Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nami niwatakie Waislamu wote mfungo mwema wa Ramadhani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimekuwa nikizungumzia sana suala la Serikali kuhakikisha inalipa madeni kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Leo nasisitiza Serikali mlipe madeni kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, hizi pesa siyo zenu nyinyi mnatunza tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jana nilikuwa najaribu kupitia ripoti mbalimbali, ripoti ya BoT imeonyesha 26% ya deni la ndani la Serikali wanakopa kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Ukienda kwenye ripoti ya CAG latest imeonyesha Serikali inadaiwa trilioni 2.7 bado haijalipa. Hapo sijazungumzia yale madeni ya kurithi ya kabla ya ile Sheria ya mwaka 1999 Serikali kuamuru madeni yalipwe wakati hakukuwa na michango. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hata mnapokopa kopeni kulingana na taratibu zilizowekwa na mifuko. Nitolee tu mfano Mfuko wa Bima ya Afya, Serikali ilikopa shilingi bilioni 220 kwenye sekta mbalimbali ikiwepo Wizara ya Mambo ya Ndani, 60% ya huo mkopo ambayo ni shilingi bilioni 132 walikopa hakuna makubaliano yoyote ya kimaandishi wala hakuna riba. Sheria Na. 5, kifungu kidogo cha (1)(f) cha Sera ya Uwekezaji wa Mifuko ya mwaka 2020 imeeleza bayana kwamba Serikali ikikopa ikope kibiashara na ilipe riba. Msipolipa riba mnachangia mifuko kukosa mapato, hilo hamfanyi. Hii ni kinyume kabisa na lengo kuu la mifuko kwa mujibu wa kifungu cha 33 cha Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2015. Kopeni, lipeni na fuateni taratibu. Hii ilishajitokeza hata kwenye mkopo wa UDOM kipindi hicho, mmechukua pesa kule hamkuingia mkataba, mkataba mkaingia baadaye, tuache! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala ambalo ni muhimu sana kwa wafanyakazi. Tumeliahirisha, liliwekwa kiporo baada ya sintofahamu iliyotokea mwaka 2018, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli akaingilia kati akasitisha kunyonya wafanyakazi kwa kikokotoo kibovu ambacho tulizungumza kwenye Bunge hili. Nimeona kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ukurasa wa 60 ameligusia kidogo lakini hawajasema bayana ni lini suala hili mtalitatua kisheria kwa kuleta mabadiliko Bungeni ili yale wanayoyataka wafanyakazi; kikokotoo chao kilichobeba hatma ya maisha yao baada ya kutumikia Taifa hili kwa jasho na damu kiwe cha neema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuliwaambia mwanzo kikokotoo hiki mkiweke kwenye sheria kisiwe kwenye Kanuni ya Waziri hawakutusikia na hawakushirikisha wadau matokeo yake wakaleta kikokotoo kibovu cha 1/580 kuliko hata kile kilichokuwa mwanzo cha 1/540. Tulitegemea kingekuwa chini ya 1/540 basi hata ingekuwa ya 1/520 kama walivyokuwa wamependekeza awali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo mstaafu anastaafu unamwambia ile full pension unampa 25%, asilimia 75% utamlipa kidogo kidogo, haiwezekani kumpangia mtu pesa zake. Yeye mwalimu anayelipwa pension yake labda milioni 40 umlipe 25%, 25% ya milioni 40 akajenge, anasomesha huyo huyo mwalimu, bado hajaweka sawa mazingira mmeyaweka mabovu. Haiwezekani kwa nini tuwapangie mbona nchi za wenzetu wanachukua 50% wengine 75%, 25% siyo sawa kwa wafanyakazi wa Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia michango haipelekwi, sasa hivi wastaafu wengi hawalipwi. Ukienda huko Mbeya utasikia kilio hicho hicho, Bunda na maeneo mengi hawa Wabunge wanajua wastaafu hawalipwi na hawalipwi kwa sababu michango maeneo mengi haipelekwi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano tu NSSF michango ya wanachama ya shilingi bilioni 284 mwaka mzima haijakusanywa. Ukienda pale Bima bilioni 24, ukienda Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi milioni 116 ziko nje wastaafu watalipwaje? Serikali hailipi madeni na michango haikusanywi, siyo sawa! Hizi pesa siyo zetu ni za watumishi wa nchi hii, tuwape morale, tuwarudishie kikokotoo chao, tukusanye michango yao ili wastaafu wetu wawe na uhakika wa kulipwa kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia miaka mitano hawa watumishi sisi tunapanga mambo hapa wanaenda kuyatekeleza kwa kinyongo, five years hatujawapandishia mishahara. Wana stress ya kupandishiwa mishahara, wana stress ya kikokotoo kibovu, wana stress ya pesa Serikali wanachukua kwenye mifuko yao hawalipwi, wana stress wenzao wanaostaafu hawalipwi kwa wakati, wao waliokuwa kwenye utumishi hawajui hatma yao itakuwaje, siyo sawa! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala hili Mheshimiwa Hayati Rais JPM alisema, hivi sisi Wabunge tukimaliza tunapewa kitita chetu, hawa ambao tunatunga mambo yetu humu ndani wanaenda kuyatekeleza unawapangia 25%. Tutekeleze kazi hii kwa uadilifu, Mungu atulipe tuache legacy ya kuwatetea wafanyakazi wa Taifa hili ambao wanashinda usiku na mchana kutekeleza hiyo miradi mnayojivunia leo kwamba imetekelezwa, siyo ninyi ni hawa ambao mazingira yao ya kazi, hatma ya kiunua mgongo chao ni mabovu, tutimize wajibu wetu. Tulinde Taifa letu kwa kuhakikisha haki za wafanyakazi zinakuwa nzuri. Ahsante sana. (Makofi)