Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. January Yusuf Makamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bumbuli

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. JANUARY Y. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikushukuru kwa nafasi uliyonipa ya kutoa mchango na mimi katika hoja iliyoko mezani, namshukuru Mungu kwa neema zake na baraka zake za afya na uhai na leo tumeuanza mwezi Mtukufu wa Ramadhani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa naongea mara ya kwanza tangu uchaguzi uishe, napenda kuwashukuru wananchi wa Bumbuli kwa heshima waliyonipa ya kuendelea kuwa Mbunge wao. Nampongeza pia Mheshimiwa Spika, wewe Naibu Spika, Wabunge wote waliochaguliwa na wananchi kwa kuaminiwa na dhamana hii kubwa na muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza wetu mpya Mheshimiwa mama Samia Suluhu Hassan kwa kushika hatamu za uongozi wa nchi yetu. Nampongeza ndugu yangu Dkt. Philip Mpango kwa kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais, nawapongeza Mawaziri wote kwa imani ambayo Marais mawili wameonyesha kwao na tunawatakia heri na baraka wakifanikiwa katika kazi zao nchi yetu na sisi imefanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina mambo mawili napenda kuyazungumza leo siku ya leo. La kwanza ni mambo ya Jimboni kwangu Bumbuli; mambo ya barabara, umeme, kiwanda chetu cha chai na kadhalika na la pili ni suala zima la umoja, mshikamano, utulivu na upendo miongoni mwetu na nitaanza na hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe pole za dhati kabisa kwa sababu tunaelekea mwisho wa arobaini kwa Watanzania kwa kuondokewa na kiongozi wetu jasiri na shupavu Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. Pole zaidi kwa familia hasa mama Janeth na Watoto. Msiba huu umetuingiza katika kipindi cha mpito ambacho hatukukitarajia na mpito siku zote una mashaka, wasiwasi, hofu, mshtuko na huzuni. Kwa hiyo wananchi kote waliko wana hayo mambo ya hofu, shaka, mshtuko, huzuni na wasiwasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi ambacho Watanzania wanahitaji uongozi wetu, sisi ambao ni viongozi, ni sasa. Bahati nzuri Mheshimiwa Rais wetu mpya ametoa kwa kauli zake na vitendo vyake, ametoa mwelekeo mpya ambao unaleta matumaini mapya ya kutupunguzia huzuni, mashaka, mshtuko na wasiwasi. Mwelekeo alioutoa Mheshimiwa Rais una sehemu nne: Ya kwanza ni kupunguza maumivu ya jeraha la msiba; sehemu ya pili ni kutuunganisha Watanzania; sehemu ya tatu ni kuendeleza mema na mazuri aliyofanya Rais wetu aliyepita; na sehemu ya nne ni mwelekeo alioutoa Mheshimiwa Rais ni kufanya maboresho, marekebisho na mabadiliko pale panapostahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama leo kwa heshima na tahadhima mbele ya ninyi viongozi wangu kutoa wito wangu kwamba nasi tujielekeze huko katika mwelekeo huo huo ambao ameutoa Mheshimiwa Rais. Kipindi ambacho nchi yetu inahitaji umoja, utulivu na mshikamano ni sasa. Kkauli za utengano, kauli za kutiliana shaka, kauli za kutuhumiana, kauli za kuhukumiana, hazijengi na zinawachanga wananchi. Mambo makubwa aliyoyafanya Rais wetu aliyepita Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli hayatafutika, hayatafutwa, hayatapotea na hayatapotezwa kwa kauli yeyote ya kubezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa wale miongoni mwetu ambao wanatoa maoni na ushauri wenye nia njema wa kuweka mambo sawa, wa kuyatengeneza vizuri, wasibezwe, wasihukumiwe katika dhamira zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, dhamira ya kauli na ushauri na maoni ipo ndani ya moyo wa mtu. Mtu anaposifu kwamba mama Samia ameanza vizuri asihukumiwe kwamba anatafuta cheo, anapokosoa isionekane ni nongwa na anapokaa kimya isionekane amesusa. Naomba sana tusihukumiane katika dhamira za kauli na vitendo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi aliyotufanyia Rais Dkt. Magufuli naweza kuichukulia kama vile ametushonea nguo nzuri kabisa ya kupendeza, akitokea mtu akaona kwamba ile nguo kuna uzi umejitokeza tuukate, isionekane dhambi; akijitokeza mtu akasema katika hii nguo kifungo kimelegea hebu tukiweke vizuri, isionekane huyo mtu ni msaliti. Mtu huyo anapofanya kazi hiyo ya kukaza kifungo au kukata uzi, nguo ikapendeza, bado sifa ni ya mshonaji. Kwa hiyo, naomba sana kwa sababu dalili nilizoziona sio nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema kwamba sisi kama viongozi tunayo haki na wajibu wa kutoa maoni kuhusu mambo yetu yaendeje, lakini njama, vikundi, vigenge vya kuweka mashinikizo kwamba kipi kifanyike, hatua zipi zichukuliwe, zipi zisichukuliwe, si sawa kabisa na haitujengei umoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, uongozi wa nchi ni jukumu kubwa na la kihistoria, Rais wa nchi yetu ana madaraka na nguvu na mamlaka makubwa sana na kwa vyovyote vile katika uongozi wake anaacha alama. Mwalimu Nyerere ameacha alama, Mzee Mwinyi ameacha alama, Mzee Mkapa ameacha alama, Kikwete ameacha alama na Rais Dkt. Magufuli ameacha alama, ndio asili ya urais. Sasa wajibu wetu sisi kama viongozi tuliopo ni kulinda yale mema ambayo viongozi wetu wameyafanya kuanzia wakati wa Mwalimu, mpaka Rais Magufuli.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tupiganie kuyalinda yaliyofanywa na Rais Magufuli, lakini tusipigane wakati tunafanya hivyo. Tukipigana kwa mambo ya nyuma, tutashindwa kupigania mambo mazuri ya mbele ambayo Rais mpya anataka kuyafanya. Vikumbo vya nani ni mnazi zaidi wa Rais Dkt. Magufuli, nani mnazi zaidi wa Rais Samia na viwiko vikali ambavyo watu wanataka kupigana havisaidii wala kujenga. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa, kengele ya pili imegonga.

MHE. JANUARY Y. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba upendeleo wa dakika tatu nimalizie.

NAIBU SPIKA: Hapana, majina ninayo mengi sana hapa mbele, ahsante sana.

MHE. JANUARY Y. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa na makubwa mbeleā€¦

NAIBU SPIKA: Ahsante sana.

MHE. JANUARY Y. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kusema kwamba tuheshimiane, tusihukumiane na tumsaidie kiongozi wetu, tuwe na umoja na upendo kwa sababu utulivu ndani ya Bunge ndio utasaidia kiongozi wetu atawale vizuri. Ahsante sana. (Makofi)