Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Arusha Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nitumie fursa hii kukushukuru sana kwa kunipatia nafasi ili na mimi kama Mbunge niweze kutoa mchango wangu.
Mheshimiwa Spika, mimi nitajielekeza kwenye mambo mawili. La kwanza tunafahamu kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu leo amewasilisha taarifa yake na kwenye taarifa hiyo ameomba aidhinishiwe fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 116,784,244.
Mheshimiwa Spika, tutakumbuka hivi karibuni Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan aliweza kutoa hotuba elekezi wakati anawaapisha Makatibu Wakuu; hotuba ambayo ilikwenda kukonga nyoyo za Watanzania. Hotuba ambayo ilikwenda kutoa matumaini kwa wawekezaji, hotuba ambayo ilitoa matumaini kwa watanzania wote kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, kabla sijaenda kwenye hoja yangu ya msingi nataka nikumbushe yafuatayo. Tumekuwa na awamu tano na leo tuna awamu ya sita, na utamaduni wetu kama Taifa tumekuwa kila awamu tumeipa nafasi na heshima inayostahili ili iweze kuongoza nchi. Wakati wa Rais Nyerere tulizungumza masuala yanayohusiana na Rais Nyerere wakati wa Rais Mwinyi tulimpa fursa Rais Mwinyi, wakati wa Rais Mkapa, wakati wa Rais Kikwete, wakati wa Hayati Rais Magufuli na sasa tuna awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan lazima tumpe credit anazostahili, lazima tumuunge mkono lazima tutengeneze mambo humu ndani ya kisheria ili yakarahisishe utekelezaji wa mambo kule. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwanza nilikuwa nataka niweke wazi, kwamba lazima Wabunge tukubali kwamba tupo awamu ya sita, na ni vizuri sasa tukaweka mtiririko wa kujenga hoja zetu za kumsaidia Rais wetu kuongoza Taifa.
Mheshimiwa Spika, lakini la pili kwenye kipengele hicho; sisi mpinzani wetu si vyama vya siasa, mpinzani wetu ni changamoto za Watanzania. Leo ukizungumza watumishi wanamanung’uniko kuhusu mishahara yao na kupanda madaraja; kwa miaka mitano hawajapanda madaraja. Leo ukizungumza kuhusu bodi ya mkopo unaona sheria ilikuwa inasema asilimia nane baadaye imekwenda asilimia 15 na kibaya zaidi sheria zote zinazotungwa huwa zinaanzia pale. Sheria yetu ilirudi mpaka nyuma. Watumishi kule wanalia, watu waliosoma vyuo wanalia, lakini hayo mambo yamepitishwa ndani ya Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini ukiangalia pia tuna changamoto kwenye bima afya, tuna changamoto pia kwenye ajira, manung’uniko ni makubwa. Kwahiyo, kazi ya Bunge hili ni kurekebisha sheria kutoa mapendekezo na ushauri ambao Serikali ikiufanyia kazi matumaini yataendelea kudumu kule kwa Watanzania. (makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo; mimi naona hotuba ya Rais wetu Samia Suluhu Hassan tukiifanyia kazi itatusaidi sana kuirahisishia kazi Serikali kwenye masuala mbalimbali. Utaona kila Waziri atakayekuja hapa baada ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, wote watasema mambo yao lakini hatimaye wataomba kuidhinishiwa fedha; hizo fedha zinatoka wapi kama hatukutengeneza mazingira mazuri ya kupata fedha hizo?
Mheshimiwa Spika, mimi nitatoa mapendekezo yangu kwenye sheria nne. Tuna Sheria ya Kazi, Sheria ya Uhamiaji Sheria ya Uwekezaji na tuna Sheria ya Kodi; ziko nyingi, lakini kwasababu muda ni mchache mimi nitazungumzia hizo sheria nne.
Mheshimiwa Spika, ukienda kuangalia sheria ya kazi kwenye Kanuni Kifungu 9(d) tunaambiwa the Employer has provided sufficient evidence from recognize job such mechanism that has been unable to fulfill the particular post due to lack of qualified personnel in the Tanzania labour market. Lakini ukiangalia kanuni hiyo hiyo ya tisa kifungu (9)(2)(d) inasema in the event bulk requitement work permit maybe granted at a ratio of ten local employees to one none citizen employee.
Mheshimiwa Spika, lakini ukienda kwenye sheria hiyo hiyo la labour inakwambia kwamba mwekezaji anapokuja kuwekeza Tanzania atapewa kibali kwa miaka mitano, kama mtaji wake una umuhimu na mkubwa anaweza kwenda hata zaidi ya kumi. Sasa unajiuliza huyu mwekezaji unampa kibali cha kazi mwajiri wake ni nani? na mtu amekuja kuwekeza na yeye pia atakuja kuajiri watu?
Mheshimiwa Spika, ukienda Zanzibar tu hapo wanayo sheria hiyo hiyo pia kama ya kwetu, lakini wao mwekezaji anapata Residential Permit hapati work permit, lakini ukija Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kitu ni kingine.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia pia sheria ya uwekezaji kifungu cha 24 (1) tunaambiwa 24_(1). Every business enterprise granted a certificate of incentives under this act shall be in tinted to an initial automatic in may grand quarter of up to five persons during the startup period.
Ukitaka kuanzisha biashara utapewa watu watano lakini ukiangalia pia sheria ya Uhamiaji kifungu cha; 18 (2) nakuambia 18_2 Resident’s permit shall be issued for any period not exceed three years and may be renewed for any period not exceeding two years by any endorsement of renew endorsed on it by the director but so that the total period of the validity of the original permit and its news shall not in any case exit five year.
Mheshimiwa Spika, ukisoma hivi sheria tatu hazizungumzi utafikiri kila sheria ina nchi yake, sheria ya uwekezaji inakwambia sisi tunakupa incentives ukija kuwekeza Tanzania tutakupa wageni watano, ukienda sheria ya kazi inakwambia sisi ukija kuajiri Tanzania kila ukiajiri 10 tutakupa mgeni mmoja, ukiangalia sheria hiyo hiyo pia labour Kamishna anaambiwa huyo mgeni atakubalika kama hakuna Mtanzania mwenye sifa. Ukiangalia hizi sheria kama vile kila sheria na nchi yake, kila sheria ina dini yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukiangalia nchi kama Kenya leo ukienda pale na Dola yako 100,000 unaruhusiwa pale kufanya uwekezaji na unapata vibali bila urasimu wa aina yoyote, ukienda nchi kama Dubai same case ukienda nchi kama Canada ukipeleka tu Dola 750,000 unapewa kabisa na unaruhusiwa kabisa kukaa permanently, ukienda Uturuki ukinunua nyumba tu kiasi cha Dola 200,000 unarahisishiwa kazi unafanya shughuli zako. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini hakuna kazi ngumu kama kufanya biashara katika nchi ya Tanzania. Tumepata bahati, tumepata Rais mwenye maono, tumepata Rais ambaye amekubali kuwa open minded, tumepata Rais ambaye amewapa nafasi Waheshimiwa Mawaziri mlioteuliwa ili muweze kuja hapa na mapendekezo ya kisheria ili tuweze kufanya harmonization ya sheria zetu, tuwe na sheria moja; mwekezaji asizurure.
Mheshimiwa Spika, mtu kama Dangote kwa mfano kawekeza kiwanda kikubwa sana kule kusini leo akitaka kuja mfano Tanzania eti na yeye pia unamwambia aombe work permit, ili iweje? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi naangalia malalamiko na manung’uniko mengi tunayoyapata nje ya Bunge.
Mheshimiwa Spika, ninakupa mfano. Mimi nilivyokuwa Mkuu wa Mkoa, na ndiyo maana nikagombea Ubunge, kila kitu ninachokiona nikitaka kuingilia kati wananiambia hapana hiyo ni sheria. Sasa ukishakuwa Mkuu wa Mkoa kazi yako ni kusimamia sheria huna uwezo wa kutoa ushauri ndani ya Bunge ya namna ya kubadili sheria.
Mheshimiwa Spika, nikasema nimepata bahati na fursa ya upendeleo kwa Mwenyezi Mungu ya kuingia humu ndani nitoe mchango wangu na maoni yangu. Niombe Bunge lako Tukufu lichukulie very serious jambo hili ili tuweze kubadilisha na kurekebisha sheria zetu. (makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini kwanini nimesema hayo, hapa Serikali ilikuja kuahidi hapa kwenye hotuba ya Rais kwamba tutatoa ajira milioni nane. Ukizungumzia kutoa ajira milioni nane maana yake unazungumzia kila mwaka utatoa ajira milioni 1,600,000, Serikali yetu watumishi wake wa Umma toka uhuru mpaka leo hawajawahi kuzidi 600,000 na mishahara wanayolipwa kwa mwezi ni milioni 660 sasa unajiuliza kama toka uhuru kwa miaka zaidi ya 50 tunaajiri watu 600,000 tutafikiaje target hii ya Milioni nane.
Mheshimiwa Spika, kwa maoni yangu ili tufikie target hii lazima tuweke msukumo na nguvu kubwa sana kwenye private sector. Lazima twende tukafanyie kazi changamoto zote ambazo zimesemwa kwenye private sector humu Wabunge kila siku tumekuwa tunalalamika…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Dakika zako zimekwisha ninakupa dakika mbili umalizie.
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Nilikuwa nasisitiza kwamba tunahitaji kuweka nguvu kubwa sana kwenye private sector, tunahitaji kufanya harmonization ya sheria zetu, tunahitaji pia kujiuliza hivi leo kwanini mtu anamaliza degree anaendesha boda boda? Leo tunatakiwa tujiulize kwanini mwekezaji anang’ang’ania kuja na wageni kutoka nje ilhali Watanzania hapa wapo? na akija pale atamlipa fedha nyingi atamlipia vibali pamoja na changamoto zote, lakini kwanini bado anamuhitaji?
Mheshimiwa Spika, hitimisho langu, naomba Watanzania watuelewe, tunaposema wawekezaji wapewe vipaumbele hatuna maana ya kunyima ajira za Watanzania. Tunasema wapewe vipaumbele kwa sababu tunafahamu kama tukisema mwekezaji ratio yetu ni 1:10 basi anapoajiri watu 10 maana yake 9 watakuwa ni Watanzania au anapoajiri mgeni mmoja 10 watakuwa ni Watanzania. Kwa hiyo, tutakuja na mapendekezo ya sheria ambayo yatawalinda Watanzania lakini pia yatampa amani mwekezaji ili ajira ziongezeke na changamoto iweze kuondoka. (Makofi)
Mheshimwia Spika, la mwisho kabisa sababu muda ni mdogo, sisi Arusha pale tuna kiwanda cha General Tyre kwenye jitihada hizi…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa
Mzungumzaji)
SPIKA: Bahati mbaya muda hauko upande wako Mheshimiwa.
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana.