Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante kuweza kupata nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa ninapenda kuikumbusha Wizara hii mwaka 2017, 2018, 2020 kuja 2021 tulizungumzia suala la bima ya afya kwa wote. Taifa lisilokuwa na watu wenye afya haliwezi kuingia kwenye uchumi wa kati. Taifa ambalo lina wazee wengi waliolitumikia lakini hawana bima ya afya kuwasaidia hatuwezi kuwatendea haki wazee hao waliotumikia Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, lakini taifa lenye watoto wenye siku moja na miaka mpaka mitano wasiokuwa na bima tunawaweka katika matatizo makubwa sana ya kiafya na hatima yake hatuwezi kupata Watanzania ambao watatumia akili zao kwa sababu afya zao zina mgogoro na hawana bima ya afya.
Mheshimiwa Spika, ninaiomba Wizara, kwa sababu Wizara ya Afya ilizungumza kwenye bajeti ya 2017/2018, kwamba wataleta bima ya afya, na wewe ulisisitiza sana; tunaomba tafadhali sana tulete kwa hati ya dharula tuweze kupata bima ya afya kwa wote, maana bila afya kuna mgogoro.
Mheshimiwa Spika, kuna magonjwa ambayo hayaambukizi. Leo hii tuna watu wengi wenye magonjwa ya kisukari, tuna watu wenye magonjwa ya figo, gharama zake ni kubwa sana. Tunaomba Watanzania hawa wawekewe bima ya afya maana ni haki yao ya kimsingi kuhakikisha afya zao ziko salama.
Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie suala la kilimo. Asilimia themanini ya watu na wananchi wa Tanzania ni wakulima, na kilimo ni uti wa mgongo. Ninafahamu na ninamkumbuka Baba wa Taifa kwa kauli mbiu hii kwa Watanzania wote. Leo hii tunapozungumzia kilimo tunategemea kilimo kinachotegemea mvua pekee. Ninaomba, sasa tuna miaka 60 ya uhuru, tunahitaji kuhakikisha kilimo chetu kinakuwa sio kilimo cha chakula pekee kwa maana kwenda mdomoni, tunakataka kilimo cha Biashara.
Mheshimiwa Spika, ninafahamu tuna ekari nyingi sana hapa Tanzania na Watanzania wengi ni wakulima wanaotumia zana za kizamani. Na wale wawekezaji wanaokuja asilimia kubwa wao wanapewa ardhi iliyobora na wao wana mitaji mikubwa kwa sababu walikotoka wanakopeshwa. Watanzania hawakopesheki kwa sababu hawana vitu vya kuweka kama rehani kule benki na hivyo wanabaki kuwa wakulima wa kawaida.
Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wangu wa Mbeya tunafahamu Mikoa mitano ya Mbeya, Ruvuma tukienda na Iringa zile big five ambazo zilikuwa zinasaidia Taifa hili na kulisha nchi nzima leo hii Benki ya Kilimo inayokopesha wakulima ipo Dar es Salaam na wala haipo Mbeya, wala haipo Ruvuma, wala haipo Iringa. Tunaomba tuifanye benki, hii ni benki ya wakulima…
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, taarifa.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA:… wakulima wetu wanalima, leo hii tunalima parachichi, Wakenya wanakuja kununua parachichi…. (Makofi)
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Pokea taarifa Mheshimiwa Kagenda
T A A R I F A
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Spika, napenda kumpa taarifa msemaji kwamba Benki ya Kilimo ipo Mkoani Mbeya pale mjini karibu na Bojan na imetenga mwaka huu bilioni 17.8 kwa ajili ya Mkoa wa Mbeya. Ahsante. (Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika
SPIKA: Mheshimiwa Mwakagenda, pokea taarifa, kumbe huna habari
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ninayo habari, hujo ndiye kaka yangu, Amenye, naomba niendelee.
Mheshimiwa Spika, leo hii mkulima anayelima mchele pale Kyela ambako ni kakangu sasa hivi ametoka kusema, anashindwa kupata mbolea kwa wakati, anashindwa kupata mbolea kipindi cha upandaji wa Mpunga. Anasema habari ya benki kule kwao Mwaya ndugu zake walioko Mwaya hawana hata fedha ya kukopa kwenda kulima mpunga maana kumbuka mpunga wa Kyela ni mpunga bora Afrika hata Nyerere alikuwa anatoa gunia moja la mpunga kwa Wajapan wanatupa gunia kumi leo hii wanakyela hawana hela ya kukopa kwa ajili ya mashamba ya mpunga.
Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia kilimo tunazungumzia pia masoko. Tunalima leo maparachichi ni kweli tunauza sasa hivi Shilingi 1,400 kwa kilo, lakini soko la dunia parachichi moja wanasogeza bei inauzwa kwa bei at least dola moja. Kwa nini Wizara hii ya Kilimo, ndugu yangu Bashe ninaomba utusaidie, kwamba mkulima kutoka shambani asiwepo dalali wa katikati apeleke moja kwa moja Australia akauze na mchumi wa Mtanzania ukapanda. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia masoko, nazungumzia soko la chai, Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuja Wilayani Rungwe; namshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu aliona chai ya Rungwe inauzwa kwa bei ya kuonewa, kwa maana ya kilo Shilingi mia mbili wakati wenzetu wa Njombe wanauza kilo Shilingi mia tano. Mheshimiwa Waziri Mkuu ulifanya kituo chema, unafahamu, ukaweka tume ya kuchunguza kwa nini chai hii inauzwa kwa bei hiyo. Ninaomba Mheshimiwa Waziri Mkuu ukija utupe majibu sisi wana Rungwe na Wanambeya ile tume iliishia wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunazungumzia mifugo, mifugo pamoja na mazao yake, nazungumizia suala la maziwa. Leo hii kule kwetu Mbeya lita moja ya maziwa ni Shilingi mia sita, lakini utashangaa sana maji lita moja ni Shilingi elfu moja, mwekezaji wa maji anapata chanzo cha maji anaweka chupa ya plastiki anauza maji kwa Shilingi elfu moja kwa lita moja. Mkulima wa Mkoa wa Mbeya anauza maziwa kwa Shilingi mia sita yeye mkulima ni mtumwa wa ng’ombe, amkatie majani, ahakikishe anamtunza na madawa yake lita moja Shilingi mia sita. Tunaomba Serikali mtusaidie maziwa angalau yapande bei hata lita moja iwe Shilingi elfu moja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu Ngozi. Leo hii watanzania tuna ng’ombe nyingi lakini ngozi imewekwa zile alama sijui zinaitwaje, zinaondoa ubora wa Ngozi. Ninaomba ng’ombe wetu watafutiwe namna nyingine ya kuwatambua ile hali ya kuwachoma ng’ombe maalama tuipunguze. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niongelee habari ya miundombinu. Mimi nipo kamati ya miundombinu kwa mara ya kwanza nimeona SGR ikiwa imejengwa vizuri, tatizo letu sisi tulikuwa tunalalamika juu ya madeni ya taifa linapokuwa kubwa hatuoni kazi ikifanyika. Safari hii SGR tumekopa na fedha za ndani lakini kazi tumeiona.
Mheshimiwa Spika, pamoja na makofi haya ya furaha tunahitaji kuwajengea uwezo Watanzania kuweza kuitumia reli hii itakapokuwa tayari ili kukuza uchumi wa Watanzania. Ninaomba maeneo yale ambayo reli inapita tuhakikishe tumewawezesha Watanzania wale kujua umuhimu. Si tu hivyo ninaamini reli hii itasaidia yale malori yanayopita kwa wingi hasa njia yetu ya Dar es Salaam, Mbeya, Tunduma ambayo baada ya muda mfupi inaharibika ninaamini sasa watumie reli hiyo iliyotengenezwa ikiwepo SGR lakini na reli ya TAZARA bila kuisahau. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi ninaamini sana kwamba kila kitu kikifanywa kwa makusudi au kwa bahati mbaya tunaomba sana sana utunzaji wa miundombinu hii, tuisimamie kama Taifa kwa umoja wetu. Ninampongeza sana Rais, Rais juzi ameenda kusaini mkataba ule wa Hoima. Tulipitisha sheria kwenye Bunge hili kwamba mkataba wowote ukipitishwa basi uje hapa Bungeni. Mimi ninampongeza sana kwamba at least tumemuona ameenda kusaini na sasa tunasubiri atuletee hapa Bungeni na sisi tujue ni kitu gani kizuri hiki Rais wetu amesaini, tunamsubiri na tunampongeza. Lakini Bungeni lazima mkataba huo pia uje sawa sawa na sheria tuliyoipitisha.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya ninakushukuru sana, ahsante kwa kunisikiliza. (Makofi)