Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lupa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili nami nichangie hoja iliyo mbele yetu.
Kwanza, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Lupa waliokichagua chama changu kwa kura nyingi sana, kuanzia Rais, Mbunge na Madiwani, kura nyingi sana nawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema na kama alivyosema Mheshimiwa Rais, hatutawaangusha. Uchaguzi umekwisha, sasa iliyobaki ni kufanya kazi, ni kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, ni kutekeleza ahadi ambazo wagombea tuliahidi kwenye
majukwaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimboni kwangu kuna genge limeibuka linaeneza uongo kwamba barabara ya lami kutoka Chunya kwenda Makongolosi aliyoahidi Mheshimiwa Rais haitajengwa! Eti haitajengwa kwa sababu kuna watu wamekula hela na hao watu wamekimbilia nje ya nchi!
Mheshimiwa Naibu Spika, wale ni waongo, ni watu ambao kwenye uchaguzi walishiriki na walikuwa wanatamba kwamba wangeshinda kwa kishindo! Wameshindwa kwa kishindo! Wanashindwa pa kutokea, wanaeneza uongo! Hilo wananchi wa Lupa ni jipu, mtajua namna
ya kulitumbua wakati ukifika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiangalia Hotuba ya Mheshimiwa Rais nalinganisha sana na maneno, yaani nikiangalia hotuba yake na matendo yake, nalinganisha sana na maneno na matendo ya Yohana Mbatizaji zaidi ya miaka 2000 iliyopita. Kwa ruhusa yako, naomba nisome
paragraph moja aliyosema Yohana Mbatizaji kwenye Injili ya Luka 3:7-14. Siyo maneno yangu haya, maneno ya Yohana Mbatizaji:
“Basi aliwaambia makutano ya wale waliomwendea ili awabatize. Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja? Basi toeni matunda yapatanayo na toba, wala msianze kusema mioyoni mwenu tunaye baba, ndiye Ibrahimu, kwa maana nawaambia kwamba katika mawe haya Mungu aweza kumuinulia Ibrahimu watoto. Na sasa hivi shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti na kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.
Makutano wakamuuliza, tufanye nini basi? Akawajibu akiwaambia, mwenye kanzu mbili na ampe asiye na kanzu na mwenye vyakula na afanye vivyo hivyo. Watoza ushuru nao wakaja kubatizwa wakamuuliza, Mwalimu tufanye nini na sisi? Akawaambia, msitoze zaidi kitu zaidi
kuliko mlivyoamriwa. Askari nao wakamuuliza wakisema, na sisi tufanye nini? Akawaambia, msidhulumu mtu wala msishtaki kwa uongo tena mtoshewe na mishahara yenu.”
Mheshimiwa Naibu Spika, haya maneno ni ya miaka 2000 iliyopita! Ni maneno ambayo yako kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Rais Magufuli, yanafanana; anawaambia Watendaji wa Serikali, Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, wote timizeni wajibu wenu, vinginevyo shoka liko shinani. Mti usiozaa matunda utakatwa! (Makofi)
Sasa msianze kulalamika, aah mimi, hapana! Timizeni wajibu wenu. Yohana Mbatizaji alikuwa anawaambia hawa, ili warithi Ufalme wa Mbingu. Mheshimiwa Rais Magufuli anawaambia Watendaji wa Serikali ili tuondoe umasikini kwa Watanzania, ili tulete maendeleo kwa Watanzania. Kwa hiyo, timizeni wajibu wenu, vinginevyo shoka liko shinani, mti usiozaa utakatwa na kutupwa motoni. Ninaomba hotuba hii hasa pale kwenye vipaumbele ambavyo ameweka Rais, Serikali mhakikishe Wakuu wa Mikoa wanayo, Wakuu wa Wilaya wanayo, Watendaji wanayo waangalie Rais ameweka vipaumbele gani kwenye hotuba yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hotuba hii anasema wakulima na wavuvi, hasa wakulima, wataletewa pembejeo kwa wakati, watawekewa huduma za ugani, watatafutiwa masoko panaposumbua! Jimboni kwangu mwaka uliokwisha wakulima wa tumbaku wamesumbuka sana, soko la tumbaku halipo. Naomba sana Mheshimiwa Waziri wa Kilimo hili ni jipu lako la kwanza, uhakikishe wakulima wa tumbaku wa Jimbo la Lupa na hasa nchi nzima, watafutiwe soko la zao lao kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, iko nchi ya Zimbabwe ambayo yenyewe imeingia ubia na Jamhuri ya Watu wa China kwamba tumbaku yote ya Zimbabwe inanunuliwa na China. Unajua Wachina wako wengi sana, wako watu 1.6 billion kwa hiyo, chakula kinahitajika kingi, vinywaji
vingi, hata tumbaku ya kuvuta inahitajika nyingi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, naomba jipu hili ulishike vizuri ili wakulima wa tumbaku wa Jimbo la Lupa na nchi nzima mwaka huu wapate soko la uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Hotuba hii ya Mheshimiwa Rais aliongea kwamba anataka kuleta Muswada Bungeni kubadilisha vipengele fulani vya Sheria ya Manunuzi, ili iharakishe, ilete unafuu wa kuleta huduma kwa Watanzania. Nawaambia wadau wote, nimeongelea Sheria ya Manunuzi miaka 10 Bungeni hapa kwamba jamani eeh, bajeti yetu inatakiwa ni trilioni 20! Ujue kwamba 70% ya hela hizo inaenda kwenye manunuzi! Sasa mkiona Rais mwenyewe wa nchi ameshtuka anasema tuongelee manunuzi, muichukulie very positively watendaji wote, ili mlete mapendekezo mazuri ya kuirekebisha sheria hiyo, ili iweze kuharakisha kupeleka huduma kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, pale ambapo muda wa tender ni siku 60, kwa nini, inachelewesha kupeleka huduma kwa Watanzania. Pale ambapo tender sum ya kujenga barabara kutoka hapa kwenda Iringa ni shilingi milioni 200, lakini variations zinazotolewa hapo inafika milioni 600, ni vitu vya kuviangalia hivyo. Pale ambapo Mtendaji au Accounting Officer kwenye Wizara, kwenye Idara, anasema ikifika shilingi milioni 50 lazima akapate kibali kwa Accountant General! Hilo ni la kuliangalia, ili hiyo nayo threshold iongezwe kutoka milioni 50 iende 500 au bilioni moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, sera ya magari; nimesema sana Serikali iwe na sera ya magari. Kuwe na sera ya magari siyo kwamba huyu ananunua hili, huyu ananunua hili, hapana, kuwe na sera ya magari kabisa. Kenya, Rwanda, Zambia na Malawi wana sera ya magari!
Kwingine kote kuwe na Sera ya Magari! Hiyo Sera mkiiandika vizuri na mkaitia kwenye Sheria, kuna kitu Watendaji wa Serikali wanafanya sana hapa, una-acquire property ya Serikali by tender, lakini sasa katika kui-dispose sheria inasema u-dispose by tender! Magari wanajiuzia!
Hiyo naomba isimamishwe kwenye mapendekezo ambayo yataletwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, mwaka jana Serikali yetu nzuri ilitangaza kupitia kwa Rais na kwa Waziri Mkuu kwamba Mkoa wa Mbeya utagawiwa kuwe na Mkoa wa Songwe na wa Mbeya na kwamba Wilaya ya Chunya itagawiwa kuwe na Wilaya mbili; Wilaya ya Songwe na ya Chunya. Namwomba sasa Mheshimiwa Simbachawene atekeleze ahadi hiyo haraka, ili kila Wilaya katika hizo Wilaya mbili itengeneze Halmashauri yake ili kuharakisha kuwapelekea huduma wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, kuna kitu kinanisumbua sana, kinanisumbua kweli, consistency! Nimeshindwa namna ya kusema Kiswahili, consistency! Wakati wa mjadala wa kusema Jamhuri yetu ya Tanzania tuwe na Serikali ngapi, mbili, tatu! Wanasema aah, hapana,
Zanzibari bwana wakae mbali kule, wakae mbali! Hapana, hapana, kuwe na Serikali yao huko! Sawa bwana! Wakati wa uchaguzi, wanasema aah, wale ndugu zetu bwana, lazima tuwasaidie wale, consistency! Nakushukuru sana. (Makofi)