Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kwimba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SHANIF M. JAMAL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana umenipa nafasi na mimi nichangie hoja iliyo mbele yetu. Kwanza kabisa, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema niweze kusimama kwenye Bunge lako Tukufu nichangie hoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, naomba nitoe pole kwa Mama Janet Magufuli, watoto, familia na Watanzania wote ambao tumepata msiba mkubwa wa kuondokewa na Rais wetu wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. Nichukue nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu na Kamati yake ya Mazishi kwa kutenda haki kumpa heshima zote ambazo Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alilikuwa anastahili, tangu siku ilipotangazwa…
T A A R I F A
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mansoor, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Esther Matiko.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nafikiri wote tunajua kwamba tumepewa dakika chache, dakika tano, dakika saba. iti chako kilishatoa mwongozo kwamba kutoa pole na pongezi tushafanya kama Bunge hapa ndani wasifanye repetition. Sasa kama Mbunge anaona dakika ni nyingi kwake atupunguzie wengine walau tuweze kuchangia kwa manufaa ya Taifa hili. Ahsante. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, ni kweli, niliwasomea Kanuni hapa, nadhani ni Kanuni ya 175, naomba tuipitie Kanuni hiyo inasema nini kwa sababu wakati ule nilieleza kwa kirefu, Mbunge ambaye anaanza moja kwa moja kwenye hoja tunaweza kupeleka ujumbe huko nje kama hajali hivi ama yeye hataki kutoa pongezi au hataki kutoa pole lakini huyo ndiye atakayekuwa anafuata Kanuni zetu zinavyosema. Kwa hiyo, tukitaka kuzungumza hayo tutafute hoja ambayo hayo tunaweza kuyasema kwa namna tofauti kuliko kuzisema moja kwa moja kwa sababu Kanuni tuliyotunga wenyewe hii hapa 175 inatutaka tufuate utaratibu huo. Karibu umalizie mchango wako Mheshimiwa Shanif Jamal.
MHE. SHANIF M. JAMAL: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naongea kwa niaba ya wananchi wa Kwimba na hapa ndiyo sehemu ya kusema pole kwa wanafamilia.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Shanif tuelewanie vizuri, humu ndani kila mtu ni mwakilishi wa watu fulani lakini Kanuni tulizozitunga zinasema hivyo, kwa hiyo tufufate tu Kanuni , endelea na hoja yako. (Makofi)
MHE. SHANIF M. JAMAL: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee na hoja kwamba siku ya msiba wakati mazishi yalikuwa yanafanyika Kitaifa Dodoma, nakata Bunge hili litambue kwamba watu takribani bilioni 4 walikuwa wanafuatilia kwenye runinga mbalimbali mazishi ya Rais wetu Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. Maana yake ni kwamba Rais wetu alikuwa anapendwa na watu wengi sana ulimwenguni, ni Rais wa kipekee, ni Rais wa mfano. Kwa hiyo, mimi nimeona ni vema niseme hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia wananchi wa Jimbo la Kwimba tunamshukuru sana Rais wa Awamu ya Tano kwa mambo makubwa mengi ambayo amewafanyia wananchi wa Tanzania. Niseme machache tu, la kwanza ametupa elimu bila malipo, wananchi wa Kwimba tunamshukuru sana, watoto wetu wanakwenda shule mpaka sekondari bila malipo. La pili, nataka nishukuru SGR inayojengwa itapita kwenye Wilaya ya Kwimba, italeta uchumi kwenye maeneo yetu, mambo ni mengi ametufanyia Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano. Pia ametoa heshima kwa Machinga, wafanyabiashara wadogo wadogo miaka hii mitano hawasumbuliwi, hawakimbizwi wana heshima. Hii heshima yote ametuletea Rais wetu wa Awamu ya Tano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii pia kumpongeza Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuapishwa kwa Mujibu wa Katiba kuwa Rais wetu wa Awamu ya Sita. Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan ametoa hotuba mbalimbali za maelekezo. Hotuba aliyotoa siku ya kuapishwa Mawaziri aliongea takriban dakika 87 na kuendelea, alikuwa anatoa maelekezo kwa kila Wizara, hiyo ilikuwa ni hotuba ya darasa. Naomba hotuba hiyo ingeletwa hapa Bungeni ikatusaidia wakati tunachangia Wizara ili tuendane na maelekezo ambayo Rais wetu mama Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametoa kwa Wizara mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii pia kuongea kuhusu hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Naomba niseme mambo machache. La kwanza, Jimbo la Kwimba tumekuwa na miradi mingi ya maji ambayo imetekelezwa na imeshamalizika, lakini tatizo kubwa tulilonalo, tumejengewa tenki la lita milioni mbili la maji ambalo linategemewa maji yatoke Ziwa Victoria yapande juu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo letu ni kwamba bomba linaloleta maji kwenye hilo tenki limeharibika siku nyingi, leo ni takribani miezi sita. Tenki limekamilika la lita milioni mbili ili litoe huduma kwa wananchi wa Mji wa Ngudu na maeneo mengine, leo maji hayajafika, wananchi wa Jimbo la Kwimba wanateseka kwa maji, kwa sababu ya bomba hilo limeharibika. KASHWASA, wameshapeleka maombi kwenye Wizara ya Maji kuomba wasaidiwe ili waweze kukamilisha. Nina imani na Mheshimiwa Waziri Aweso, kilio chetu ameshakisikia, tunaomba atusaidie wananchi wa Kwimba wapate maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni suala la barabara. Tuna barabara ya lami ya Hungumarwa - Ngudu - Magu, sasa ni miaka mitano barabara yetu tayari imeshafanyiwa upembuzi yakinifu, lakini hatujui lini Wizara ya Ujenzi itatangaza hiyo barabara. Tunaomba tupate mwelekeo, Wizara ya Ujenzi ituambie lini itatangaza?
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Ahsante sana. (Makofi)