kitaifa, alikopita Mheshimiwa Mama Samia aliahidi, alikopita Mheshimiwa Hayati Dkt. Magufuli aliahidi, sasa badala ya kila Mbunge kuwa anasimama anakumbusha ahadi ya Rais, ni vyema zikawekwa kwenye kitabu kimoja tukajua kwamba, ahadi za Viongozi wa Kitaifa ni hizi. Kuna mahali waliahidi barabara kama Mvumi pale, kuna mahali waliahidi madaraja, kuna mahali waliahidi kuchimba mabwawa; tukifanya hivyo, tutarahisisha Wabunge wote kwa pamoja tutakuwa tunadai tu ahadi za viongozi zitekelezwe ambazo ziko kwenye kitabu kimoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikishukuru Chama cha Mapinduzi, kimefanya kazi kubwa sana kwenye uchaguzi uliopita. Hiki Chama hakina mashaka kwamba ndiyo chama pekee kilichobaki kwenye eneo la ukanda huu kinachotetea maslahi mapana ya wananchi wa nchi yake. Kwa kweli bila uchoyo, nataka nimshukuru sana Katibu Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Bashiru, tunakushukuru sana kwa kazi kubwa ambayo uliifanya. Jamani mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, jambo kubwa ambalo Mheshimiwa Waziri Mkuu amelisema hapa ni kuhakikisha kwamba Serikali inaendelea kusimamia amani na utulivu wa nchi yetu. Amani na utulivu haviwezi kuwepo kama kuna baadhi ya Watanzania na baadhi ya Wabunge wanamsema vibaya Hayati Mheshimiwa Dkt. Magufuli, haiwezi kuwepo amani na utulivu. Haiwezekani! Kwa hiyo, leo nataka kujitoa muhanga hapa. Haiwezekani tuwe na viongozi ambao wanajaribu kupinga mambo mazuri aliyoyafanya Hayati Mheshimiwa Dkt. Magufuli, haiwezekani. Hatuwezi kuwavumilia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hawa wanaomsema vibaya leo Hayati Mheshimiwa Dkt. Magufuli, watamsema vibaya Mheshimiwa Samia. Hii ni tabia! Jamani Hayati Mheshimiwa Dkt. Magufuli amefanya kazi kubwa sana kwenye nchi hii. Maana lazima tukubaliane, unajua kuna wengine wanafikiri labda Mheshimiwa Samia alikuwa bench akaingia kucheza mpira, hapana. Mheshimiwa Samia alikuwa anacheza pamoja na Hayati Mheshimiwa Dkt. Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, aliyemtaja Mheshimiwa Samia ni Hayati Mheshimiwa Dkt. Magufuli mwenyewe. Siku zote Hayati Mheshimiwa Dkt. Magufuli amekuwa akisema, kama akijitabiria kifo chake; kila hotuba yake alikuwa akisema siku moja nitakufa. Kwa hiyo, alikuwa anajua, akiondoka yuko Mheshimiwa Samia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunataka watu wamheshimu. Huwezi kuondoa legacy ya Hayati Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwenye nchi hii na kwenye Bara la Afrika, haiwezekani. Haiwezekani, haiwezekani! Hatuwezi kuwavumilia watu wa namna hiyo. Nasi kama viongozi ambao tumelelewa, hivi leo Mbunge gani hapa hakutetewa na Hayati Mheshimiwa Dkt. Magufuli? Tuko humu ndani kwa sababu ya Hayati Mheshimiwa Dkt. Magufuli na Mheshimiwa Samia. Kila sehemu walipita.

Mheshimiwa Spika, kuna watu hapa walikuwa hata hawachaguliki, Hayati Mheshimiwa Dkt. Magufuli na Mheshimiwa Samia wakipita wanasema, tupeni huyu, tutafanya naye kazi, tutamrekebisha. Kwa sababu yao, watu wakachaguliwa. Leo wasemwe vibaya sisi tupo! Leo Hayati Mheshimiwa Dkt. Magufuli asemwe vibaya hata arobaini haijaisha! Hili jambo halikubaliki. Hawa watu washike adabu na adabu ziwashike, hatutaki warudie tena mambo ya kipuuzi kama haya. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, anasimama mtu anasema eti mradi ule wa maji tuuache! Unajua mimi nina hakika kwamba, hata mle ndani inawezekana hata kaburi la Hayati Mheshimiwa Dkt. Magufuli lilitikisika! Tuuache mradi ule wa Mwalimu Nyerere? Ule mradi una faida kibao! Pale ametuambia hapa Mheshimiwa Majaliwa kwamba tumetumbukiza shilingi trilioni mbili; tuziache ziteketee? Kwa sababu gani? Ule mradi kwa taarifa yenu, mimi sio Profesa Professor, mimi ni wa Darasa la Saba, lakini ngoja niwape faida za ziada za ule mradi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, ngojeni niwape faida za ziada za ule mradi. Lile bwawa linalochimbwa pale, upana wake peke yake ni kilometa 25, lakini urefu wa maji yatakayokuwa pale ni kilometa 100; hapa na Kibaigwa. Hilo ni bwawa au ziwa? Pale linazaliwa ziwa! Hii nchi itabidi wachoraji wa ramani mbadilishe, msitaje maziwa yale tuliyonayo, mwongeze na Ziwa la Magufuli linalozaliwa pale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye lile ziwa, pembeni kutajengwa hoteli za utalii, pale patawekwa samaki watu watavua, lakini ziwa lile linagusa Wilaya tano. Hivi jamani elimu ya Tanzania kweli inatusaidia? Kama wa Darasa la Saba naelewa, halafu Profesa huelewi, inakuwaje? Inakuwaje? Inakuwaje? (Makofi/Kicheko/Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, haiwezekani, ni lazima tusome na vile vile tuwaeleze watu vitu vya kweli. Tusiwadanganye wananchi. Amesema hapa Mheshimiwa Waziri Kalemani, umeme wa maji ndiyo umeme wa bei rahisi kuliko umeme wowote. Kwa nini tunawadanganya Watanzania? Kama tuna madili yetu tuyaeleze, lakini tusiingize kuanza kuharibu image ya Hayati Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwa wananchi wakati tegemeo lao kubwa ni Mheshimiwa Samia kutekeleza mambo waliyoyapanga na ndugu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kila sehemu watu wana matumaini makubwa sana na Mheshimiwa Rais Samia. Kazi yetu sisi Wabunge ni kumtia moyo, siyo kuanza kumrudisha nyuma, siyo kuanza kuzungumza kana kwamba Mheshimiwa Samia ni mtu mwingine na Hayati Mheshimiwa Dkt. Magufuli ni mtu mwingine, haiwezekani. Haiwezekani! Haiwezekani! Nasi Wabunge tuko humu, haiwezekani!

Mheshimiwa Spika, Samia ni Magufuli na Magufuli ni Samia. Wamefanya kazi kubwa na sasa Samia anaelekea kwenda kuitendea Tanzania jambo la ajabu, kukamilisha ile miradi waliyokubaliana na Hayati Mheshimiwa Dkt. Magufuli na siyo hivyo tu, na kuongeza mingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi hii Rais anayetawala, anatekeleza Ilani na vile vile anakuja na maono yake. Tusianze kumtangulia Rais. Rais ana maono yake. Mnaposikia huko watu wanafanya Ibada Makanisani na Misikitini wanamwombea, pale busara zinaongezeka, anawaza mambo mengine makubwa ya kuitendea nchi. Nani asiyejua kwamba ziwa la mama ndiyo linalolea mtoto? Sisi tuna Imani kubwa na Rais aliyepo, kwa hiyo, tusianze kumzongazonga na kuanza kumfananisha sijui Magufuli na Samia, sijui Samia bora kuliko Magufuli, inatoka wapi hiyo? Hawa wote ni kitu kimoja, wamechezea timu moja, wote wamezaliwa na Chama cha Mapinduzi. Huyu ni kada wa Chama chetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, nimesema mimi najitoa muhanga eti kwa sababu nagombea NEC, sijui mtaninyima kura. Mkininyima hiari yenu, lakini leo napasuka hapa. (Makofi/Kicheko)

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge! (Kicheko)

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika,…

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge wa CCM, naomba kuwahoji, Mheshimiwa Lusinde amepita NEC? (Kicheko/ Makofi)

WABUNGE FULANI: Amepita! (Kicheko/Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa umepita bwana. (Makofi/ Kicheko)

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, watu wengi wanataka kuliharibu suala ambalo umelisema. Suala la ujenzi wa bandari, Hayati Mheshimiwa Dkt. Magufuli alieleza mabaya yaliyoko kwenye mkataba. Kazi tuliyonayo sisi ambao tumebaki hai, kama upo uwezekano, tufanye mapitio upya ya ule mkataba. Wewe hujasema ijengwe kama ilivyo; na ulikuwa msimamo wako wa siku zote hata Hayati Mheshimiwa Dkt. Magufuli akiwepo. (Makofi)

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, ngoja nataka niseme hapo.

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Haya, Mheshimiwa Kingu.

T A A R I F A

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Nataka nimpe taarifa mzungumzaji anayesema kwamba hata watu ambao wanaendelea kumshambulia na kutaka kumchafua Spika wetu kuhusiana na Mradi wa Bagamoyo ni vile hawajui kwamba alichokuwa amekisema Spika hata kwenye Bunge la mwaka 2020 alikuwa amemaanisha kwamba kama kuna upungufu kwenye mradi wa Bagamoyo, kama nchi tuyatoe na mazuri tuyapokee, tuendeleze mradi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninatoa rai kwamba sisi kama Bunge, nampa taarifa msemaji, tusikubali kuona image yoyote ya kutaka kumdhalilisha Spika wetu kwenye hilo jambo.

Mheshimiwa Spika, nina imani kaka yangu ataipokea taarifa yangu. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Lusinde, unaipokea taarifa?

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa ya Kingu. Hauwezi ukachoma nyumba moto kwa sababu ndani ya nyumba kumeingia panya, haiwezekani. Tunachofanya pale, yale maovu tunayaondoa, kinachobaki kinaletwa hapa Bungeni, wananchi wanaelimishwa kwamba ubora wa bandari ya Bagamoyo ni huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hakuna kitu chochote kilichokosewa. Nimesimama hapa kufungua dimba…

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Taarifa ya Mheshimiwa Musukuma.

T A A R I F A

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Napenda kumpa taarifa tu mzungumzaji kwamba, mawazo yanayotolewa na Senior Lusinde, Darasa la Saba ni mawazo… (Kicheko)

Waheshimiwa Wabunge, msicheke, ni mawazo ambayo kama alivyosema, humu ndani kuna watu watu ni Maprofesa na ma-Ph.D yenu hamna hayo mawazo.

Mheshimiwa Spika, sasa kiti chako, haya mawazo tukiwa tunayaacha yanapoteapotea, hayawezi kuwa na kumbukumbu kwenye Taifa letu. Unaonaje watu kama hawa ukawatunukia hata Udaktari wa heshima ili hata... (Makofi/ Kicheko)

SPIKA: Mheshimiwa Lusinde, unapokea taarifa?

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, napokea kwa mikono miwili kwa sababu mtathmini naye ana elimu kama yangu. Kwa hiyo, napokea taarifa. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nataka nipige mabomu ya ndani na ya masafa marefu. Kabla ya uchaguzi uliopita, tuliwaasa baadhi ya viongozi, tujenge tabia ya ustaarabu; ukiongoza chama, ukiongoza timu ya mpira, tusishindwe na makocha? Juzi tumemwona Kocha wa Timu ya Taifa Etienne Ndayiragija; timu imefungwa, kajiuzulu katoka.

Mheshimiwa Spika, tunashangaa wako wanasiasa ving’ang’anizi; kaongoza chama, kilikuwa na Wabunge 100, sasa hivi kina Mbunge mmoja; bado naye anasimma kuzungumza eti Mwenyekiti wa chama. Mwenyekiti wa chama gani? Unasema vitu vya uongo, eti akaunti yangu ilifungwa. Hayati Mheshimiwa Dkt. Magufuli alikuwa anafanya kazi BoT? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, Nani asijejua kuna utaratibu wa kibenki? Kama una madeni, una vitu vingine, akaunti yako ikafungwa, ni mambo ya BoT na benki ambayo umefungua akaunti. Hayo yanamhusu nini Rais? Kwa hiyo, tunataka kuwaambia Watanzania, utamaduni wa kitu kikifanywa vibaya unajiuzulu, kisiishie kwenye CCM. Vyama vyote viige. Umeongoza chama kikiwa na Wabunge 100, umepigwa uchaguzi, kimepata Mbunge mmoja toka. Onyesha ustaarabu kwamba jamani nimepigwa. Baba bata yule yupo tu; watoto wametumbukia naye mwenyewe katumbukia, bado ana haki ya kusimama. Unasimama kuzungumza nini wakati hapa kijana mdogo tu kamtoa nishai? (Kicheko/ Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, wanasiasa wa namna hii hatuna haja nao. Kuna mmoja nataka nimtumie kombora yuko Ubelgiji, aendelee kukaa huko huko, asitubabaishe. Wamwache Mheshimiwa Samia afanye kazi ya nchi. Asije mtu akamtangulia Rais ooh, Mheshimiwa Rais huyu nataka nikae naye. Ukae naye uzungumze naye kitu gani? Sisi tuko hapa kumtetea Mheshimiwa Samia na tuko hapa kumpigania Mheshimiwa Samia.

Mheshimiwa Spika, Serikali anayoiongoza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ina Wabunge wa kutosha, tutasimama imara kuhakikisha nchi yetu inakwenda. Watanzania wanataka maendeleo, hawataki maneno mengine. Ndiyo maana slogan ya Mheshimiwa Rais sijui kama watu wameielewa vizuri!

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Samia hajasema kuna mabadiliko, kasema kazi iendelee. Maana yake wale walioko kazini waendelee. Anachokisema Mheshimiwa Rais Samia, nidhamu ya wafanyakazi iendelee, nidhamu ya uadilifu kwenye mapato na matumizi iendelee, nidhamu ya uchapa kazi iendelee, reli ijengwe, viwanja vya ndege vijengwe, maji yapatikane, bwawa lijengwe, umeme upatikane, kazi iendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi/Vicheko/Vigelegele)