Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ndanda
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa namna ya pekee kwa kunipa nafasi ya kuchangia leo ambayo ni siku ya pili ya mjadala wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, nianze kwa kutoa shukrani kwako wewe mwenyewe, Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu na Waheshimiwa Wabunge wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Mtwara wakiongozwa na Mheshimiwa Chikota, viongozi wa chama na Serikali wa Mkoa wa Mtwara, mikoa ya jirani na majimbo Jirani, wananchi wote wa Jimbo la Ndanda na majimbo jirani, kwa namna ya pekee walivyoshiriki kwenye msiba wa mke wangu mpendwa Beatrice na walivyotupa faraja. Ahsanteni sana, nawashukuru. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimerudi hapa kuendelea kufanya kazi zangu nilizotumwa na wananchi wa Jimbo la Ndanda na nimesimama ili nami niweze kuchangia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikiliza vizuri sana Hotuba ya Waziri Mkuu, nami nimeamua kuchagua maeneo manne au matano hivi ambayo ningependa nichangie kwa sababu ndiyo yanagusa Watanzania na wakazi wa Ndanda. Sehemu ya kwanza kabisa ni suala la kilimo; nitatumia hapo muda mrefu kwa sababu nataka kuona wananchi wale, wakazi wa Ndanda na Watanzania ambao ni zaidi ya asilimia 75 wanapata manufaa kutokana na kazi za mikono yao na kazi zao za shambani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu ameongea suala la umeme, nami nitachangia hapa pia masuala ya afya na masuala ya barabara na mwishoni mambo mengine ya mtambuka kwa ujumla. Kwenye suala la kilimo, nimefanya mazungumzo kwa kina na Naibu Waziri, Mheshimiwa Bashe na kujaribu kumweleza mambo yanayotusibu sisi wakulima na hasa wakulima wa Korosho kwenye sekta hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwakumbushe tu Wabunge wenzangu wote kwa ujumla kwamba, mtakumbuka katika mazao makubwa matato yanayotajwa kimkakati ni pamoja na korosho, lakini kwa masikitiko makubwa sana, mwaka 2020 uzalishaji wa Korosho ulipungua msimu uliopita kutoka msimu ule wa mwanzo. Mwaka 2020 tulipata tani 205 tu, wakati msimu uliofuatia nyuma ulikuwa ni tani 330. Hii imetokana na kutokutimiza wajibu wetu sawa sawa kwenye kuwasaidia wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo ambalo naiomba Serikali ifanye sasa; na tumesikia hapa na kupata majibu kwamba kuna mkakati mzuri kabisa ambapo Serikali inakwenda kununua pembejeo kwa pamoja na kuzigawa kwa wakulima ili ziweze kuwafikia kwa wakati na vile vile tunaamini zitakuwa na ubora unaotegemewa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana na nimsisitize sana Mheshimiwa Hussein Bashe, kama mpango huu umepangwa na Serikali, basi utimizwe kama vile ambavyo mmekusudia ili kuweza kuongeza uzalishaji wa korosho. Inasikitisha kuona wafanyabiashara wanajinufaisha sana inapofika misimu ya wakulima kuweza kupata pembejeo pamoja na virutubisho vingine ambavyo vinatumika kwenye mikorosho.
Mheshimiwa Naibu Spika, msimu uliopita na misimu mingine huko nyuma tumeshuhudia sulphur ikiuzwa mpaka kati ya shilingi 35,000/= mpaka shilingi 50,000/= kwenye maeneo mbalimbali, jambo ambalo ni baya sana kiasi kwamba wakulima walikuwa wanashindwa kununua na kuhudumia mikorosho yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tumefurahi kuona nia njema ya Serikali hii ya Awamu ya Tano na Awamu ya Sita kwamba ambapo wanatuahidi kwamba bei za sulphur sasa itapungua mpaka kufikia shilingi 29,000/=, tena zitatolewa kwa wakulima kwa njia ya mkopo ambayo baadaye mnunuzi atachangia kiasi na mkulima naye atakatwa baada ya kuuza korosho zake. Hii itawasaidia sana kwa sababu tutajiondoa kwenye ile mikopo mikubwa iliyoko kwenye mabenki ambayo ilikuwa na tozo kwa riba kubwa kiasi kwamba wakulima walikuwa hawanufaiki na hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba pia Wizara ya Kilimo waboreshe na mifumo ya ununuzi wa Korosho, wasimamie vizuri sana masuala ya ushirika kwa sababu ndiyo yanayoumiza wakulima kila mara. Pia tuboreshe na ule mnyororo mzima wa zao la Korosho, tusiishie tu kununua Korosho; na kila mara nimekuwa nalisema hili jambo ndani ya Bunge hapa, japokuwa wengine hawataki kulielewa sana, kwamba unapovuna Korosho magunia 100 unapata pia na Kochoko au mabaki ya korosho, yale mabibo; na yenyewe unaweza kupata takribani gunia 75 mpaka gunia 100, zinakaribiana. Hizi kule kwetu kila mara nimesema, tunazitumia kupika gongo. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaambie Waheshimiwa Wabunge, ninachokiomba sasa, Serikali warasimishe na kurekebisha haya mambo, kwa sababu hatuwezi kuyakwepa. Tumeishi namna hiyo, sasa isiwe tena tunasema ni pombe haramu kabla hatujawaeleza ili iweze kuwa halali, nini kifanyike? Nia nzuri ya Wizara iwe ni kuona wakulima wananufaika na mazao yao ya shambani kama wanavyonufaika wakulima wa mazao mengine kwenye maeneo mengine; wakulima wa Kahawa, wakulima wa Miwa na wenyewe wote wananufaika na wanapata mazao makubwa na faida kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni suala la umeme. Nimemsikia hapa Mheshimiwa Waziri Mkuu anasema, mpaka sasa kuna vijiji takribani 1974 na ninamwomba sana Mheshimiwa Waziri naye tulikuwa tukiongea mara nyingi kwamba kwenye Jimbo Ndanda mpaka sasa kuna vijiji 29 ambavyo havina umeme kabisa na hasa zaidi kuna Kata mbili ambazo na zenyewe hazina umeme kabisa; Kata ya Msikisi pamoja na Kata ya Mpanyani. Naomba mfanye kwa haraka sana kuhakikisha vijiji hivi vinapata umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri; na haya mambo yapo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Kama ambavyo kila mara nimesema, nimefurahi sasa kusimama hapa nikiitetea Ilani ya Chama cha Mapinduzi, achilia mbali sera zetu na mambo mengine, lakini nataka nione ilani hii inatekelezwa na sisi tusimame kwa kifua mbele kwamba ilani yetu imetekelezwa katika eneo letu na watu wa Ndanda nao wajivunie kwamba wamepata sasa msimamizi kwa ilani inayotekelezwa na Serikali hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye masuala ya afya, nawaomba sana Waziri wa afya na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba tuhakikishe sasa Hospitali ile ya Kanda ya Mtwara inamaliziwa ili wananchi wale waweze kupata huduma. Sasa hivi tunatumia Hospitali ya Ndanda ambayo watu wengi wanailalamikia kwamba ina gharama kubwa sana kwenye kutoa huduma. Nami nataka niwaambie, ukubwa wa gharama huu ni kwa sababu ya uhaba wa Vituo vya Afya vilivyopo kwenye maeneo haya. Kwa mfano, wakazi wa Ndanda walijitahidi sana kujenga boma lao kwa ajili ya Kituo cha Afya, limekamilika mpaka kufika level ya lenta katika Kata ya Mpanyani, Kata ya Mihima na Kata ya Namajani na kwenye maeneo mengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba badala ya kuwafanya watu wa Ndanda wakatibiwe kwa gharama kubwa kwenye Hospitali ya Mtakatifu Benedict ya pale Ndanda Mission, basi sasa tukamilishe kujenga kile Kituo cha Afya kilichopo pale ili gharama ziweze kupungua na pia tuwapunguzie adha ya kusafiri safari ndefu ya kwenda Jimbo la Ruangwa huko kwenye Kijiji cha Nandanga kwenda kupata matibabu jambo ambalo siyo zuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nisisitize pamoja na lile suala la korosho ni suala la barabara. Kwa kipindi kirefu sana tumekuwa na tatizo kubwa sana la barabara. Kuna hii barabara ambayo sijasikia kila mara inatajwa, lakini ni introduction ya barabara inaitwa Cashewnut Ring Road. Barabara hii inaanzia Nangurukuru – Liwale – Ruagwa – Nachingwea – Masasi – Newala – Nanyamba - Mtwara yenye wastani wa kilometa kama 400. Naomba sana, ili bandari yetu iweze kutumika vizuri, basi tuhakikishe hii barabara tunaikamilisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi uliyonipatia na ninawashukuru sana vijana wa Bunge wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)